Mombasa. Msanii wa Bongo Fleva, Sefu Shabani Ramadhan maarufu Matonya, ameachiwa kwa dhamana baada ya kukaa rumande kwa zaidi ya siku 20 katika gereza la Shimo La Tewa lililopo Mombasa, Kenya, kufuatia tuhuma za ubakaji.

Matonya aliachiwa jana Jumanne, Aprili 28, 2026 baada ya kukamilisha masharti ya dhamana yaliyowekwa na Mahakama ya Shanzu Aprili 9, 2026.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Aprili 29, 2026, rafiki yake, Rashid Naaman amesema Matonya aliachiwa jana kwa dhamana.

“Ndiyo, ameachiwa. Alitoka gerezani jioni ya Jumanne,” amesema.

Msanii huyo amechapisha video katika mtandao wake wa Insta akisema anamshukuru Mungu na Watanzania kwa maombi yao baada ya kuachiwa kwa dhamana.

“Namshukuru Mungu nimepata dhamana ya kuwa nje katika mahakama ya Kenya lakini pai niwashukuru Watanzania wote kwa dua na maombi pamoja na Wakenya wote,” amesema Matonya.

Kuhusu tuhuma zinazomkabili, amesema hawezi kulizungumzia kwa sababu lipo mahakani huku akiomba atolewe kwenye hizo siasa.

“Siwezi kulizungumzia maana lipo kwenye maakama, lakini naomba wanitoe kwenye hizo siasa za masuala ya ubakaji hilo jambo sio na wote waliopanga wanajua wenye walichokipanga kwa ajili ya maslahi yao,” ameongeza.

Awali, msanii huyo alifikishwa mahakamani akituhumiwa kwa ubakaji shtaka ambalo alikana. Mahakama ilimruhusu kuachiwa kwa dhamana ya Sh500,000 za Kenya (Sh10 milioni), ikiwa ni pamoja na masharti ya kuwasilisha pasipoti yake mahakamani na kutokutoka nje ya eneo la mamlaka ya mahakama bila kibali.

Aidha, mahakama iliagiza mamlaka za uhamiaji kuweka tahadhari maalum ili kuzuia uwezekano wa msanii huyo kuondoka nchini bila idhini.

Katika kipindi cha zaidi ya wiki tatu alichokuwa rumande, juhudi za kukamilisha masharti ya dhamana zilihusisha kupata mdhamini kutoka Kenya na kuwasilisha nyaraka muhimu, ikiwemo barua zilizoidhinishwa na idara ya uhamiaji.

Kwa sasa, Matonya anakabiliwa na shtaka la ubakaji kinyume na kifungu cha 3(1)(a) kinachosomwa pamoja na kifungu cha 3(3) cha Sheria ya Makosa ya Ngono akidaiwa kutenda kosa hilo Aprili 7, 2026 katika nyumba ya ghorofa eneo la Nyali, Kaunti ya Mombasa.

Pia anakabiliwa na shtaka mbadala la kufanya kitendo cha aibu dhidi ya mtu mzima.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa polisi, siku ya tukio mlalamikaji alikutana na mshtakiwa pamoja na rafiki yake baada ya mawasiliano ya simu.

Inadaiwa walikutana katika duka la pombe eneo la Bamburi kabla ya kuelekea Nyali walikokaa pamoja wakinywa na kula.

Taarifa zinaeleza kuwa baadaye walilala, huku mshtakiwa na rafiki yake wakiwa chumbani na mlalamikaji akiwa sebuleni. Inadaiwa kuwa mshtakiwa alitoka chumbani usiku na kwenda sebuleni ambako anadaiwa kumbaka mlalamikaji kwa nguvu.

Tukio hilo liliripotiwa polisi na kusababisha kukamatwa kwake.

Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tena Aprili 30, 2026 kwa hatua za awali kabla ya kuanza kusikilizwa rasmi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *