Morogoro. Watoto watatu wanaoishi katia Mtaa wa Area Six, Kata ya Kichangani, Manispaa ya Morogoro wamefariki dunia kwa kutumbukia kwenye shimo lenye maji ya mvua, ambalo awali lilikuwa likitumika kuchimba kokoto kwa ajili ya ujenzi.                            

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Andrew Kantimbo, kupitia taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari, amesema miili ya watoto hao ilikutwa ikielea kwenye shimo hilo jana jioni. Baada ya kuopolewa, miili hiyo ilipelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya uchunguzi na kusubiri taratibu za kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.

Kamanda Kantimbo amewataja watoto hao waliofariki dunia kwa kuzama kuwa ni Jackson Henry (miaka miwili), Mukimil Loghati (miaka minne) na Mursin Ramadhani (miaka minne), wote wakiwa wakazi wa Mtaa wa Area Six.

Akisimulia tukio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa huo wa Area Six, Habibu Degedela, amesema alipata taarifa za tukio hilo saa jana saa 12:30 jioni akiwa kwenye majukumu yake ya kuwatumikia wananchi. Alipigiwa simu na msamaria mwema aliyemtaarifu kuwa miili ya watoto hao ilikuwa ikielea kwenye shimo hilo.

“Baada ya kupata taarifa hizo, haraka nilikimbilia eneo la tukio na kukuta watoto wawili tayari wamefariki, na mmoja akiwa mahututi. Tulifanya jitihada za kuopoa miili ile miwili, na yule aliyekuwa mahututi tulimuwahisha kwenye kituo cha afya kilichopo jirani na eneo la tukio, lakini akiwa huko naye alifariki dunia,” amesema Degedela.

Amesema shimo hilo lililosababisha vifo vya watoto hao limechimbwa na mwananchi mmoja (jina limehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi) kwa lengo la kupata kokoto za ujenzi anaoufanya kwenye kiwanja chake. Hata hivyo, serikali ya mtaa huo ilishamuonya na kumchukulia hatua kutokana na shimo hilo kuhatarisha usalama wa watoto na wananchi wengine.

“Tulishamfuata na kumuonya. Baadaye tulimfikisha kwenye vyombo vya kisheria na akaamriwa kulifukia shimo hilo, na kweli alilifukia. Lakini baada ya siku chache alirudia kulifukua na kuendelea kuchimba kokoto kwa njia ya siri, hadi leo limesababisha vifo vya watoto hawa wadogo. Kama mzazi na kiongozi wa mtaa huu nimeumia sana,” amesema Degedela.

Kuhusu hatua zitakazochukuliwa dhidi ya mwananchi huyo anayetuhumiwa kuchimba shimo hilo, Degedela amesema kuwa kwa sasa suala hilo lipo mikononi mwa vyombo vya usalama, likiwemo Jeshi la Polisi, ambalo linaendelea na uchunguzi.

Aidha, amesema kuwa kupitia mikutano ya mtaa na vikao vya Baraza la Maendeleo la Kata (BMK), wamepanga kuweka ajenda ya usalama na kutoa elimu kwa wananchi kuchukua tahadhari, hasa katika kipindi hiki cha mvua.                                                         

Amesisitiza kuwa mkazi yeyote anayechimba shimo kwa ajili ya choo, karo, kufyatua tofali au matumizi mengine, ahakikishe analifunika au kulifukia mara baada ya kukamilisha shughuli husika.

Amesema kipindi hiki cha mvua kinaambatana na hatari mbalimbali, ikiwemo nyumba na majengo ambayo hayajakamilika (mapagala), ambayo kutokana na mvua nyingi huweza kupata nyufa na kusababisha madhara. Hivyo, wananchi wanapaswa kuwa karibu na watoto wao wadogo ambao wako kwenye hatari zaidi.

“Pia ipo miti mikubwa ambayo kutokana na mvua hizi mizizi yake imeoza, na inaweza kuanguka na kusababisha madhara kwa watoto wanapocheza chini yake. Mzazi ahakikishe muda wote anafahamu mtoto wake yuko wapi. Usiruhusu ipite hata nusu saa bila kujua mahali alipo mtoto wako,” amesisitiza Degedela.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *