
Taarifa hiyo ya tathimini imetolewa kupitia uchambuzi wa mfumo wa kubaini uhakika wa chakula (IPC), uliochapishwa leo Jumatano na Wizara ya Kilimo ya Lebanon kwa ushirikiano na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO pamoja na la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP.
Familia zilizokuwa zarejea kwenye hali ya janga
Mwakilishi wa WFP nchini Lebanon, Alison Oman-Lawy amesema tahadhari iliyotolewa katika tathmini iliyopita sasa imethibitika.
“Kwa bahati mbaya, hali ya hatari tuliyoionya hapo awali sasa imedhihirika. Mafanikio yaliyopatikana kwa juhudi kubwa yamefutika haraka,” amesema.
Ameongeza kuwa familia nyingi zilizokuwa zikijitahidi kuendelea kuishi sasa ziko katika hatari kubwa zaidi kutokana na migogoro, kufrushwa kwa watu na kupanda kwa gharama za maisha.
“Familia ambazo zilikuwa zinajikongoja kuishi sasa ziko kwenye hatari ya kurejea katika hali ya janga, huku migogoro, watu kukimbia makazi yao na kupanda kwa bei ya bidhaa vikifanya chakula kuwa ghali zaidi,” amesema Oman-Lawy.
Sekta ya kilimo yaendelea kudhoofika
Kwa upande wake, mwakilishi wa FAO nchini Lebanon, Noura Araba Haddad amesema matokeo ya uchambuzi huo yanaonesha kuwa mishtuko ya mara kwa mara inaendelea kudhoofisha maisha ya wakulima na kuathiri uhakika wa chakula nchini humo.
“Matokeo haya yanaonesha haja ya dharura ya kutoa msaada wa kilimo kwa wakulima ili kuzuia hali kuendelea kuwa mbaya zaidi,” amesema Haddad.
Sekta ya kilimo, ambayo ni chanzo muhimu cha chakula na kipato kwa wananchi wengi, imeathiriwa vibaya na bado haijapona tangu kuzuka kwa migogoro mwaka 2014.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa uharibifu wa mashamba, kuhama kwa familia za wakulima, ugumu wa kufikia maeneo ya kilimo, kupanda kwa gharama za pembejeo na hali ya kutokuwa na usalama vinaendelea kudhoofisha uzalishaji wa chakula, huku hatari hizo zikiongezeka wakati msimu wa upandaji wa mazao ya masika ukielekea mwisho.
Waziri wa Kilimo: Uhakika wa chakula ni jukumu la wote
Waziri wa Kilimo wa Lebanon, Nizar Hani amesema kulinda uhakika wa chakula nchini humo ni jukumu la pamoja la kitaifa na kimataifa.
“Kuwekeza katika sekta ya kilimo ni muhimu ili kuhakikisha utulivu na kuimarisha mnepo wa jamii za wenyeji dhidi ya majanga yanayojirudia,” amesema.
Wakati huo huo, mfumuko mkubwa wa bei na gharama za chakula vinaendelea kupunguza uwezo wa wananchi kununua mahitaji muhimu, huku kupungua kwa misaada ya kibinadamu na uhaba wa fedha vikifanya hali kuwa ngumu zaidi kwa familia nyingi.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yameonya kuwa bila msaada wa uhakika wa kibinadamu, upatikanaji bora kwa maeneo yaliyoathirika na mazingira tulivu ya kiusalama na kiuchumi, hali ya ukosefu wa chakula nchini Lebanon huenda ikaendelea kuwa mbaya zaidi katika miezi ijayo.