
Utafiti huo uliongozwa na Chuo Kikuu cha Addis Ababa kwa ushirikiano na Wizara ya Afya ya Ethiopia pamoja na Shirika la Umo0ja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP, unachunguza jinsi matibabu ya lishe yanavyoweza kutolewa kupitia mfumo wa kawaida wa huduma za afya ya msingi badala ya kutegemea zaidi mifumo ya misaada ya dharura ya kibinadamu.
Mafanikio katika wilaya tano
Utafiti huo uliofanyika kati ya mwaka 2023 na 2025 katika wilaya tano za Oromia, Sidama, Afar, Somali na maeneo ya Kusini, umeonesha kuwa huduma za MAM zilipatikana katika karibu vituo vyote vya afya vya maeneo yaliyoshirikishwa.
Watafiti pia wamebaini kuimarika kwa uratibu kati ya mamlaka za mitaa, kufuatwa vizuri kwa miongozo ya matibabu, usimamizi bora wa ugavi wa bidhaa za lishe, pamoja na kuongezeka kwa uelewa wa jamii kuhusu huduma za utapiamlo.
Maafisa wamesema hatua hiyo ilichangia kupungua kwa kiwango cha utapiamlo katika wilaya zilizofanyiwa utafiti.
“Kuunganisha usimamizi wa MAM katika mpango wa kawaida wa wahudumu wa ugani wa afya kunasaidia kuhakikisha utambuzi wa mapema, mwendelezo wa huduma, na upatikanaji wa haki wa huduma za lishe na afya zinazookoa maisha zaidi ya huduma za dharura,” amesema Bi. Hiwot Darsene, Afisa Mkuu wa Ofisi ya Uratibu wa Lishe katika Wizara ya Afya.
Ameongeza kuwa “Matokeo yanaonesha kuwa pale ambapo kuna miongozo ya kitaifa, usimamizi na vifaa vya kutosha, vituo vya afya vinaweza kutoa huduma zenye ubora wa juu.”
Wito wa ufadhili endelevu na kuimarisha mifumo
Watafiti na maafisa wa afya wameeleza kuwa mafanikio ya muda mrefu yatategemea uwepo wa ufadhili endelevu, mifumo imara ya ugavi pamoja na mafunzo endelevu kwa wahudumu wa afya walioko mstari wa mbele. Dkt. Rahel Argaw, Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Afya katika Chuo Kikuu cha Addis Ababa, amesema utafiti huo unatoa ushahidi wa vitendo unaoweza kusaidia kuimarisha sera za kitaifa za lishe na kuboresha utoaji wa huduma.
“Ushirikiano huu unaonesha namna tafiti makini zinazolenga sera zinavyoweza kuboresha utoaji wa huduma na kuokoa maisha,” amesema Dkt. Argaw. “Chuo Kikuu cha Addis Ababa kinajivunia kuchangia ushahidi unaosaidia Ethiopia kuimarisha viwango vya kitaifa, kuwasaidia wahudumu wa afya walioko mstari wa mbele, na kuharakisha mapambano dhidi ya utapiamlo wa watoto na akina mama.”
Ethiopia yapiga hatua katika kupunguza utapiamlo
Kwa mujibu wa matokeo ya hivi karibuni ya Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya (DHS), Ethiopia imefanikiwa kupunguza kiwango cha udumavu wa lishe kali kutoka asilimia 10 mwaka 2016 hadi asilimia tano mwaka 2026, jambo linaloonesha mafanikio ya sera zake za lishe na afya.
Hapo awali, matibabu ya Utapiamlo wa Kati wa Papo kwa Papo yalikuwa yakitolewa zaidi kupitia mifumo ya misaada ya kibinadamu, lakini wataalamu wanasema hali hiyo ilisababisha mapungufu katika mwendelezo wa huduma na uhusiano mdogo na huduma nyingine za afya.
“Utafiti huu unaonesha kuwa kuunganisha huduma za MAM katika mfumo wa afya ya msingi wa Ethiopia si tu kunawezekana bali pia kunaleta matokeo,” amesema Dkt. Mutinta Hambayi, Naibu Mkurugenzi wa WFP nchini Ethiopia.
“Kwa uwepo wa vifaa vya kutosha, wahudumu wa afya waliofunzwa, na uratibu mzuri, watoto na akina mama wanaweza kupata huduma kwa wakati karibu na makazi yao.”
Warsha ya kitaifa yajadili upanuzi wa huduma
Matokeo hayo yamewasilishwa katika warsha ya kitaifa ya usambazaji wa matokeo iliyofanyika Addis Ababa, ikiwakutanisha maafisa wa serikali, mamlaka za afya za kikanda, washirika wa maendeleo, mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na watafiti.
Washiriki wamejadili mikakati ya kupanua huduma za MAM zilizojumuishwa katika mfumo wa afya nchini kote pamoja na namna ya kudumisha mafanikio yaliyopatikana kupitia ufadhili wa uhakika na mifumo imara ya ugavi.
WFP, shirika kubwa zaidi duniani la misaada ya kibinadamu, limesema litaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya ya Ethiopia pamoja na washirika wa kimataifa kupanua huduma za lishe zinazotolewa ngazi ya jamii ili kupunguza utapiamlo wa watoto na akina mama kote nchini.