Ripoti iliyoandaliwa na Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu nchini Sudan imeonyesha kuwa watu 6,000 wanashikiliwa na wapiganaji wa kundi la waasi la Rapid Support Forces (RSF) katika magereza huko El Fasher, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kaskazini, magharibi mwa nchi, na pia imerekodi ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa na kundi hilo dhidi ya raia.

Mkuu wa kamati iliyoandaa ripoti hiyo, Kamal al-Din al-Dandrawi, alisema katika warsha iliyofanyika jana Jumapili, kwamba kamati yake imerekodi ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanywa na RSF, akieleza kuwa ripoti hiyo imejumuisha visa vya kukwepa adhabu, vitendo vya ukatili vilivyorekodiwa dhidi ya wanawake na watoto, pamoja na ukiukwaji wa haki za raia za elimu na afya.

Al-Dandrawi amesisitiza kwamba vita nchini Sudan vimesababisha “janga kubwa zaidi la binadamu duniani,” na kusema kuwa vimewalazimisha watu milioni 14 kukimbia makazi yao, na kusababisha uhaba mkubwa wa chakula kwa takriban watu milioni 25.

Kwa mujibu wa mashirika ya ndani na ya kimataifa, kutekwa El Fasher Oktoba 26, 2025, kuliambatana na mauaji dhidi ya raia, huku kukiwa na maonyo kuhusu kugawanyika nchi ya Sudan kijiografia.

Mwaka jana Oktoba 29, kamanda wa Rapid Support Forces (RSF) Mohamed Hamdan Dagalo alikiri kwamba vikosi vyake vimefanya “uhalifu” huko El Fasher, akidai kwamba ameunda kamati ya kuchunguza suala hilo.

Mashirika ya afya na ya kutetea haki za binadamu ya Sudan yanawatuhumu wapiganaji wa RSF kuwa wanawashikilia zaidi ya watu 19,000 katika jela za “Degris” na “Kobar” katika jimbo la Darfur Kusini, na vituo vingine vya kizuizini huko Darfur, magharibi mwa Sudan.

Waasi wa Rapid Support Forces (RSF) wanadhibiti majimbo matano ya Darfur huko magharibi mwa Sudan kati ya majimbo yote 18 ya nchi hiyo.

Eneo la Darfur linaunda takriban humusi (moja ya tano) ya ardhi ya Sudan yenye ukubwa wa zaidi ya kilomita mraba milioni 1.8.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *