
Dar es Salaam. Benki ya Ushirika (Coop Bank) imeeleza mkakati wa kukuza uchumi jumuishi katika mkakati wa 2026/30 huku ikiwezesha utoaji wa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh101 bilioni katika kipindi mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake.
Katika kipindi hicho, kitabu cha mikopo cha benki hiyo iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Aprili mwaka jana jijini Dodoma, kimeonyesha imeongezeka na kufika Sh101.02 bilioni kutoka Sh16 bilioni ikiwa ni ukuaji wa asilimia 506.
Aidha kwa mujibu wa takwimu za robo ya kwanza ya mwaka 2026, vilevile mali za benki zimeongezeka na kufika Sh178.7 bilioni kutoka Sh46.8 bilioni katika kipindi kama hicho mwaka 2025, sawa na ukuaji wa asilimia 281.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Aprili 29, 2026 Mkurugenzi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Godfrey Ng’urah amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa benki kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia makundi muhimu ya kiuchumi.
Amesema amana za wateja nazo zimeongezeka na kufika Sh101.5 bilioni kutoka Sh12.5 bilioni sawa na asilimia 709.
“Pesa za wanahisa pia zimeongezeka na kufika Sh42.1 bilioni katika robo ya kwanza ya mwaka huu kutoka Sh27.4 bilioni ya robo ya kwanza ya mwaka 2025 ikiwa ni ukuaji wa asilimia 54,” amesema.
Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja, benki imekuwa kwa kasi ikijikita kuongeza ujumuishi wa watumiaji wa huduma za kibenki.
“Ifikapo mwaka 2030, tumepanga kufikia lengo la kuongeza watumiaji wa huduma za kibenki milioni 10,” amesema.
Akinukuu utafiti wa FinScope unaoonyesha sehemu kubwa ya wananchi bado hawajajumuishwa kikamilifu katika huduma rasmi za kifedha, amesema Coop Bank imelenga kufikia watu milioni 10 katika mkakati wake wa miaka mitano.
“Hivi sasa Watanzania wanaotumia huduma za kibenki ni milioni nane, tunahitaji ku double (kuongeza idadi kama hiyo) na kuwafikia watu milioni 10 ifikapo 2030, tukilenga kuwafikia wajasiriamalli vijana, wajasiriamali wadogo na wa kati milioni mbili na makundi mengine,” amesema.
Akizungumzia mkakati wa kukuza uchumi kupitia kilimo, Ng’urah amesema kilimo kinaweza kutumia huduma za kibenki na kubainisha kwamba taasisi za fedha nyingi zitajilaumu kwa kuona ni kwa nini uchumi wa nchi hii haujaenda kwenye kilimo kwa muda mrefu.
“Katika kilimo si tu kwa ajili ya chakula, bali ni biashara, ni mali ghafi ya viwanda, ukitaka kuongelea ujumuishi wa kibenki kama hujaenda kwenye kilimo ni ndoto, kwani Watanzania waliopo mijini hawazidi asilimia 35, asilimia iliyobaki wapo kwenye miji midogo na vijiji na wengi wao shughuli zao ni kilimo.
“Ili kubadili uchumi wa nchi hii ni lazima uwape mitaji wakulima, sekta ya kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, uwekezaji katika kilimo ni msingi wa ukuaji wa uchumi jumuishi,” amesema Ng’urah.
Aidha, Ng’urah ameeleza pia namna benki hiyo ilivyowekeza katika mifumo ya kidijitali ikiwemo huduma za Coopesa, Coop Net na Coop Wakala, ambazo zinalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kote nchini.