
Dar es Salaam. Zaidi ya manusura 100 wa vitendo vya ukatili wa kijinsia wamepokewa na kuhudumiwa katika Kituo cha Mkono kwa Mkono (One Stop Center) kilichopo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala jijini Dar es Salaam ndani ya kipindi cha miezi mitatu sawa na siku 90.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi, Aprili 30, 2026 na Nicodemis Kimaro kutoka Dawati la Jinsia, Wanawake na Watoto kutoka katika kituo hicho wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) katika kituo hicho.
Kimaro amesema katika kipindi cha miezi mitatu kutoka Januari hadi Machi 2026, wamepokea manusura watoto 101 kati ya hao wakike wakiwa 84 na wakiume 17.
Aidha, amesema baadhi ya manusura hao ni watu wazima huku wanawake wakiwa 15 na wanaume mmoja.
Amebainisha matukio mengi yanayoripotiwa yanahusisha ukatili wa kingono, hususan ubakaji na ulawiti ambapo waathirika zaidi ni watoto walio chini ya umri wa miaka 18.
Amesema manusura hao wamekuwa wakifikishwa kituoni hapo na kupatiwa huduma jumuishi zinazohusisha wataalamu wa ustawi wa jamii, polisi, madaktari, wanasheria na washauri wa kisaikolojia, wote wakifanya kazi kwa pamoja kuhakikisha manusura wanapata msaada wa haraka.
“Huduma zetu ni bure kwa manusura wote. Tunahakikisha kila anayefika hapa anapata msaada stahiki bila kujali uwezo wake wa kifedha,” alisisitiza.
Kwa upande wake, daktari wa Binadamu kutoka hospitali ya Mwananyamala, Dk Yusuph Kashoro amesema manusura wanapofika kituoni hupokelewa kwanza na wataalamu wa ustawi wa jamii, kusikilizwa na kuelekezwa, kabla ya kufikishwa kwa daktari kwa uchunguzi wa kina wa kitabibu na ukusanyaji wa ushahidi.
“Tunafanya uchunguzi wa kitabibu na pia kukusanya ushahidi kama vile alama za majeraha, michubuko au sampuli za vinasaba (DNA) kwa kutumia vifaa maalum vya uchunguzi wa kisayansi,” amesema.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa manusura kuepuka kuoga au kubadilisha nguo mara baada ya tukio, kwani kufanya hivyo kunaweza kuharibu ushahidi muhimu utakaosaidia katika uchunguzi wa kesi.
“Ni muhimu manusura wafike hospitali mapema wakiwa katika hali ile ile baada ya tukio ili kuongeza uwezekano wa kupata ushahidi sahihi,” ameeleza.
Mbali na matibabu ya mwili, amesema manusura hupatiwa msaada wa kisaikolojia ili kukabiliana na athari za tukio, ikiwemo msongo wa mawazo.
Naye Mwanasheria kutoka kituo hicho, Ramadhani Kisengo amesema tangu mwaka jana, ni kesi takriban 15 tu ndizo zilizokamilika na kupata hukumu huku wengi wa watuhumiwa wa ubakaji wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.
Hata hivyo, mwanasheria huyo alieleza kusikitishwa na tabia ya baadhi ya wazazi au walezi kumaliza kesi nje ya mahakama na kudai kumaliza kifamilia.
Ameeleza kuwa tabia hiyo inapora haki ya waathirika wa vitendo vya ukatili.