MSHAMBULIAJI wa Tanzania, Mbwana Samatta, ameendelea kuandika historia yake barani Ulaya baada ya kutangazwa kuwa mchezaji bora wa mwezi wa Aprili 2026 katika klabu yake ya Le Havre Athletic Club (HAC), kufuatia kiwango bora alichoonyesha ndani ya kipindi hicho.

Samatta alitwaa tuzo hiyo akionyesha ubora katika mechi nne za Ligue 1 alizocheza Aprili ambapo alifunga mabao mawili na kuwa mhimili wa safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

Licha ya HAC kupata sare katika michezo yote minne, mchango wa mshambuliaji huyo umekuwa msaada katika harakati za chama hilo kuwa mbali na hatari ya kushuka daraja kwa sasa wapo nafasi ya 14 wakiwa na pointi 31 katika msimamo wenye timu 18.

SAMA 02

Katika mchezo wa Aprili 26 dhidi ya Metz uliomalizika kwa sare ya mabao 4-4, Samatta alicheza dakika zote 90 na kufunga bao moja huku akipata alama 7.6 kati ya 10 ya ubora katika mchezo huo.

Aliendeleza ubora wake Aprili 12 dhidi ya Nice ambapo pia alifunga bao katika sare ya 1-1, akicheza dakika 87 na kupata alama 7.0.

Katika michezo mingine, ikiwemo dhidi ya Angers (Aprili 18) ambapo alicheza dakika 68 na dhidi ya Auxerre (Aprili 5) alicheza kwa dakika 20, Samatta hakufunga lakini aliendelea kuwa na mchango katika ligi hiyo ambayo inaongozwa na Paris Saint-Germain yenye pointi 69.

Kwa ujumla, ndani ya Aprili, Samatta alicheza dakika 265 na kufunga mabao mawili, akithibitisha kuwa licha ya kuwa na miaka 33 anaweza kuwa msaada kwenye kikosi hicho.

SAMA 01

Mbali na kiwango chake cha sasa, rekodi za Samatta barani Ulaya zinaongeza uzito wa mafanikio haya. Akiwa amecheza katika ligi mbalimbali kubwa, mshambuliaji huyo ana jumla ya mechi zaidi ya 400 za klabu na kufunga zaidi ya mabao 150 katika maisha yake ya soka la kulipwa.

Aling’ara zaidi akiwa na KRC Genk ya Ubelgiji ambapo alifunga mabao 56 katika mechi 144 za ligi na kuwa mfungaji mshindani wa kiatu cha ufungaji bora ligi msimu wa 2018/19 akiwa na mabao 20 katika Jupiler Pro huku akiisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa.

Samatta pia aliweka historia alipocheza na kufunga katika Ligi Kuu ya England akiwa na Aston Villa na kuwa Mtanzania wa kwanza kufanya hivyo. Amecheza pia katika klabu kubwa kama Fenerbahçe ya Uturuki, Royal Antwerp na PAOK ya Ugiriki ambako alitwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *