Timu ya Polisi Tanzania imetanguliza mguu mmoja kurejea Ligi Kuu Bara baada ya kuichapa Tanzania Prisons kwa mabao 4-0, na kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu.

Mchezo huo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya mtoano (Play-Off) ulipigwa kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro. Tangu mapema, Polisi ilionyesha nia ya kutaka kumaliza mchezo huo kwa kuishambulia vikali ngome ya Prisons.

Katika dakika ya 15, Polisi ilifanikiwa kupata bao la kwanza kwa mkwaju wa penalti uliowekwa wavuni na Juhudi Philemon, na kufungua milango ya ushindi kwa Maafande hao. Penalti hiyo ilitokana na beki wa Prisons kuunawa mpira wakati akijaribu kuzuia shuti la mshambuliaji Tariq Seif, hatua iliyomfanya mwamuzi Seleman Nonga kutoka Arusha kuamuru adhabu hiyo.

POLI 01

Prisons ilipoteza nafasi nzuri ya kusawazisha katika dakika ya 27, baada ya mpira wa kichwa kutoka kwa winga Harun Chanongo kugonga mwamba wa chini na kutoka nje, kufuatia kona iliyochopwa na Salum Kimenya.

Hadi mapumziko, Polisi ilitoka mbele ikiwa na uongozi wa bao 1-0 huku ikitawala mchezo, wakati Prisons ikionekana kucheza kwa presha kubwa ikisaka bao la kusawazisha.

Kipindi cha pili, Polisi ilirejea kwa nguvu mpya na kufanikiwa kupata bao la pili katika dakika ya 46. Bao hilo lilifungwa kwa kichwa na Tariq Seif, akimalizia krosi ndefu kutoka kwa nahodha na beki wa kulia wa kikosi hicho, Denis Mushi.

Polisi iliendelea kuwasakama wapinzani wao na kupata bao la tatu lililowekwa wavuni kwa urahisi na beki Tatizo Shem, akimalizia mpira uliotemwa na kipa Mussa Mbisa kufuatia shuti kali la Denis Mushi.

POLI 02

Emmanuel Mpuka alihitimisha karamu hiyo ya mabao kwa kufunga goli la nne kwa mkwaju wa penalti wa kiufundi katika dakika ya 73. Penalti hiyo ilipatikana baada ya Naku Kazimoto kuangushwa ndani ya eneo la hatari.

Timu hizi zitakutana tena katika mchezo wa marudiano utakaopigwa Julai 16 kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, ili kuamua timu rasmi itakayocheza Ligi Kuu msimu ujao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *