Tuzo hiyo hutolewa kila mwaka kwa kutambua mchango wa mtu, watu au taasisi katika kulinda uhuru wa vyombo vya habari, na UNESCO ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni limetoa tangazo hilo leo kabla ya siku yenyewe ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, tarehe 3 mwezi Mei.

Matukio yaliyoripotiwa

UNESCO kupitia taarifa yake inasema inaenzi mchango wa chama hicho katika kurekodi mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari na kutetea haki zao licha ya kuongezeka kwa ghasia.

Tangu mapigano yalipoanza mwaka 2023, chama hicho kimeripoti vifo vya waandishi wa habari 32 na matukio zaidi ya 500 ya ukiukwaji wa haki dhidi ya wanahabari, huku miundombinu mingi ya vyombo vya habari nchini Sudan ikiharibiwa.

Kauli za UNESCO na Mkuu wa Chama cha wanahabari Sudan

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Khaled El-Enany, kupitia taarifa hiyo amepongeza uimara wa chama hicho akisema wanachama wake wameonesha “ujasiri wa hali ya juu” kwa kuendelea kutoa taarifa muhimu katika mazingira hatarishi.

Mwenyekiti wa chama hicho, Abdelmoniem Abuedries Ali, amesema tuzo hiyo ni heshima kwa waandishi wote wa habari nchini Sudan, “wanaoendelea kuripoti ukweli licha ya vitisho na vurugu.”

Mzozo huo umegeuza baadhi ya maeneo kuwa kama “ukanda wa ukimya,” ambapo kukatika kwa mtandao, kuharibiwa kwa vyombo vya habari na vikwazo vya kuripoti kumesababisha kuenea kwa taarifa potofu, za  uongo na propaganda. UNESCO inasema takribani asilimia 90 ya miundombinu ya vyombo vya habari nchini Sudan imeharibiwa, jambo linalowaacha wananchi wengi bila taarifa za kuaminika.

Hali halisi ya vyombo vya habari duniani

Tuzo hii inakuja wakati ambapo uhuru wa vyombo vya habari duniani unakabiliwa na changamoto kubwa.

Takwimu za UNESCO zinaonesha uhuru wa kujieleza umepungua kwa asilimia 10 tangu mwaka 2012, sambamba na ongezeko kubwa la mashambulizi ya wanahabari mtandaoni na vile vile wao wenyewe waandishi wa habari kujidhibiti mitandaoni Unyanyasaji wa mtandaoni pia umeongezeka, hasa kwa waandishi wa habari wanawake.

Tuzo hii itakabidhiwa rasmi wakati wa mkutano wa Uhuru wa Vyombo vya Habari ulioandaliwa na UNESCO utakaoanza Mei 4 hadi 6 jijini Lusaka nchini Zambia.

Mkutano huo utajadili namna ya kuimarisha uandishi huru wa habari na kupambana na habari potofu n aza uongo, mambo ambayo UNESCO inaona ni muhimu ili kuendeleza amani, uwajibikaji na utawala wa kidemokrasia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *