
Kupitia ujumbe wake wa siku hiyo António Guterres amesema waandishi wa habari wanaendelea kuwa miongoni mwa waathirika wa kwanza katika vita na migogoro, huku akionya kuwa uhuru wa vyombo vya habari duniani uko katika hatari kubwa kutokana na shinikizo za kisiasa, kiuchumi na kiteknolojia.
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa Guterres ameongeza kuwa waandishi wengi wanakabiliwa na vitisho, ufuatiliaji, unyanyasaji wa kisheria na hata kuuawa kwa sababu ya kazi yao ya kuripoti ukweli akisistiza kuwa
“Na mara nyingi zaidi, waathirika wa kwanza huwa ni waandishi wa habari ambao hujitolea kila kitu ili kuripoti ukweli si katika vita pekee, bali popote pale ambapo wenye mamlaka wanaogopa kuchunguzwa.”
Onyo kuhusu mauaji ya waandishi wa habari
Katibu Mkuu huyo amesema miaka ya hivi karibuni dunia imeshuhudia ongezeko kubwa la mauaji ya waandishi wa habari, hasa katika maeneo ya vita, huku wengi wakilengwa kwa makusudi.
Ameeleza kuwa hali hiyo imechangiwa na kile alichokiita “kutoadhibiwa kwa wahalifu,” akibainisha kuwa asilimia kubwa ya uhalifu dhidi ya wanahabari hauchunguzwi wala kupewa adhabu.
“Asilimia themanini na tano ya uhalifu unaofanywa dhidi ya waandishi wa habari haupelelezwi na wala hauadhibiwi, kiwango hiki cha kutokuchukuliwa hatua hakikubaliki.”
Guterres pia ameonya kuwa shinikizo za kiuchumi, matumizi ya teknolojia mpya kama Akili Mnemba au AI na kuenea kwa taarifa potofu vinaendelea kudhoofisha uhuru wa vyombo vya habari na kuharibu imani ya wananchi kwa taarifa za kuaminika.
Amesema hali hiyo inahatarisha mshikamano wa kijamii na kufanya migogoro kuwa migumu zaidi kuzuiwa au kutatuliwa.
“Uhuru wote unategemea uhuru wa vyombo vya habari. Bila uhuru huo, hakuwezi kuwa na haki za binadamu, maendeleo endelevu wala amani.”
Katika hitimisho la ujumbe wake, Katibu Mkuu huyo ametoa wito kwa dunia kuwalinda waandishi wa habari na kuhakikisha ukweli pamoja na wale wanaousema wanakuwa salama.