HALI imekuwa mbaya kwa kocha mkuu wa maafande wa Tanzania Prisons, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’ baada ya kufikisha mechi sita mfululizo za Ligi Kuu bila kuonja ladha ya ushindi tangu alipotambulishwa kikosini humo Februari 27, 2026.

Nsajigwa aliyejiunga na timu hiyo, Februari 27, 2026 akichukua nafasi ya Mkenya Zedekiah ‘Zico’ Otieno, aliyeondoka kwa makubaliano ya pande mbili, Februari 25, 2026 ameiongoza Prisons katika mechi sita, bila ya kuonja ladha ya ushindi.

NSA 04

Hatua ya kucheza mechi hizo sita mfululizo bila ya kuonja ladha ya ushindi imejiri baada ya kikosi hicho cha maafande kuchapwa mabao 3-0, dhidi ya TRA United, katika pambano la Ligi Kuu lililopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Katika mechi hiyo ya leo, mabao ya TRA United, yalifungwa kupitia kwa Ramadhan Salum ‘Chobwedo’, aliyefunga dakika ya tatu, Joseph Akandwanaho dakika ya 62 na Khassimuh Mugoya dakika ya 73 na kuzidisha presha kwa Shadrack Nsajigwa.

NSA 02

Katika mechi hizo sita za Ligi Kuu ambazo Nsajigwa ameiongoza timu hiyo, amepoteza nne na kutoka sare mbili, ingawa kwa ujumla kikosi hicho kimecheza 20 kikishinda tatu, kikitoka sare tano na kupoteza 12 kikiwa nafasi ya 15 na pointi 14.

Kwa upande wa TRA United ushindi huo unaifanya kusogea hadi nafasi ya tano kwenye msimamo kutoka ile ya saba, ikiwa na pointi 30 baada ya kucheza mechi 20 ambapo kati ya hizo kikosi hicho kimeshinda nane, sare sita na kupoteza pia sita.

NSA 03

Kwa miaka ya mwanzoni mwa taaluma yake, Nsajigwa aliwahi kuichezea Tanzania Prisons ya Mbeya, kisha kujiunga na Yanga aliyoitumikia kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2012, huku pia akiwa ni nahodha wa kikosi cha timu ya taifa ya Taifa Stars.

NSA 01

Mechi nyingine ya leo iliyokuwa ya kuvutia pia, ilipigwa kwenye Uwanja wa Airtel, Singida, ambapo wenyeji, Dodoma Jiji walishindwa kutamba nyumbani, baada ya kulazimishwa suluhu dhidi ya kikosi cha Namungo FC, ‘Wauaji wa Kusini’. Kwa matokeo hayo yanaifanya Dodoma Jiji kubakia nafasi ya nane na pointi 25, baada ya kushinda mechi sita, sare saba na kupoteza pia saba, huku Namungo FC ikishika nafasi ya tisa na pointi 23, ikishinda tano, sare nane na kupoteza pia saba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *