
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Dk Evaline Munisi kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) akichukua nafasi ya Rahma Riyadh Kisuo ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Dk Munisi ni Katibu Mkuu wa chama cha NCCR-Mageuzi ambaye hivi karibuni Rais Samia alimteua kuwa mbunge kupitia nafasi zake 10.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Jumamosi Mei 2, 2026 na Katibu Mkuu Kiongozi Dk Moses Kusiluka imeeleza mabadiliko hayo yamefanywa na Rais Samia ikiwamo uhamisho wa makatibu wakuu wa Wizara.
Makatibu wakuu waliohamishwa wizara ni Eliakim Maswi amehamishwa kutoka Wizara ya Katiba na Sheria kwenda Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu.
Pia, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk John Jingu amehamishiwa Wizara ya Katiba na Sheria.
Hivi karibuni Rais Samia alimteua Dk Munisi kuwa mbunge kupitia nafasi zake 10.
Dk Munisi alikuwa mgombea mwenza wa urais kupitia tiketi ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 huku mgombea urais akiwa Haji Ambar Khamis.
Aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi mwaka 2025 na baadaye kuwa mgombea mwenza.
Dk Munisi anachukua nafasi ya Rahma Riyadh Kisuo ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) baada ya uteuzi wake kutenguliwa.
Kisuo aliteuliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia NGO’s na baadaye kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Mahusiano mnamo Novemba 2025.
Dk Munisi anafuata nyayo za Queen Sendiga ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 alikuwa mgombea urais kupitia chama cha Alliance for Democratic Change (ADC).
Pia, Sendiga ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, ndani ya ADC alikuwa Naibu Katibu Mkuu. Hata hivyo, uteuzi wake kuwa Mkuu wa Mkoa umemfanya kuwa mwanachama wa CCM.