Musoma. Jeshi la Polisi mkoani Mara limeagizwa kuchukua hatua mapema kuzuia uhalifu kabla haujatokea katika jamii badala ya kusubiri uhalifu utokee ndipo lichukue hatua.

Agizo hilo limetolewa mjini Musoma leo Jumamosi Mei 2, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi kwenye maadhimisho ya Siku ya Polisi mkoa wa Mara.

Kanali Mtambi amesema kumekuwepo na tabia ya polisi kuchukua hatua baada ya uhalifu kutokea, jambo ambalo amesema limekuwa likisababisha jamii kupata bughudha na usumbufu bila sababu za msingi.

“Kuchukua hatua baada ya matukio si vibaya na ni jukumu lenu polisi, lakini tunakuwa tumeiacha jamii ipate bughudha na kadhia ambazo hawakutakiwa kukumbana nazo kama tungeweza kuzuia vitendo hivyo kutokea,” amesema.

Baadhi ya askari polisi mkoani Mara wakiwa kwenye gwaride wakati wa maadhimisho ya Siku ya Polisi mkoani humo.

Amesema kuzuia matukio ya uhalifu kutokea katika jamii kutaiwezesha jamii kuishi kwa amani na utulivu, hivyo Serikali kuweza kutekeleza majukumu yake hasa ya kuwaletea maendeleo wananchi kama ilivyokusudiwa.

Kanali Mtambi amesema takwimu zinaonyesha kuwa kiwango cha uhalifu katika mkoa huo kimeshuka kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita na kwamba hali hiyo imetokana na jitihada zinazofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama mkoani humo, likiwemo Jeshi hilo la Polisi. Ameongeza kuwa ili hali hiyo iweze kuwa endelevu ni lazima polisi wajikite katika kuzuia uhalifu kutokea.

“Tumeambiwa kuwa mkoa wetu haupo katika mikoa 10 nchini yenye idadi kubwa ya vitendo vya uhalifu, sasa ili tuendelee kuwa katika nafasi nzuri ni lazima tuhakikishe tunazuia uhalifu kabla haujatokea,” amesema.

Kanali Mtambi pia amewataka wakazi wa mkoa huo kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili mkoa uendelee kuwa salama muda wote, kwa maelezo kuwa jukumu la ulinzi wa mkoa na nchi kwa ujumla ni la wananchi wote.

Amewataka wananchi hao kutoa taarifa kwa ajili ya kufichua vitendo vya uhalifu na wahalifu wenyewe, huku akiongeza kuwa Serikali mkoani humo haitasita kuwachukulia hatua wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo, na kuwataka wananchi wote kutii sheria bila shuruti.

“Serikali tayari imesema inataka kuleta tabasamu kwa wananchi, sasa sisi hatuko tayari kuona kuna mtu anazuia lengo hilo lisifanikiwe kwa kufanya uhalifu ambao kwa namna moja ama nyingine utasababisha wananchi washindwe kujiletea maendeleo au Serikali kuwaletea wananchi wake maendeleo,” amesema.

Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo alisema lengo la maadhimisho ya Siku ya Polisi pamoja na mambo mengine ni kutaka kuwatambua askari polisi waliofanya vizuri pamoja na kutafakari kwa pamoja mafanikio na changamoto zinazowakabili ili kuweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Amesema vitendo vya uhalifu, vikiwemo mauaji, vimepungua kwa kiwango kikubwa ndani ya mkoa huo, hali iliyosababisha mkoa huo kutokuwa miongoni mwa mikoa 10 yenye uhalifu mkubwa nchini.

“Kwa miaka miwili mfululizo hatupo kwenye mikoa 10 inayoongoza kwa mauaji nchini pamoja na vitendo vingine, lakini pia mkoa wetu umeongoza kwa kufanya operesheni nyingi za kusaka wahalifu, operesheni ambazo pia zimekuwa na matokeo chanya katika kuimarisha hali ya ulinzi na usalama katika jamii,” amesema Kamanda Lutumo, ingawa hakuweza kutaja takwimu.

Baadhi ya wadau wa Jeshi la Polisi mkoani humo wamesema kupungua kwa vitendo vya uhalifu mkoani humo ni ishara ya uwepo wa ushirikiano mzuri kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.

“Sote ni mashahidi, kwa kipindi cha nyuma mkoa wetu ulikuwa kinara wa vitendo hivyo ikiwemo mauaji, lakini leo ni jambo la faraja kusikia kuwa hatupo kwenye 10 bora. Hii hali inatakiwa kuwa endelevu,” amesema mbunge mstaafu wa Musoma Mjini, Vedastus Mathayo.

Mathayo amesema uwepo wa amani na utulivu ndani ya mkoa huo ni kichocheo cha maendeleo kwani wananchi watakuwa huru kushiriki katika shughuli za kimaendeleo na kuboresha uchumi wao.

Askofu wa Kanisa la Bonde la Baraka, Daniel Ouma amesema kuimarika kwa amani na usalama katika mkoa wa Mara ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya vyombo vya dola na wadau wengine wa amani, wakiwemo viongozi wa dini.

“Niipongeze Serikali ya mkoa kwa namna ambavyo imekuwa ikishirikiana na sisi viongozi wa dini, na ushirikiano huu umekuwa na matokeo chanya katika nyanja mbalimbali, ikiwemo kwenye suala zima la amani na utulivu katika mkoa wetu,” amesema Askofu Ouma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *