
Arusha. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu Dodoma, imetupilia mbali maombi ya aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Upangaji Mikopo katika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Chikira Jahari, aliyekuwa akipinga kufukuzwa kwake kazi.
Uamuzi huo umetolewa Aprili 30, 2026 na Jaji Dk Mustapher Siyani, baada ya kubaini kuwa mwombaji hakuthibitisha kuwepo kwa ukiukwaji wa sheria au haki ya kusikilizwa katika mchakato wa kinidhamu uliosababisha kufukuzwa kwake.
Chikira aliwasilisha maombi ya mapitio ya mahakama Januari 5, 2026, akiomba kufutwa kwa uamuzi wa Katibu Mkuu Kiongozi wa Septemba 16, 2019 uliothibitisha kusitishwa kwa ajira yake na kuamuru arejeshwe kazini.
Katika hoja zake, alidai kunyimwa haki ya msingi ya kusikilizwa kwa kuwa hakupatiwa ripoti ya uchunguzi iliyotumika dhidi yake, jambo lililomnyima nafasi ya kuandaa utetezi wa kina.
Pia, alidai kuwa kulitumika ushahidi mpya katika hatua za rufaa bila kupewa nafasi ya kuujibu.
Hata hivyo, upande wa Serikali ulipinga madai hayo, ukieleza kuwa hakuna sheria inayomlazimisha mwajiri kumpa mfanyakazi ripoti ya uchunguzi, na kwamba taratibu zote zilifuatwa ipasavyo.
Serikali ilisisitiza kuwa mwombaji hakuthibitisha kuwa aliomba nyaraka hizo na kunyimwa, wala kuonesha jinsi alivyoshindwa kujitetea.
Uamuzi wa Mahakama
Katika uamuzi wake, Jaji Siyani alieleza kuwa Mahakama katika mashauri ya mapitio ya kimahakama haina jukumu la kuchunguza uhalali wa maamuzi yenyewe kama ilivyo katika rufaa, bali huchunguza kama taratibu za kisheria zilifuatwa ipasavyo.
Alisisitiza kuwa ili mwombaji afanikiwe kupata amri za kufuta uamuzi wa mjibu maombi wa pili na wa tatu na kuamuru kurejeshwa kazini kwa mwombaji huyo, alipaswa kuonesha wazi kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria, matumizi mabaya ya mamlaka, au uvunjaji wa kanuni za haki asilia kama vile haki ya kusikilizwa.
Akichambua hoja ya kutopatiwa ripoti ya uchunguzi, Jaji Siyani alibaini kuwa hakuna ushahidi uliotolewa mahakamani kuonesha kuwa mwombaji aliomba ripoti hiyo na kunyimwa, wala hakuna sheria inayoweka wajibu kwa mwajiri kutoa ripoti hiyo kwa mfanyakazi katika mchakato wa kinidhamu.
Mahakama pia ilibaini kuwa mwombaji aliwasilisha utetezi wake kikamilifu wakati wa mchakato wa kinidhamu, hali inayodhihirisha kuwa hakuzuiwa kujieleza au kujitetea ipasavyo kama alivyodai.
Kuhusu madai ya ushahidi mpya, Mahakama ilieleza kuwa nyaraka zilizowasilishwa zinaonesha wazi kuwa mwombaji mwenyewe alitaja baadhi ya mambo aliyoyaita “mapya” katika rufaa zake, hivyo haikuwa sahihi kudai kuwa hakuyafahamu au hakupata nafasi ya kuyajibu.
Kutokana na uchambuzi huo, Mahakama ilifikia hitimisho kuwa mwombaji ameshindwa kuthibitisha kuwa haki zake zilikiukwa au kwamba kulikuwa na dosari za kisheria katika mchakato uliosababisha kufukuzwa kwake kazi.
Kwa msingi huo, Mahakama ilikataa kutoa amri ya kufuta maamuzi yaliyofanywa na waajiri wake, na pia ikakataa kutoa amri ya kumrejesha kazini na badala yake ilitupilia mbali maombi hayo.
“Kwa kuwa mwombaji ameshindwa kuthibitisha madai yake, maombi haya yanatupiliwa mbali,” ilieleza sehemu ya uamuzi wa Mahakama.
Mahakama pia iliamua kutotoa amri yoyote kuhusu gharama za kesi, ikimaanisha kuwa kila upande utabeba gharama zake wenyewe.
Rufaa/Msingi wa kesi
Septemba 25, 2025 Mahakama ya Rufani chini ya jopo la majaji watatu, ambao ni Barke Sehel, Khamis Ramadhan Shaaban na Dk Ubena Agatho, walikubali rufaa iliyokuwa imekatwa na Chikira aliyekuwa akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu kumnyima kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya mahakama kupinga kufukuzwa kazi.
Katika uamuzi wake, Mahakama ya Rufani ilifuta na kubatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu, na kurejesha jalada la shauri hilo Mahakama Kuu ili maombi hayo yasikilizwe mbele ya Jaji mwingine baada ya kukubaliana na sababu za rufaa za Chikira.
Chikira alikata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, uliotolewa Desemba 17, 2020, ambao ulitupilia mbali maombi ya kufungua shauri la mapitio.
Ilidaiwa kuwa kati ya Januari 2014 hadi 2016 alishindwa kuratibu mapitio ya vigezo vya utoaji wa mikopo ambapo zaidi ya Sh2.254 bilioni zilitolewa kwa wanafunzi 294 wa Chuo Kikuu cha Mt. Joseph ambao hawakukidhi vigezo na kuisababishia Serikali hasara.
Katika rufaa hiyo ya madai, Chikira alikata rufaa dhidi ya Bodi ya HESLB, Tume ya Utumishi wa Umma, Katibu Mkuu Kiongozi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Jaji Sehel amesema Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kupitia rekodi za rufaa hiyo na kueleza kuwa Jaji wa Mahakama Kuu aliingilia uhalali wa maombi ya msingi na akatoa majibu ya shauri ambalo lilikuwa halijawasilishwa na kusikilizwa na Mahakama.