Dar es Salaam. Mkongwe katika Bongo Fleva nchini Joseph Haule ‘Profesa Jay’ amerudi katika majukumu yake, hii ni baada ya kukinukisha katika jukwaa la Bongo Fleva Honours, ambapo alifanikiwa kutumbuiza kwa dakika 180.
Tukio hilo lilifanyika usiku wa kuamkia Mei 2,2026 katika ukumbi wa 710 Kawe Garden Jijini Dar es Salaam.
Licha ya afya yake kuendelea kuimarika taratibu msanii huyo alitumbuiza ngoma zote akiwa amekaa kwenye kiti huku akisimama mara chache, akiimba nyimbo mbalimbali ikiwemo ile aliyoshirikishana na Diamond ‘Kipi Sijasikia’ wimbo ambao kwasasa umetizamwa mara milioni 16 katika mtandao wa YouTube.
Mbali na kukiwasha kisawa sawa katika show hiyo wasanii wenzake walipanda jukwaani kusapoti anachokifanya akiwemo Naibu Waziri Sanaa, Michezo, na utamaduni Hamis Mwinjuma, Ay, Joe Makini pamoja na Jay Mo. Ambapo walifanikiwa kuimba wimbo wa ‘Hapo vipi’ ngoma iliyoachiwa mwaka 2015, Bongo Dar es Salaam nk.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamilisha show hiyo Professa amemshukuru Sugu kwa kumtunuku tuzo ya heshima huku akifunguka kuwa amepanga kufanya ziara katika mikoa mbalimbali nchini kwa ajili ya kuwafikia mashabiki wake.
“Kwanza nashukuru Mungu lakini pia Nawashukuru Watanzania wamenipokea kwa mapokezi makubwa. Tuzo ambayo nimepewa na Sugu inamaana kubwa sana kwangu maana yake watu wanajua mchango wangu kwenye muziki huu na kweli ni kwamba nimechonga barabara mziki huu ni ajira kubwa kwa vijana wengi wa Kitanzania kwahiyo kwa kitengo chao cha kutambua mchango wangu mdogo kwenye mziki huu ni kitu kikubwa sana kwangu.
“Nilipokea nafasi ya kutumbuiza kwenye jukwaa hili la Bongo Fleva Honours kwa mshtuko kwa sababu hili ni jukwaa kubwa lakini Mungu kanipa nguvu na uwezo nimeweza kufanya na watu wamependa. Kwa sasa niko vizuri nimeweza kuperfome masaa 3 na nitaendelea kufanya ziara nyingine kadri siku zinavyozidi kwenda, kwakweli maombi yamekuwa mengi watu wakinitaka niende mikoa mbalimbali. Nina mpango wa kuanza ziara kuwatembelea mashabiki zangu kila sehemu,”amesema Profesa
Aidha ameendelea akieleza kuwa “ndio tumepanga kufanya tour hapa ndio tumezindua na baada ya hapa tutaendelea kuwapa ratiba,”
Sugu alivyomkabidhi tuzo ya heshima
Mwanzilishi wa Bongo Fleva Honours, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amemkabidhi tuzo ya heshima msanii huyo kwa mchango wake kwenye muziki wa Bongo Fleva. Mchango ambao umeleta ajira kwa vijana.
“Tunakukabidhi tuzo hii kama utaenda kuiweka sebuleni au sehemu yoyote, utaenda kuweka hii kama kumbukumbu kwamba sisi kama Taifa tumetambua mchango wako kwenye muziki wa Bongo Fleva, mchango ambao umeleta nafasi ya ajira kwa vijana. Vijana wengi sana wangekuwa wanakaba lakini muziki umewabadilisha,” amesema Sugu
Alichokizungumza LadyJay Dee na Fid Q
“Hongera sana leo ni siku yako kubwa, siku yako ya kuheshimishwa na watu wote tunakupenda na tupo hapa kwa ajili ya kukusherehekea na kukupa moyo. Umepigana vita na umefanya safari ndefu sana umeiheshimisha tasnia ya burudani hapa Tanzania na umekuwa mfano bora kwa vijana wakike na wakiume.
Tunakushukuru sana kwa mchango wako mkubwa ambao umekuwa ukituinspire kila siku iendayo kwa Mwenyezi Mungu na siku ya leo (jana) ningependa kuwepo lakini kwa bahati mbaya nimeshindwa kufika kutokana na mambo yaliyo nje ya uwezo wangu. Najua hautoniangusha utafanya kama ambavyo umekuwa ukifanya mara zote,”amesema LadyJay Dee
Kwa upande wa Fid Q ameeleza kuwa ameamua kumsapoti Professa kwasababu ni mtu ambaye alimrudisha tena kwenye gemu.
“Nipo hapa kwa sababu najivunia yeye najivunia uwepo wake, najivunia namna amekuwa akituinspire, amekuwa akituongoza njia. Niseme tuu Profesa ni mchonga njia. Kihistoria mimi nilisha giveup kufanya haya mambo ya kimuziki lakini kuna ngoma aliitoa baada ya kusikiliza nikaamua kurudi katika muziki,”amesema Fid Q
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche alikuwepo katika show hiyo huku akifichua kuwa amemtambua Profesa tangu alipokuwa shule.
“Mimi nimekuwa mfuasi wa Professa Jay tangu niko shule A-lever mpala O-lever. Lakini baadaye nimefahamiana naye tulipokuwa Bungeni wote akawa rafiki yangu, ndugu yangu na Mwananchama mwenzangu. Hili ni jambo kubwa na tumeliunga mkono kwa sababu ni sehemu ambayo imetengeneza ajira kwa vijana,”amesema Heche