Njombe. Watanzania wametakiwa kuwakumbuka watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu kwa kuwapatia misaada inayohitajika, ili nao waishi kwa furaha kama ilivyo kwa watoto wengine wanaoishi na wazazi wao.

Wito huo umetolewa leo Mei 3, 2026 na Mkurugenzi wa Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Compassion, Sister Lusia Mlowe, wakati wakipokea msaada wa vitu kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (Tughe) Mkoa wa Njombe katika hafla fupi iliyofanyika mkoani hapa.

Amesema jamii ina wajibu wa kuona kuwa yapo makundi mbalimbali ambayo yanahitaji msaada wao, hivyo wajitahidi kuwakumbuka mara kwa mara kwa kuwapatia mahitaji muhimu.

Mkurugenzi wa Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Compassion, SR lusia Mlowe akizungumza baada ya kupokea msaada kutoka chama cha wafanyakazi mkoani Njombe waliotembelea kituo hicho kwa ajili ya kuwapa matumaini na faraja kwa kutoa mahitaji muhimu.

Amesema watoto hao wanakabiliwa na changamoto nyingi, lakini si rahisi wao kutoka kwenye vituo na kwenda kuomba, bali ni jamii inatakiwa kuwatembelea na kuwaona.

Ameishukuru Tughe kwa upendo wao wa kuwatembelea na kuwaona baada ya kumalizika kwa sherehe za maadhimisho ya Mei Mosi ambazo kitaifa zilifanyika mkoani Njombe.

“Tunawashukuru sana Tughe kwani watu wengi huwa hawaguswi na kitu hiki, lakini wafanyakazi hawa wameguswa; Mungu awabariki,” amesema Sister Mlowe.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (Tughe) Mkoa wa Njombe, Mashaka Kisulila, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tughe Taifa, Joel Kaminyoge, amesema wameguswa na malezi ya watoto hao, wakiwa pia wanaishi katika jamii na wana hofu ya Mungu.

Amesema wameona wawapelekee vitu mbalimbali watoto hao, ikiwemo televisheni na king’amuzi, ili wapate fursa ya kuangalia matukio mbalimbali yanayoendelea duniani.

“Kwa hiyo sisi kwa pamoja Tughe Mkoa wa Njombe na Tughe Taifa tumeona tulete sadaka hii na kufanya matendo ya huruma ikiwa ishara ya kumshukuru Mungu kwa kushiriki Mei Mosi kwa pamoja na kumaliza salama,” amesema Kisulila.

Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Mkoa wa Njombe, Mashaka Kisulila akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa TUGHE Taifa Joel Kaminyoge baada ya kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Compassion kilichopo halmashauri ya mji wa Njombe.

Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (Tughe), Angel Chipindula, amesema chama hicho kitaendelea kuyafikia makundi mbalimbali na kutoa msaada kama sehemu ya kurudisha kwa jamii inayowazunguka.

“Niwashukuru wageni wote wa Tughe waliofika Njombe, na kwa hili walilolifanya sisi Njombe tumejisikia vizuri. Hawaishi huku lakini waliona hawa watoto, kwa kifupi tu wakaona wanahitaji kufanya kitu,” amesema Chipindula.

Stanslaus Danda ni mmoja wa watoto wanaoishi katika kituo hicho cha Compassion, amekishukuru chama hicho cha wafanyakazi kwa kutoa msaada huo hasa televisheni ambayo itawasaidia kuona matukio mbalimbali.

“Tunawashukuru wafanyakazi wa Tughe kwa kutuletea TV tuangalie mambo yanayoendelea duniani, tunasema asante na Mwenyezi Mungu awazidishie,” amesema Danda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *