Mwanza. Viongozi wa vyama vya upinzani wameitaka Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuweka kamera za kudhibiti mwendo kasi katika Daraja la JP Magufuli ili kuimarisha usalama wa watumiaji wa daraja hilo.

Wito huo umetolewa Mei 2, 2026 na viongozi hao kutoka vyama rafiki vya siasa 13, wakiwamo waliokuwa wagombea urais mwaka 2025, mara baada ya kutembelea na kukagua daraja hilo lililojengwa kwa zaidi ya Sh700 bilioni na kuzinduliwa Juni 19, 2025 na Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza katika ziara hiyo, Katibu Mkuu wa Chama cha Makini, Ameir Hassan amesema ni wakati sasa kwa Tanroads kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa kuweka kamera zitakazosaidia kudhibiti mwendo kasi badala ya kutegemea uwepo wa askari.

“Niwaombe sana Tanroads, sasa hivi mambo ya sayansi na teknolojia yamekuwa. Tumeshuhudia hapa magari yanapita kwa mwendo kasi. Zifungwe kamera kama nchi za wenzetu wanavyofanya.

Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wakiwa kwenye daraja la JP Magufuli

“Hatuna haja ya kuweka askari hapa, tufunge kamera zinazorekodi matukio na moja kwa moja mtu apate faini kulingana na kosa lake,” amesema.

Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yataongeza nidhamu kwa madereva na kusaidia kupunguza ajali katika daraja hilo.

Amependekeza Serikali kuangalia uwezekano wa kuondoa tozo katika baadhi ya madaraja ili kupunguza malalamiko ya wananchi.

“Kwa kuwa daraja hili linatumika bure kwa watembea kwa miguu na madereva, ni vyema Serikali ikaangalia uwezekano wa kuondoa tozo katika madaraja mengine pia. Bado kuna malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, hivyo daraja hili liwe mfano wa kuigwa,” amesema.

Katibu Mkuu wa Union Multiparty Democracy (UMD), Moshi Kigundula amesema awali alikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu utekelezaji wa mradi huo kutokana na ukubwa wake pamoja na gharama kubwa zilizohusika.

“Mradi huu ulipoanza nilikuwa na wasiwasi sana. Nilikuwa na wasiwasi kutokana na ukubwa wake na mazingira ya wakati huo, hasa msimamo wa uongozi wa nchi katika kipindi hicho ndani na nje ya nchi. Nilijiuliza kama Watanzania tutaweza kuutekeleza,” amesema Kigundula.

Amesema baada ya changamoto mbalimbali, kikiwamo kifo cha aliyekuwa Rais wa wakati huo, John Magufuli kulizuka hofu zaidi kuhusu hatima ya mradi huo, lakini sasa ana furaha kuona umekamilika kwa kiwango cha juu.

“Leo nina furaha kubwa kwa sababu nimefika kujionea mradi huu umekamilika. Daraja limejengwa kwa ubora wa hali ya juu, ni zuri na linavutia. Hii ni fahari kwa Taifa,” amesema.

Naye, Mwenyekiti wa Chama Cha Kijamii (CCK), David Mwaijojele amesema vyama vya siasa vina wajibu wa kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha maendeleo yanaendelea kupatikana.

“Sisi tupo bega kwa bega na Serikali kuhakikisha maendeleo yanakwenda mbele kutoka hapa tulipoanzia sasa,” amesema.

Mwenyekiti wa Democratic Party (DP) na Mwenyekiti wa vyama rafiki, Abdul Mluya amesema ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda miundombinu ya nchi kwa kufuata sheria na taratibu.

Mwenyekiti wa Chama Cha DP ambaye pia ni Mwenyekiti wa Vyama rafiki vya siasa, Abdul Mluya akizungumza baada ya kukagua daraja la  JP Magufuli. Picha na Saada Amir

“Watumiaji wote wa daraja hili wanapaswa kuheshimu sheria ili kulinda uwekezaji huu mkubwa. Tukiharibu miundombinu hii, tunahatarisha manufaa yake kwa vizazi vijavyo,” amesema.

Ameongeza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kuimarisha ulinzi katika miradi mikubwa kwa kutumia pia teknolojia ya kisasa.

“Ni muhimu kuweka ulinzi mkali pamoja na kamera ili kudhibiti vitendo vya uharibifu na mwendo kasi. Hii itasaidia kujenga nidhamu kwa watumiaji wote,” amesema.

Mwenyekiti wa Baraza la vyama vya siasa na Mwenyekiti wa Tadea, Juma Khatibu amesema ziara hiyo imelenga kuwahamasisha Watanzania kutambua na kuthamini rasilimali za nchi.

“Lengo letu ni kuwaelimisha Watanzania wajue thamani ya mali zao na miradi ya maendeleo. Serikali imefanya kazi kubwa, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kulinda mafanikio haya,” amesema.

Kwa upande mwingine, Katibu Mkuu wa United Democratic Party (UDP) na aliyekuwa mgombea urais, Saumu Rashid amesema elimu kwa umma ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inalindwa na kudumu kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Richard Lyimo amewataka wanasiasa kusema ukweli kuhusu miradi ya Serikali badala ya kueneza upotoshaji unaoweza kuwapotosha wananchi.

Muonekano wa daraja la JP Magufuli ambalo lipo Mwanza kuweka kamera za kudhibiti mwendo kasi ili kuimarisha usalama wa watumiaji wa daraja hilo.

Katibu Mkuu wa Alliance for African Farmers Party (AAFP), Rashid Rai amesema mafanikio ya miradi mikubwa yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa amani nchini, akisisitiza kuwa ni muhimu kuendelea kulinda utulivu huo.

Katibu Mkuu wa Chama Cha National League for Democracy (NLD) na aliyekuwa mgombea urais, Doyo Hassan amesema amani ni msingi muhimu wa maendeleo na akatoa wito kwa Watanzania kushirikiana kulinda mshikamano wa Taifa.

Amesisitiza kuwa bila utulivu wa nchi, utekelezaji wa miradi mikubwa kama Daraja la JP Magufuli usingewezekana, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha amani inaendelea kudumishwa.

Akimuwakilisha Meneja wa Tanroads Mkoa wa Mwanza, William Sanga amesema tayari mchakato wa kuweka CCTV camera umeanza pamoja na ujenzi wa kituo cha polisi.

“Suala hilo lipo ndani ya mpango kazi kwa sasa ni kazi ambazo mkandarasi anaendelea nazo za kufunga CCTV camera kuanzia kwenye barabara unganishi na daraja zima ambazo zitaunganishwa na chumba maalumu ambapo daraja litatazamwa kwa saa 24,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *