
Katika karne hii ya 21, kumekuwapo na mabadiliko makubwa ya kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.
Hata hivyo, mabadiliko haya yameibua changamoto mpya na nzito: kuongezeka kwa wimbi la wanaume “waoga” ndani ya nyumba.
Uoga huu si wa kimwili, bali ni ule wa kisaikolojia na kiroho unaomfanya mwanamume ashindwe kubeba dhima ya uongozi aliyokabidhiwa na asili.
Badala ya kuwa nguzo ya nyumba, mwanamume muoga amekuwa mzigo, chanzo cha migogoro, na hatimaye janga linalosababisha kusambaratika kwa familia nyingi.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa uhusiano, Silvia Joackim, mabadiliko ya mifumo ya maisha na malezi, yamekuwa na mchango mkubwa katika hali ya baadhi ya wanaume kushindwa kubeba jukumu la uongozi ndani ya familia.
“Mwanaume hushindwa kuongoza si kwa kukosa uwezo bali mara nyingi ni kwa kukosa kujiamini na uelewa wa nafasi yake katika mazingira ya sasa ya maisha,” anasema.
Anaeleza kuwa wanaume wengi hawakupata mifano sahihi ya uongozi walipokuwa wakikua, jambo linalowafanya kushindwa kufanya uamuzi wanapokuwa katika familia zao na hatimaye kujikuta wakikwepa wajibu wao.
Naye mchambuzi wa masuala ya familia, Efreim Kolimba, anasema uongozi wa mwanaume ndani ya nyumba, haupaswi kutafsiriwa kama ubabe, bali ni wajibu wa kusimamia, kulinda na kubeba uamuzi wa familia kwa busara.
Anaongeza kuwa kukwepa jukumu hilo kunaweza kuleta pengo la uamuzi na kuathiri ustawi wa familia kwa jumla.
“Ukikwepa jukumu la kuongoza, wengine wataongoza maisha yako,” anasema.
Maeneo ya uoga
Kimsingi, uoga huu unajidhihirisha katika namna mbalimbali, kuanzia kukwepa kufanya uamuzi mgumu, kutojua majukumu ya msingi, hadi ukaidi wa kutotaka kujifunza wala kutafuta maarifa ya kuongoza ndoa.
Kutofanya uamuzi
Mwanaume muoga anatambulika kwa sifa moja kuu: Kushindwa kufanya uamuzi. Katika familia, mwanamume anapaswa kuwa dira.
Lakini mwanamume muoga huishi kwa hofu ya kukosea, hofu ya kulaumiwa, na hofu ya kuonekana mbaya.
Matokeo yake, anashindwa kutoa msimamo kwenye mambo ya msingi kama vile maendeleo, nidhamu ya watoto, au hata matumizi ya fedha ndani ya nyumba.
Mwanamume wa aina hii huachia mke kila kitu. Mke anapouliza, “Tutafanya nini kuhusu ada?” au “Nyumba yetu inaelekea wapi?”, jibu la mwanaume huyu mara nyingi ni, “Wewe unaonaje?” au “Tutaona mbele.”
Aidha, wanaume hawa hawajui majukumu yao ya msingi. Hawajui kuwa mwanamume ni mlinzi wa hisia, usalama na mwelekeo wa familia.
Wao huchukulia majukumu kama kutoa fedha pekee (tena kama wanazo), wakisahau kuwa uongozi ni zaidi ya pochi.
Ukaidi wa kutojifunza
Tatizo kubwa zaidi linalomfanya mwanamume muoga kuwa hatari ni kukataa kujifunza.
Kuna dhana potofu miongoni mwa wanaume wengi kuwa “kujua kila kitu” ni sifa ya kiume. Hivyo, hata wanapokwama, hawataki kusoma vitabu, hawahudhurii semina za ndoa, na wala hawatafuti washauri wa kuwaongoza.
Uoga wao unawafunga kwenye gereza la ujinga. Wanaogopa kuonekana hawajui, hivyo wanajivika vazi la ujuaji ambalo halina maarifa ndani yake.
Dunia inabadilika, mahitaji ya wanawake yanabadilika, na malezi ya watoto yanazidi kuwa magumu kutokana na teknolojia.
Mwanamume asiyetaka kutafuta maarifa mapya ni kama nahodha anayetumia ramani ya mwaka 1920 kuongoza meli mwaka 2026; ni lazima agonge mwamba.
Mwanamume muoga anaogopa kuambiwa ukweli. Anapoelezwa upungufu wake, badala ya kufanyia kazi, anatumia hasira kama kinga ya kufunika uoga wake.
Hii inamfanya ashindwe kukua. Mwanaume wa kweli ni yule anayekiri kuwa hajui jambo fulani na yuko tayari kuketi chini na kujifunza namna ya kuwa mume bora au baba bora.
Mkwamo wa migogoro
Uoga unajidhihirisha zaidi pale migogoro inapotokea. Kwenye ndoa yoyote, kutofautiana ni jambo la kawaida, lakini kwa mwanamume muoga, ugomvi ni mlima usioweza kupandika.
Badala ya kukaa chini na mkewe, kuzungumza kwa hoja, na kutafuta suluhu ya kudumu, mwanamume huyu ana tabia kuu mbili: kukaa kimya au kukimbia
Anapokosana na mwenza wake, hajui la kufanya. Anaogopa kukabiliana na hisia za mkewe. Anashindwa kuomba msamaha hata kama amekosea, kwa sababu anaona kuomba msamaha ni udhaifu.
Vilevile, anashindwa kutoa msamaha kwa sababu anaogopa kuonekana ameshindwa vita. Hivyo, kero ndogo hukua na kuwa donda ndugu.
Wanaume hawa wamekuwa wepesi wa kufikiria kuachana kuliko kupambania ndoa zao.
Ni rahisi kwao kuanza maisha mapya na mwanamke mwingine (ambako nako wataenda kufeli) kuliko kurekebisha kile walichonacho.
Huu ndio uoga uliopitiliza, yaani uoga wa kushindwa “kufanya kazi” ya ndoa. Ndoa ni kazi inayohitaji ujasiri wa kukabiliana na upungufu wako na wa mwenza wako.
Ni lazima jamii ianze kuzungumza waziwazi kuhusu hali hii. Wanaume wanapaswa kuelewa kuwa ujasiri si kupiga meza au kuwa na sauti nzito, bali ni uwezo wa kusimamia uamuzi, kubeba majukumu, na kuwa na unyenyekevu wa kutafuta maarifa pale wanapopungukiwa.
Ili kuokoa familia, mwanamume lazima auvae ujasiri wa kiakili. Lazima akubali kuwa kiongozi si kuwa mtawala, bali ni kuwa mtumishi wa kwanza wa familia yake.