
Katika pitapita yetu mitandaoni, tumeona clips nyingi zinazopotosha hasa kwa wanandoa.
Leo, tutaongelea suala zima la ‘chakula cha usiku’ hata ‘kifungua kinywa’ kwa wanandoa. Katika kusikiliza, kuna moja ilituvutia, kutufikirisha, kutustua, na kutufanya tujadili suala hili nyeti. Tunapoongelea chakula cha usiku, tunaamini wanandoa wanatuelewa.
Kuna mtu anayejiita mtaalamu. Anawanasihi wanandoa eti wasile chakula cha usiku muda mrefu. Yeye anapendekeza wasizidishe dakika mbili. Ukiuliza ni kwanini? Anaseme eti tuwachunguze wanyama huwa wanafanya kitu hii kwa muda gani.
Yeye anapendekeza dakika mbili kama kuku. Kwanza, binadamu si wanyama na wana tofauti katika karibu kila jambo japo mahitaji yao ya kibailojia yaweza kuwa sawa au kukaribiana.
Pili, wanyama, japo si wote, hawawezi kula chakula cha usiku kwa muda mrefu kwa sababu wengi hawana mikono wala mazingira wezeshi. Pia, wanyama na binadamu tuna maumbile na mahitajio tofauti linapokuja suala la chakula cha usiku.
Mfano, twiga, kimaumbile, hawezi kula kwa muda mrefu. Wakati twiga hana uwezo huo, jiulize. Nguruwe, aina fulani ya nyoka hasa ‘rattlesnakes’ wanaweza kula hata kwa saa kadhaa. Mbali na hao, hata mbwa hula kwa muda mrefu. Je, hawa siyo wanyama?
Tatu, wanyama hawana mazingira mazuri ya kulia chakula cha usiku. Hivyo, kuwalinganisha na wanadamu ni kukosa maarifa au kutaka kupotosha kama siyo kutafuta sifa kwa kusema vitu visivyoingia akilini.
Nne, j swali ni je, wanandoa watumie muda gani kula chakula cha usiku? Kimsingi, hakuna muda maalum ijapokuwa kula kwa muda mrefu kuna raha yake.
Kuna tofauti ya kula na kupwakia. Binadamu hapaswi kupwakia. Hivyo, ni muda gani wanandoa wale chakula cha usiku, hakuna jibu moja wala mawili.
Kwani, mosi, hutegemea na afya ya wahusika. Kama wahusika wana afya nzuri, wataweza kuhimili mikiki hata kwa saa nzima au pungufu au zaidi.
Tano, hutegemea na maandalizi kabla ya kula chakula. Wanyama wanaotumia muda wa dakika mbili kula chakula cha usiku, mara nyingi, hurukiana.
Binadamu hawapaswi kufanya hili. Ndiyo maana, tunasema, tena kutokana na uzoefu si wa miaka 10 wala 20 kuwa kuna tofauti kubwa baina ya wanyama na binadamu.
Sita, mbali na maandalizi, pia, inategemea na wahusika wana njaa au tuseme hamu kiasi gani. Wanakula baada ya muda gani ingawa hakuna ratiba ya kula iwapo afya zao na uzoefu vinaruhusu.
Wapo wanaojiita wataalamu wanaoweka hata ni mara ngapi wahusika wale chakula cha usiku. Kimsingi, hakuna muda wa mara ngapi. Mwili umepewa uwezo wa kutaka au kutotaka kula.
Kama manjisikia mna hamu ya kula, kuleni bila kujali upuuzi kama vile wanaume wanapunguza nguvu zao na kuhatarisha maisha yao kwa kula mara kwa mara chakula cha usiku. Si kweli.
Saba, wanasayansi wa masuala ya ndoa na mwili wa binadamu wanakubaliana kuwa kula chakula cha usiku mara kwa mara huimarisha afya ya akili na moyo, kinga, huongeza usingizi, pia, hupunguza uwezekano wa kupata tezi dume kwa wanaume.
Nane, kwa vile walengwa ni watu wazima na wenye uzoefu, kwa wale wasiojibana au kusikiliza wataalamu uchwara, jiulize. Huwa mnakula chakula cha usiku mara ngapi hata kwa siku, wiki, au mwezi?
Tisa, kwa wale ambao umri umeenda, uwezo wa kula chakula cha usiku unaweza kukuhakikishia kuwa afya yako ni njema. Mbali na hili, chakula cha usiku ni sehemu muhimu katika maisha ya binadamu inayowapatia fursa kufanya mazoezi ya viungo bila kuteseka wala kugharimia hasa kwa wale wanaokwenda kwenye gyms.
Mbali na yote hapo juu, hamu ya chakula cha usiku ni kigezo au ushahidi kuwa wawili si wanapendana tu bali wanahitajiana na kutegemeana.
Tutoe angalizo na onyo. Tunaposema ulaji wa chakula cha usiku ni muhimu kwa wanandoa, hatumaanishi watu wale kila chakula. Hapana, kufanya hivyo, ni kutafuta magonjwa na kuzalisha watoto wasiopangiliwa wala kuhitajika.
Tumalizie kwa kuwasihi wanandoa wasikilize mahitaji, miitikio, na uwezo wa miili yao katika jambo hili. Kimsingi, ulaji wa chakula cha usiku, kwa walio katika ndoa, hauna masharti wala kufundishwa zaidi ya kusikiliza miili na nyoyo zenu.