Nyota wa zamani wa Chelsea, Marseille, Galatasaray na timu ya taifa ya Ivory Coast, Didier Drogba, ameteka ukumbi wa Bunge baada ya kutangazwa jina lake na Spika.

Drogba (48), ametambulishwa Bungeni kama mgeni wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda akiwa miongoni mwa wageni katika siku ambayo hotuba ya wizara hiyo inasomwa leo.

Mapema asubuhi leo, Drogba ameingia tofauti na wageni wengine ambao hutumia lango C ambapo ametumia lango A ambalo ni maarufu kama lango la Waziri Mkuu.

Baada ya kuingia, Drogba amepokewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa.

Mara baada ya Spika, Mussa Azzan Zungu kumtambulisha, wabunge walipiga makofi kwa sauti za juu na kuchukua muda mrefu kuliko mgeni mwingine yeyote aliyetambulishwa kwa siku ya leo.

Hata hivyo, utambulisho wa Drogba na kocha Mkuu wa Taifa Stars, Miguel Gamondi ulikuwa tofauti kwani wageni wengine walitambulishwa na Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga, lakini wawili hao walitambulishwa na Spika.

Hii si mara ya kwanza kwa Didier Drogba kutua Tanzania kwani alishawahi kuja na timu ya Taifa ya Ivory Coast kucheza dhidi ya Taifa Stars Januari 4, 2010, mechi ya kirafiki jijini Dar es Salaam katika Uwanja wa Benjamin Mkapa. Katika mchezo huo, Ivory Coast ilishinda 1-0 kwa goli lililofungwa na Didier Drogba.

Juni 16, 2013, Ivory Coast ilicheza tena dhidi ya Tanzania jijini Dar es Salaam katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia (Tanzania 2-4 Ivory Coast). Hata hivyo, Drogba hakushiriki katika mchezo huu kwani licha ya kuja na kikosi alikuwa majeruhi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *