
Kamanda wa kitengo cha juu zaidi cha uendeshaji wa operesheni za kijeshi cha Iran ameonya kuwa majeshi ya Iran yatalenga vikosi vyovyote vya kigeni, hasa vile vya Jeshi la Marekani, vitakavyojaribu kukaribia au kuingia katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, njia nyeti ya kimkakati ya baharini.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, Meja Jenerali Ali Abdollahi, kamanda wa Makao Makuu ya Khatam al-Anbiya, amesisitiza tena kuwa usalama wa Mlango wa Bahari wa Hormuz uko chini ya mamlaka ya pekee ya vikosi vya kijeshi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amebaini kuwa kupita salama kwa meli zote katika njia hiyo muhimu ya maji lazima kuratibiwe na vikosi vya kijeshi vya Iran. Jenerali Abdollahi amesema kuwa “viongozi wahalifu na jeshi la Marekani lenye hulka ya uchokozi na ugaidi” hivi karibuni wamegeukia vitendo vya uharamia na uporaji katika maji ya kimataifa, hatua inayohatarisha biashara ya kimataifa na usalama wa uchumi wa dunia.
Ameonya kuwa viongozi hao, pamoja na washirika wao, wanapaswa kufahamu kwamba “taifa la Iran lenye msimamo thabiti na ujasiri,” pamoja na vikosi vyake vya kijeshi, litajibu tishio au uchokozi wowote, kwa kiwango chochote na katika eneo lolote la Iran, kwa “majibu makali na yenye majuto.”
Kamanda huyo amethibitisha kuwa Iran itaendelea kulinda na kusimamia kwa uthabiti usalama wa Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Aliwataka wamiliki wa meli za kibiashara na meli za mafuta kuepuka jaribio lolote la kupita bila uratibu wa awali na vikosi vya kijeshi vilivyopo katika mlango huo, akionya kuwa kutofanya hivyo kunaweza kuhatarisha usalama wao.
Pia amewaonya wanaounga mkono Marekani, akisema kuwa “waungaji mkono wa Marekani dhalimu” wanapaswa kuwa waangalifu na kujiepusha na hatua zozote zitakazoweza kuleta majuto.
Ameonya kuwa hatua yoyote ya kichokozi ya Marekani inayolenga kuvuruga hali ya sasa haitazaa matokeo mengine isipokuwa kuzidisha mivutano na kuhatarisha usalama wa meli katika eneo hilo.
Rais wa Marekani, Donald Trump, amedai katika kauli za hivi karibuni kuwa Marekani itakuwa “ikihakikisha uhuru wa harakati za meli katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.”
Aliongeza kuwa hatua hizo zingeanza asubuhi ya Jumatatu kulingana na saa za Asia Magharibi.
Tangu Februari 28, wakati Marekani na Israel zilipoanzisha vita vya uchokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Iran imezuia Mlango wa Bahari wa Hormuz kwa meli za mafuta na gesi zinazohusishwa na tawala hizo pamoja na zile zinazoshirikiana nazo, ikiwa ni jitihada ya kudumisha usalama katika njia hiyo muhimu ya kimkakati.