
DODOMA: SERIKALI imesema hadi kufikia mwezi Aprili 2026 Sh milioni 699 sawa na asilimia 67.5 zilikusanywa kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato, hata hivyo kiwango hicho hakijafikia lengo la mwaka wa fedha 2025/2026 la kukusanya Sh bilioni 1 kutoka katika vyanzo sita vya Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo.
Vyanzo hivyo ni viwanja vya Benjamin Mkapa na Uhuru, ada za mafunzo na mitihani kutoka Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, vitambulisho vya waandishi wa habari, machapisho ya picha, mabango na majarida, usajili wa magazeti, na ada ya mwaka ya magazeti 28.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda ametoa takwimu hizo wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 leo Mei 04, bungeni jijini Dodoma.
“Miongoni mwa sababu za kutofikia kwa lengo ni pamoja na kupungua kwa matukio katika viwanja vya Benjamin Mkapa na Uhuru kutokana na kufungwa kulikotokana na ukarabati unaoendelea katika viwanja hivyo,” amesema Makonda.