Mshambuliaji wa Kagera Sugar, raia wa Zambia Obrey Chirwa, anaendelea kutesa huko kwenye ligi ya Championship zamani daraja la kwanza akishika nafasi ya kwanza katika chati ya wafungaji msimu huu wa 2025/2026.

Nyota huyo ambaye alitua hapa nchini Julai Mosi 2016 akijiunga na Mabingwa wa Kihistoria Wananchi, Yanga akitokea FC Platinum ya Zimbabwe bado anaendelea kuonyesha makali yake huko Championship kwenye viunga vya Kaitaba, Kagera.

Chirwa aliachana na Yanga Julai 17, 2018, kisha akajiunga na Nogoom FC ya Misri, kabla ya kurejea tena hapa nchini kujiunga na Azam FC, Novemba 8, 2018, huku akiichezea pia, Hobro IK kutoka Denmark.

Licha ya kuchezea timu mbalimbali hapa nchini, mshambuliaji huyo kwa sasa anaichezea Kagera Sugar, inayoshiriki Ligi ya Championship msimu huu, huku akionyesha kiwango bora cha kuipambania nembo ya Kagera Sugar kurejea tena katika Ligi Kuu msimu ujao.

Mshambuliaji wa Kagera Sugar, raia wa Zambia Obrey Chirwa. Picha na Mtandao

Kinara wa mabao

Chirwa amekuwa na mwendelezo mzuri wa kufunga mabao ambapo mshambuliaji huyo ndiye anayeongoza akiwanayo 14, akifuatiwa na Adam Uledi aliyekuwa Transit Camp, na sasa KMC FC na Ramadhan Hashim wa B19 FC waliofunga 11, kila mmoja.

Rekodi ya mabao matatu (hat-trick)

Mshambuliaji huyo, anashikilia rekodi ya mchezaji wa kwanza wa Ligi ya Championship msimu wa 2025-2026 kufunga mabao matatu (hat-trick), wakati kikosi hicho cha Kagera Sugar kilipoifunga Hausung FC ya Njombe mabao 3-1, Desemba 2, 2025.

Katika mchezo huo uliyochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba, Chirwa alifunga mabao hayo, na kufikisha 14, akiwa ndiye anayeongoza.

mshambuliaji mwingine aliyefunga hat-trick ni Boniface Mwanjonde wa Mbeya Kwanza ambaye alipachika mabao matatu katika ushindi wa mabao 5-0, dhidi ya B19 FC, Desemba 17, 2025.

Mshambuliaji wa Kagera Sugar, raia wa Zambia Obrey Chirwa. Picha na Mtandao

Timu moja, mabao mawili

Chirwa mwenye umri wa miaka 32 anayo historia ya kuifunga timu moja mabao mawili huku yeye akizichezea timu mbili tofauti zilizokuwa katika Ligi Kuu.

Msimu wa 2024-2025, Chirwa alianza kuichezea Kagera Sugar, ambayo aliifungia bao moja, wakati kikosi hicho kilipochapwa mabao 3-1, dhidi ya Fountain Gate, katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa, Septemba 27, 2024.

Baada ya kuichezea Kagera, dirisha dogo la Januari 2025, nyota huyo alijiunga na KenGold kwa mkopo, ambayo aliifungia pia bao moja, katika ushindi wa kikosi hicho wa mabao 2-0, dhidi ya Fountain Gate, mechi iliyopigwa, Februari 10, 2025.

Alivyoshuka daraja

Katika timu alizocheza mshambuliaji huyo kwa msimu wa 2024-2025, kwa maana ya Kagera Sugar na KenGold, zote zimeshuka daraja, zikitoka Ligi Kuu Bara na kushiriki Ligi ya Championship, kutokana na kutokuwa na mwenendo mzuri kwa msimu huo. Kagera iliyodumu katika Ligi Kuu Bara kwa miaka 20, tangu ilipoanza kushiriki 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024-2025, baada ya kushinda mechi tano tu, sare mara nane na kupoteza mara 17, ikishika nafasi ya 15, kufuatia kukusanya pointi zake 23.

Timu hiyo inayonolewa na aliyekuwa golikipa nyota wa Simba, Yanga na timu ya Taifa Stars, Juma Kaseja aliyewahi kuitumikia pia Kagera Sugar akiwa mchezaji na kocha wa makipa, kwa sasa anakipambania kikosi hicho ili kirejee tena katika Ligi Kuu Bara.

Kwa upande wa KenGold baada ya msimu bora wa 2023-2024, ilipotwaa ubingwa wa Championship, mambo yalikuwa tofauti, kwani iliposhiriki Ligi Kuu msimu wa 2024-2025, iliburuza mkiani kwa pointi 16, ikishinda mechi tatu, sare saba na kupoteza mara 20.

Mshambuliaji wa Kagera Sugar, raia wa Zambia Obrey Chirwa. Picha na Mtandao

Mfungaji bora kombe la FA

Miongoni mwa kumbukumbu nzuri kwa Chirwa katika soka la Tanzania, ni kuibuka pia mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho la FA, ambapo nyota huyo anakumbukwa msimu wa 2016-2017, aliibuka kinara, baada ya kufunga mabao matano akiwa na Yanga.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, Azam, Namungo, Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars na KenGold, aliibuka kidedea msimu huo wa 2016-2017, ikiwa ni msimu wa pili tangu michuano hiyo iliporejea tena kuchezwa baada ya kutofanyika kwa miaka 13, mfululizo, tangu mara ya mwisho iliposimama ikifahamika kwa Kombe la FAT mwaka 2002.

Katika msimu wa 2016-2017, Chirwa alifunga mabao hayo matano ya Kombe la FA na kuibuka kinara wa ufungaji bora, ingawa, nyota huyo alikosa ubingwa huo wa michuano hiyo, baada ya kuchukuliwa na watani zao Simba iliyoifunga Mbao FC mabao 2-1.

Kinachomsubiri

Iwapo mambo yakienda vyema tunaweza kumuona tena Chirwa akirejea upya Ligi Kuu ambapo hadi sasa Chama lake la Kagera Sugar linashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi ya Championship kwa pointi 55 zikiwa ni pointi tatu nyuma ya vinara Geita Gold ambao wameshakusanya idadi ya pointi 58 hadi sasa katika michezo 23.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *