
Dodoma. Mbunge wa zamani na aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi ameongoza katika matokeo ya uwakilishi wa ubunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA).
Chumi amepata kura 219 sawa na asilimia 98.6 ya idadi ya kura zote 223 zilizopigwa, huku kura nne zikimkataa, idadi ambayo ilimfanya awe mbele ya wagombea wenzake kwenye nafasi hizo tatu zilizokuwa zikigombewa.
Wabunge wengine waliochaguliwa leo Jumatatu, Mei 4, 2026 ni Kambarage Wasira ambaye amepata kura 214 sawa na asilimia 96.6, na kura tisa zilimkataa, huku Fatuma Kange ambaye amepata kura 153 akikataliwa na wabunge 70, hivyo ushindi wake ni asilimia 76.1.
Uchaguzi wa EALA umefanyika kuziba nafasi za waliokuwa wabunge James Ole Milya (Simanjiro), Dk Ngwaru Maghembe (Mwanga) na mbunge wa kuteuliwa Angella Kizigha.
Katibu wa Bunge, Baraka Leonard, ametangaza matokeo hayo kwa kutaja idadi ya walioshiriki kupiga kura kwamba walikuwa 223 kati ya wabunge 401 waliokuwapo, ingawa kwa mujibu wa Katiba, nafasi za ubunge Tanzania ni 404.
“Waheshimiwa wabunge, kwa mujibu wa Katiba Bunge hili lina nafasi 404 za wabunge, lakini waliopo kwa sasa ni wabunge 401, na waliopiga kura leo ni wabunge 223,” amesema Leonard.
Kwa mujibu wa katibu huyo, taarifa za kuchaguliwa kwa wabunge hao zimetokana na kibali cha Spika wa Bunge la EALA baada ya kumjulisha uwepo wa nafasi tatu za wabunge wa Tanzania kutokana na kanuni zinazozuia wabunge wa kuchaguliwa au kuteuliwa katika Taifa lolote ndani ya Jumuiya hiyo kuwa wabunge wa EALA.
Spika wa Bunge, Mussa Zungu, amewaagiza wachaguliwa hao kwenda kusimamia umoja wa kitaifa, kushughulikia masuala ya biashara ili Taifa linufaike, na pia wakaangalie mipaka ya Taifa.
Zungu amesema kama ambavyo Bunge limewaamini na kuwachagua, ndivyo ambavyo nao wanatakiwa kurudisha fadhila kwa wapiga kura na Watanzania, na hilo linawezekana ikiwa watakuwa na umoja na ushirikiano.