Kibaha. Tume ya Taifa ya Mipango imezindua mafunzo ya Mwongozo wa Kitaifa wa Uidhinishaji wa Miradi ya Maendeleo (NDPAG) kwa lengo la kuimarisha ubora wa miradi ya maendeleo nchini.

Mafunzo hayo yameanza leo Mei 4, 2026 Kibaha mkoani Pwani yakihusisha wakurugenzi wa sera na mipango, wakurugenzi wa ufuatiliaji na tathmini pamoja na wakuu wa idara na vitengo kutoka wizara na taasisi za Serikali.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Katibu Mkuu wa Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dk Tausi Kida amesema lengo la mafunzo hayo ni kujenga uelewa wa pamoja kuhusu matumizi sahihi ya mwongozo huo.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo yaliyoandaliwa na Tume ya Mipango wakifuatilia mada mbalimbali leo, Mei 4, 2026. Picha na Sanjito Msafiri.

Amesema mwongozo huo ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inaandaliwa na kuidhinishwa kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.

“Tunataka kuona miradi yenye ubora, yenye matokeo chanya na inayotekelezwa kwa ufanisi huku rasilimali za umma zikitumika ipasavyo,” amesema.

Ameongeza kuwa kupitia mwongozo huo, Serikali inalenga kurahisisha uamuzi wa vipaumbele, kuimarisha uwajibikaji pamoja na kuongeza tija katika matumizi ya fedha na nguvu kazi.

Dk Kida amesema washiriki wa mafunzo hayo wanatarajiwa kuleta mageuzi katika maeneo muhimu ikiwamo kuboresha maandalizi ya miradi yenye matokeo makubwa, kuimarisha uchambuzi wa vipaumbele, kuongeza ufanisi wa utekelezaji pamoja na kukuza uwazi na uwajibikaji.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo yaliyoandaliwa na Tume ya Mipango wakifuatilia mada mbalimbali leo, Mei 4, 2026. Picha na Sanjito Msafiri.

Amewataka washiriki kutumia mafunzo hayo kuwa chachu ya kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV).

“Matarajio yetu ni kuona mabadiliko chanya katika ubora wa maandiko ya miradi, utekelezaji wake na tathmini ya viashiria vya maendeleo,” amesema.

Awali, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango anayeshughulikia ufuatiliaji na tathimini, Sostenes Kewe amesema kuwa mafunzo hayo ni mwanzo wa mpango wa kuyasambaza nchi nzima kwa taasisi za umma, sekretarieti za mikoa na mamlaka za Serikali za mitaa kupitia kanda mbalimbali.

“Mafunzo haya ni muhimu kwani yanaongeza uelewa kwa watendaji, hivyo imani yetu ni kuwa yataleta mbadiliko chanya,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *