Kupitia taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi, Türk amebainisha kuwa serikali imetumia mashtaka ya jinai na vizuizi vya kiutawala kudhoofisha uhuru wa kujieleza, jambo ambalo limeharibu misingi ya demokrasia iliyopatikana nchini humo tangu mwaka 2011.

“Ukandamizaji na vitendo vya kuzuia haki ya kiraia vinavyofanywa na mamlaka za Tunisia vinadhoofisha haki za watu zinazolindwa chini ya Katiba ya nchi na majukumu yake ya kimataifa ya haki za binadamu,” amesema Türk.

Mashirika ya kiraia yafungiwa

Miongoni mwa mifano ya hivi karibuni ya ukandamizaji huu amesema Mkuu huyo wa Haki za Binadamu ni kusitishwa kwa muda kwa mashirika makubwa ya haki za binadamu na asasi za kiraia. Siku ya Jumanne wiki hii, mahakama ya Tunisia imelisimamisha shirika la kimataifa la Avocats Sans Frontières au mawakili wasio na mipaka kwa siku 30, ikidai kuwepo kwa uzembe wa kikanuni, jambo ambalo limekuja siku chache baada ya kusimamishwa kwa umoja mashuhuri  wa Haki za Binadamu nchini Tunisia.

“Tunaona ongezeko la matukio haya ambapo mamlaka za Tunisia zinatumia vikwazo vilivyowekwa na mahakama kuminya matumizi ya haki ya uhuru wa kujumuika, bila kuzingatia kanuni za uhalali, ulazima, na usawa zinazohitajika ili vizuizi hivyo vikubalike,” ameeleza Türk.

Vizuizi dhidi ya uhuru wa vyombo vya Habari

Vizuizi vya serikali dhidi ya vyombo vya habari vimeendelea kushika kasi, ambapo mnamo tarehe 24 Aprili mwaka huu, mwandishi wa habari Zied El Heni amekamatwa kulingana na sheria inayoelekeza kwamba matumizi ya mitandao ya mawasiliano ni kosa la jinai kwa kigezo cha “kuwadhuru wengine,” na bado anaendelea kushikiliwa kabla ya kesi kusikilizwa. 

Waandishi wengine 28, akiwemo Mourad Zghidi, walikamatwa mwaka jana, wakashtakiwa na kuhukumiwa vifungo mbalimbali gerezani kwa mambo yanayohusiana na kazi zao, kulingana na sheria ya mwaka 2022 ya “kupambana na makosa yanayohusiana na mifumo ya habari na mawasiliano.”

“Natoa wito kwa mamlaka za Tunisia kuwaachilia mara moja na bila masharti wale wote walioshikiliwa au kufungwa kwa kutoa maoni yao, haki hiyo inalindwa chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu, na kuondoa vizuizi vyote vya kiholela dhidi ya uhuru wa kujieleza na kujumuika,” amesema Kamishna Mkuu.

Matumaini ya kidemokrasia nchini Tunisia

Türk amehitimisha akisema, “Mafanikio ya Tunisia ya kidemokrasia na haki za binadamu baada ya mwaka 2011 lazima yalindwe, na siyo kubomolewa hatua kwa hatua.” Huku akisititiza kuwa vikwazo dhidi ya uhuru wa kimsingi lazima vibaki kuwa jambo nyeti, linalozingatia sheria ya wazi, na liambatane na usimamizi madhubuti wa mahakama. 

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR imewatia moyo wabunge wa Tunisia wanaoendelea na juhudi za kufanyia marekebisho sheria hiyo ya mwaka 2022 ambayo imekuwa ikitumiwa kuharamisha ukosoaji na kauli zinazolindwa na Haki za Binadamu, ikiwa ni pamoja na ukosoaji wa maafisa wa umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *