Chanzo cha picha, Getty Images
Mvutano kati ya Marekani na Iran umeongezeka tena baada ya pande hizo mbili kurushiana mashambulizi saa 24 zilizopita, katika tukio linalotajwa kuwa jaribio kubwa zaidi kwa sitisho la vita lililodumu kwa mwezi mmoja.
Hata hivyo, Rais wa Marekani Donald Trump amesema makubaliano ya kusitisha mapigano bado yanaendelea.
Iran ilidai kuwa Marekani ilishambulia meli mbili karibu na Mlango wa Hormuz pamoja na maeneo ya raia katika kisiwa cha Qeshm na pwani ya kusini mwa Iran. Jeshi la Iran limesema lilijibu kwa kushambulia meli za kijeshi za Marekani karibu na bandari ya Chabahar.
Kwa upande wake, Jeshi la Marekani (CENTCOM) limesema lilifanya mashambulizi ya kujibu baada ya Iran kutumia makombora, droni na boti ndogo kushambulia manowari tatu za Marekani. Marekani imesema hakuna meli zake zilizoharibiwa na kwamba haitaki kuongeza mzozo huo.
Akizungumza mjini Washington, Trump alipunguza uzito wa tukio hilo akisema, “Walitujaribu leo, nasi tukawajibu vikali,” huku akisisitiza kuwa sitisho la vita bado lipo. Marekani pia ilikuwa ikisubiri majibu ya Iran kuhusu pendekezo la kusitisha mapigano bila kutatua moja kwa moja suala la mpango wa nyuklia wa Iran.
Baada ya saa kadhaa za mashambulizi, televisheni ya taifa ya Iran iliripoti kuwa hali imerejea kawaida katika visiwa na miji ya pwani karibu na Mlango wa Hormuz, huku Iran ikionya kuwa itajibu kwa nguvu mashambulizi yoyote yajayo.