
Angalau watu 36 wameuawa tangu siku ay Jumanne, Mei 5, katika mashambulizi kadhaa ya waasi wa ADF, wanaohusishwa na kundi la wanajihadi la Islamic State, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kulingana na vyanzo vya ndani na usalama vilivyonukuliwa na shirika la habari la AFP.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Usiku wa Jumanne, Mei 6, kundi la ADF lilifanya mashambulizi katika vijiji kadhaa vilivyotengwa vilivyoko kwenye mpaka kati ya mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini, karibu na eneo la Beni-Mbau (Kivu Kaskazini), kulingana na vyanzo vya ndani na usalama.
Mashambulizi haya yalisababisha vifo vya watu 24 katika vijiji vya Manzungu, Musamba, Wasafi, na Mangambo, vyanzo kadhaa vya ndani huko Beni-Mbau vimethibitisha kwa shirika la habari la AFP. Afisa wa utawala wa eneo hilo, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, pia ameripoti “raia 24 wameuawa” na kadhaa hawajulikani waliko, wengi wao wakiwa wakulima. Vyanzo vya usalama viliambia AFP idadi ya vifo ya kuwa angalau watu 21.
Katika shambulio jipya la ADF siku ya Alhamisi, watu wasiopungua 15 waliuawa huko Biakato, katika eneo la Mambasa katika mkoa wa Ituri. Karibu saa sita mchana, ADF “iliwashangaza wakazi majumbani mwao. Walianza kuwaua watu kwa risasi na mapanga,” kiongozi wa shirika la kiraia huko Biakato ameiambia AFP. “Tayari tumepata miili 15, wakiwemo wanawake watatu, wanaume 11, na mtoto mmoja,” ameongeza. Idadi hii ya vifo ilithibitishwa kwa AFP na kiongozi wa shirika la kiraia katika eneo la Mambasa na vyanzo vya usalama.
Miji iliyolengwa siku ya Jumanne na Alhamisi, iliyo umbali wa takriban kilomita 70, iko katika maeneo yaliyofunikwa na misitu minene ambapo ADF ilitekeleza mauaji mengi katika miaka ya hivi karibuni, mara nyingi ikiwa ni kujibu operesheni za kijeshi.
Jeshi la Uganda limetumwa tangu mwaka 2021 kaskazini mwa mkoa wa Kivu Kaskazini na Ituri kupambana na ADF pamoja na jeshi la Kongo, lakini operesheni ya pamoja, iliyopewa jina la “Shujaa,” haijakomesha vurugu hizo.
Kulingana na shirika la Haki za Binadamu la Amnesty International, ADF imekuwa ikihusika na “utekaji nyara na kazi za kulazimishwa, kuajiri na kutumia watoto, pamoja na vurugu na uhalifu dhidi ya wanawake na wasichana, kama vile ndoa za kulazimishwa” na “mimba za kulazimishwa” nchini DRC. Kundi hilo pia “limezidi kutumia utekaji nyara kwa ajili ya fidia” na “kupata njia za kiteknolojia za hali ya juu” ili kukwepa jeshi, kulingana na shirika lisilo la kiserikali.
Mwanzoni mwa mwezi Aprili, ADF iliwaua watu 43 huko Bafwakoa, mji ulioko magharibi mwa Ituri, na kuzua hofu miongoni mwa waangalizi kwamba eneo la operesheni la kundi hilo linaweza kupanuka hadi mkoa jirani wa Tshopo, ambao umeepushwa na mzozo huo. Katikati ya mwezi Machi, pia walilenga maeneo ya uchimbaji madini yanayoendeshwa na makampuni ya Kichina katika mkoa wa Ituri.
Huko Ituri, zaidi ya watu 100,000 walikimbia makazi yao katika miezi 3
Ukosefu wa usalama katika eneo hilo tayari umesababisha maelfu ya watu kutoroka makazi yao. Kulingana na Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA), zaidi ya watu 100,000 walitoroka makazi yao kati ya mwezi Februari na Aprili 30, 2026, kutokana na ukosefu wa usalama unaoendelea.