Dar es Salaam. Wakazi wa Kimanga, Dar es Salaam, wataanza kukumbana na adha ya usafiri kuanzia kesho baada ya wamiliki wa daladala zinazotoa huduma katika barabara hiyo kutishia kuanza kugoma.
Hatua hiyo imefikiwa kama njia mbadala ya kushinikiza mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kutengeneza barabara ya Kimanga ambayo imeharibika, ikiwa na mashimo hasa kuanzia Madukani hadi Mawenzi yanayojaa maji mengi kipindi hiki cha mvua.
Baadhi ya wamiliki wa daladala wamedai hali ya barabara imekuwa changamoto, kwani imekuwa ikisababisha uharibifu wa magari yao pamoja na kuhatarisha usalama wa abiria na madereva kila siku.
Si hivyo tu, baadhi yao wamedai kuwa magari yamekuwa yakikwama mara kwa mara katika barabara hiyo na kuongeza gharama za matengenezo pamoja na uendeshaji.
Hivi karibuni, Mbunge wa Segerea (Chaumma), Agnesta Kaiza, aliuliza swali bungeni kuhusu barabara za jimboni humo, ikiwemo eneo hilo ambalo limekuwa korofi, akitaka kufahamu mkakati wa Serikali ni upi.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange, alisema mvua zinazoendelea maeneo mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, zimeharibu miundombinu ya barabara na madaraja na kumwagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini (Tarura) Mkoa wa Dar es Salaam kufuatilia na kuchukua hatua.
Akizungumza na Mwananchi leo Mei 10, 2026, Katibu wa Umoja wa Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Shifwaya Lema, amesema taarifa ya kuanza kugoma kwa wamiliki hao ameipata.
Amesema malalamiko ya wamiliki wa daladala hao kuhusu ubovu wa barabara yana hoja ya msingi, kwani yameshafikishwa mezani kwake, akieleza kuwa hali ya barabara si salama kwa uhai wa magari.
Amesema kuwa wamiliki hao wamepanga kusitisha shughuli zao kuanzia Jumatatu ili kupisha matengenezo iwapo mamlaka husika hazitachukua hatua ya kurekebisha barabara hiyo.
“Wamiliki 10 wa daladala wamefika ofisini kuelezea kilio chao. Hali ya barabara si nzuri na inahatarisha usalama wa magari,” amesema.
Lema amesisitiza umuhimu wa viongozi kuchukua hatua za haraka, hata kama ni kwa kumwaga kifusi, ili kuziba mashimo na kufanya barabara hiyo ipitike kwa urahisi, jambo litakalosaidia kuendelea kwa huduma za usafiri zinazotegemewa na wananchi.
“Badala ya wamiliki kusitisha huduma, ni muhimu viongozi wakamwaga hata kifusi kufukia mashimo ambayo yamekuwa kikwazo kwa shughuli za usafiri,” amesema.
Kwa upande wake, Suleiman Salim, ambaye ni mmiliki wa daladala zinazofanya safari barabara hiyo, amesema barabara hiyo imekuwa changamoto kubwa kwao hasa kutokana na gharama kubwa za mafuta na matengenezo ya magari.
Amesema sehemu yenye shida inaanzia Madukani hadi Tabata Mawenzi, umbali ambao hata hauzidi kilomita moja, lakini umejaa mashimo makubwa yaliyojaa maji.
“Kuna mashimo mengi yaliyojaa maji. Daladala zinapopita zinakunywa maji na hata ukipata fedha, unalazimika kuzipeleka kwenye matengenezo ambayo yanagharimu fedha nyingi,” amesema.
Salim amesema kutokana na ukubwa wa mashimo hayo, magari hulazimika kupita ndani ya maji na kusababisha sehemu ya mbele yenye silinda kuingiza maji, hali inayowalazimu kwenda mara kwa mara kwa mafundi kwa ajili ya kunyonya maji hayo.
“Gharama ya kunyonya maji kwenye silinda za gari ni kubwa, na usipofanya hivyo vifaa vinaharibika. Unaweza kufanya safari nyingi kwenda Kimanga lakini usipate faida yoyote, badala yake ukaingia hasara kubwa,” amesema.
Amesema kipindi hiki cha mvua kimeongeza ugumu wa shughuli zao. Ingawa hawajawahi kuwasilisha rasmi malalamiko yao kwa uongozi wa halmashauri, wanashangazwa na kutokuchukuliwa kwa hatua wakati eneo la Kimanga linaonekana kuwa la hadhi ya juu.
“Kimanga ni eneo la kishua, wanaishi watu wenye heshima zao, lakini hali ya barabara wanaiona na bado mamlaka hazichukui hatua. Biashara yetu imekuwa ngumu, hivyo tunalazimika kusitisha shughuli hadi barabara itakapofanyiwa matengenezo,” amesema.
Jordan Timothy, dereva wa daladala za Kimanga-Kinyerezi, amesema barabara hiyo ni changamoto huku akisema gari yake hadi sasa imekatika spring nne.
“Tunaomba mamlaka walau zije kujaza kifusi ili kuondoa changamoto tunayopitia kwa sasa kwani magari yetu yanaharibika,” amesema.
Meneja wa Tarura Mkoa wa Dar es Salaam, Geofrey Makinga, amekiri barabara hiyo ina changamoto na mamlaka hiyo inasubiri maji yapungue ili kwenda kumwaga kifusi kama hatua ya haraka.
“Hatua ya muda mrefu, baada ya kutambua matumizi ya barabara hiyo yamekuwa makubwa tofauti na walivyokuwa wanatarajia, wameipandisha hadhi na wataijenga kwa kiwango cha zege ili iweze kuhimili shughuli zinazofanyika,” amesema.
Amesema mwanzoni ujenzi wa barabara hiyo ulizingatia magari ya kawaida na daladala, lakini wamebaini matumizi yake yameongezeka kwani magari ya mchanga ni mengi, hasa usiku, yanatumia njia hiyo kupeleka mchanga kwa shughuli za ujenzi.
“Malori ya mchanga huwezi kuyazuia. Kipande kinachosumbua ni kama mita 700, na tayari tumeshapata bajeti. Kuanzia Julai tutaijenga kwa kiwango cha zege,” amesema.