Dar es Salaam. Mara nyingine mimi huwa najiuliza mwenyewe: “Hivi ndo kweli nishazeeka?” Lakini vitabu vya kiimani vinanithibitishia kuwa mawazo huumba. Yaani unapohisi kunuka kwapa, basi ujue unanuka kweli na kila utakayepishana naye ataihisi harufu yako. Inatahadharishwa kuwa mara tu uisikiapo harufu ngeni mwilini mwako, nenda haraka ukajisafi.

Kwa nini? Ni kwa sababu bora kujihami hata kama huna uhakika. Hasara ya kujihadhari bure ni ndogo ukilinganisha na hasara itakayokupata kwa uvivu wa kutahadhari. Ukionywa hata na mtu wa hovyo, hata awe kichaa, si vibaya kuchukua tahadhari. Inawezekana kichaa akakuambia kuwa hapo ulipoketi hapafai, ukadharau kumbe ni yeye katoka kuachia kinyesi hapo.

Hali hii inafanana na jeuri ya kumkataa Mungu. Unaweza usiamini kabisa uwepo wake, lakini kiyama kitakapofika na ukakutana naye uso kwa uso, jasho la meno litakutoka. Ndio maana unaonywa kuwa baada ya vita kumalizika, usipende kuokota au kukanyaga vitu usivyovijua. Pengine kuna bomu lilishindwa kulipuka, na sasa linasubiri sababu tu ya kufanya yake.

Wanasema kunguru mwoga huepusha ubawa wake. Pia kuti la mazoea ndilo linalomwangusha mgema kila wakati. Dereva mzoefu anaweza kuondoa umakini na kuweka mazoea ya njia, akakutana na kitu kigeni kilichoingia barabarani muda huohuo. Wenyewe wanasema ukimwona bi kizee anavuka barabara usiku usimkwepe, mpelekee moto tu. Sijui… maana huko mimi simo.

Tahadhari haina gharama. Lakini ukweli ni kwamba binadamu hapendi kuambiwa ukweli. Wenyewe tunajuana ndio maana rafiki yetu akiwa mfupi sana tunamwita “Tall”, na mwembamba ataitwa “Bonge”. Hapa mtaani kuna babu hana jino hata moja, lakini wahuni wanamwita “Gen-Z”! Na mwenyewe akilisikia jina hilo anaachia mapengo yote thelathini na mawili kwa furaha!

Kwa ujumla, ukweli hata kama unauma kwa kiasi gani ni tiba. Haukatazwi kujidanganya mwenyewe ili kupunguza msongo, lakini ukweli ni tiba sahihi. Uongo unaofurahisha ni kama dawa ya usingizi: unatuliza kwa muda, lakini hauponyi tatizo. Mwenzio nilikuwa nikijidanganya kwa ‘kupiga mtungi’ ili kusahau kwamba sina hela, majibu yake niliyapata mapema asubuhi. Njaa iliuma halafu sikuwa hata na senti nyekundu!

Lakini kinyume chake, Kujenga tabia ya kupokea ukweli kunaweza kukakushawishi kuchukua hatua mapema. Unaweza ukazifanya changamoto zako kuwa fursa, na ukapata njia za kuzikabili. Njaa ni changamoto mbaya na dhalili kuliko zingine zote, lakini inafundisha namna ya kutafuta misosi. Asikwambie mtu, njaa ikiuma utakula tu, hata kwa kupekua jalalani.

Watu aliofanikiwa zaidi ni wale waliokubali ukweli na kuchukua tahadhari. Wapo waliodharau maonyo ya madaktari na kuendeleza libeneke hadi wakapotea. Lakini wapo waliokaza na kufuata maelekezo ya matabibu, wakaanza kuuelekea ujana badala ya kuishia uzeeni. Kuna swahiba wangu huwa ananishangaza sana, tulikuwa tunakesha wote lakini sasa hata mchoro wa pombe hataki kuuona!

Wapo ndugu zetu waliorithi ukwasi wa kutosha kutoka kwa wazee wao. Wakabadilisha maisha na kuiga maisha ya popo: mchana wanalala usiku ndio wanatoka. Wakaanza kukesha kwenye mitungi, kunyang’anya mabibi wa wenzao, na kufakamia minofu hata kama walikuwa wamevimbiwa. Kati yao, wapo waliozivuruga afya zao, lakini wapo pia waliofilisika kabisa. Waliukataa ukweli wa “Bandubandu humaliza gogo”.

Lakini kuna wakati tuliwaona matajiri hasa wa kiarabu. Wakati wananunua nyumba uswahilini, tulidhani nao ni makabwela kama sisi. Namkumbuka mzee mmoja anayemiliki ghorofa na malori ya mizigo, anashinda mchana kutwa kwa vikombe vya kahawa kijiweni. Jamaa yetu mmoja akamfuma akila ugali kwa kisamvu nyumbani kwake. Tangu siku hiyo alibadilishwa jina na kuitwa Al-Bahir, yaani bahili la kutupwa.

Watu walisema mengi juu yake. Mara oh mganga wake ndiye aliyemtengeneza… mara sijui nini… Lakini kumbe mzee alitambua kuwa lishe bora si makoronya. Huyu mwamba anadunda akiwa mwenye afya timamu hadi leo. Hata kama ni bahili, hayo ndiyo maisha halali aliyojichagulia mwenyewe. Nidhamu ya pesa nayo ni tahadhari tosha, au umesahau kuwa “chembe na chembe mkate huwa”.

Ukweli unaeleza kuwa binadamu wa sasa anafeli kutokana na mtindo wa maisha. Hili linajumuisha mambo mengi kama aina za chakula, kazi, starehe na kadhalika. Inaeleweka kuwa chakula ni nguzo muhimu sana katika maisha ya mwanadamu. Chakula bora ni rutuba, kinga na dawa ya mwili. Lakini chakula kisichofaa ni sumu namba moja. Inashauriwa kula chakula bora kwa kiasi ili mwili uweze kumeng’enya chakula, kusafirisha virutubisho vyake na kuondoa taka za chakula kwa umakini na bila kuchoka.

Kila kinachozidi mwilini ni sumu. Vyakula asilia vina kiasi sahihi cha virutubisho vyote vya mwili. Hivi vyakula vya kisasa vinakosa sifa hiyo kwa sababu ni lazima vikuzwe na mbolea sumu tangu vikiwa shambani. Tofauti na vile vya asilia, hivi Vinaongezewa kemikali ili visiharibike. Ndio maana hindi la kuchomwa halinogi bila ndimu na pilipili.

Tahadhari katika kila jambo unalolifanya. Ukiwa safarini, kwenye starehe, mapumzikoni, na hasa kwenye chakula. Sio lazima ule kila utakachokitamani. Hapa ndipo waswahili mnapokwama. Ukimwambia ukweli huu, mswahili atakutupia jicho la kukuzogoa “we mchawi nini? Yaani mimi niache nisijisosomole, kisa…!”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *