Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi amesema hajaridhishwa na mwenendo wa mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Megawati 49.5 katika maporomoko ya maji ya mto Malagarasi kutokana na kuchelewa kwa utekelezaji wa kazi pamoja na kushindwa kuendana na masharti ya mkataba kwani amekuwa akitoa visingizio badala ya kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mkataba.
Ndejembi amebainisha hayo Mei 10, 2026 wakati wa ziara yake ya kukagua mradi wa kuzalisha umeme megawati 49.5 katika maporomoko ya mto Malagarasi mkoani Kigoma.
Amesema Serikali imeshamlipa mkandarasi huyo zaidi ya dola milioni 20 kama malipo ya awali lakini kiwango cha kazi iliyofanyika hakiendani na fedha zilizotolewa; Mkandarasi alitakiwa kujenga eneo la makazi ya wafanyakazi pamoja na barabara za mradi lakini hadi sasa hajatekeleza majukumu hayo, jambo linaloashiria uzembe katika utekelezaji wa mradi huo muhimu wa kimkakati.
Aidha, amesema Serikali haitatoa nyongeza ya fedha wala kuruhusu mabadiliko ya gharama za mradi kwani mkandarasi aliwasilisha gharama zake hapo awali; Baadhi ya wakandarasi wamekuwa na tabia ya kuomba kazi kwa gharama ndogo ili wapate zabuni na baadaye kuanza kuomba nyongeza ya fedha, jambo ambalo halitakubalika katika utekelezaji wa mradi huo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Ndejembi ameagiza meneja wa mradi huo kuondolewa mara moja kwa kuwa sehemu ya vikwazo vinavyochelewesha utekelezaji wa kazi huku akiagiza kufanyika kwa ukaguzi maalum wa matumizi ya fedha za malipo ya awali zilizotolewa kwa mkandarasi ili kubaini fedha hizo zimefanya kazi gani na kama hazijaelekezwa katika miradi mingine.
(Feed generated with FetchRSS)