DODOMA: Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, amezindua rasmi Mwongozo wa Kuratibu Ushiriki wa Wadau wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum katika Mikutano ya Kikanda na Kimataifa wa mwaka 2024, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na tija ya ushiriki wa Tanzania katika majukwaa ya kimataifa.

‎Akizungumza jijini Dodoma katika kikao cha wadau walioshiriki Mkutano wa 70 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake Duniani (CSW70), Dk. Gwajima alisema mwongozo huo umeandaliwa mahsusi ili kuimarisha usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya ushiriki wa Serikali pamoja na wadau mbalimbali katika mikutano ya nje ya nchi.



‎Amesema utekelezaji wa mwongozo huo utawezesha Serikali kuwa na mfumo madhubuti wa kufuatilia mikutano inayowahusisha wadau wa maendeleo ya jamii, jinsia na wanawake, sambamba na kutathmini manufaa yanayopatikana kwa taifa kupitia ushiriki huo.

‎“Lengo letu ni kuhakikisha kila ushiriki wa Tanzania katika mikutano ya kikanda na kimataifa unaleta matokeo yenye manufaa kwa wananchi na taifa kwa ujumla,” amesema Dk. Gwajima.

‎Ameongeza kuwa mwongozo huo pia utaimarisha uwajibikaji na ushirikishwaji kwa kuweka utaratibu unaoeleweka kuanzia hatua za maandalizi, ushiriki hadi tathmini baada ya mikutano.



‎Aidha, amewataka viongozi wa Wizara kuhakikisha wadau wanashirikishwa tangu hatua za awali za maandalizi ya mikutano hiyo, ikiwemo katika uteuzi wa viongozi, wajumbe na kamati ndogondogo zitakazosimamia ushiriki wa Tanzania katika majukwaa ya kikanda na kimataifa.

‎Dk. Gwajima amesema ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wadau utasaidia kuimarisha uwakilishi wa Tanzania na kuhakikisha sauti ya nchi inasikika kwa ufanisi zaidi katika ajenda za maendeleo ya wanawake, jinsia na makundi maalum duniani.



‎Ameeleza kuwa Tanzania inahitaji ushiriki wenye tija zaidi katika mikutano ya kikanda na kimataifa ili kuhakikisha masuala ya wanawake, jinsia na makundi maalum yanazalisha matokeo chanya kwa taifa.

‎Pia amesisitiza kuwa mafanikio ya ushiriki wa kimataifa yanategemea maandalizi madhubuti yanayojumuisha uandaaji wa ripoti za nchi, upatikanaji wa rasilimali fedha na ushirikishwaji wa makundi mbalimbali ya kijamii yakiwemo wanawake, vijana, wanaume, wazee, wajane pamoja na viongozi wa sasa na waliostaafu.

‎“Tunatakiwa kujipanga kama timu moja kuhakikisha ushiriki wetu unaendana na kaulimbiu za mikutano husika na kuleta manufaa halisi kwa nchi,” amesema Dk. Gwajima.

‎Kikao hicho kimewakutanisha viongozi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, mashirika yasiyo ya kiserikali, wahandisi wanawake, majaji pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ya jinsia na wanawake nchini, kwa lengo la kutathmini mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika Mkutano wa CSW70 uliofanyika jijini New York, Marekani mwezi Machi mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *