IRINGA: Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapunduzi (CCM), Kenani Kihongosi amewataka wananchi wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa kuendelea kushirikiana na kuwaunga mkono viongozi wao ili kuharakisha maendeleo ya eneo hilo.

Kihongosi amesema hayo leo Juni 18,2026 aliposhiriki kikao cha shina namba 10 Kata ya Ruaha Mbuyuni, Kilolo mkoani Iringa.

Kihongosi amesema maendeleo yanayoonekana katika wilaya hiyo ni matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya CCM na ushirikiano kati ya wananchi na viongozi wao.

“Shikamaneni na chama chenu, unganeni na viongozi wenu, madiwani wenu, wabunge wenu, viongozi wa serikali, viongozi wa chama ili hapa Kilolo pawe ni habu ya maendeleo,” amesema Kihongosi.

Ameeleza kuwa wananchi wanaweza kushuhudia mabadiliko makubwa yaliyofanyika katika miaka ya hivi karibuni, ikiwemo upatikanaji wa umeme vijijini pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Pia amewapongeza viongozi wa CCM Mkoa wa Iringa na Wilaya ya Kilolo kwa kuendelea kuimarisha chama na kusimamia maendeleo ya wananchi.

Kihongosi ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya chama wilayani Kilolo, ambapo alikutana na wanachama na viongozi wa CCM pamoja na kukagua utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *