
Kwa mujibu wa taarifailiyotolewa na Ofisi yake hii leo mjini Geneva, Uswisi, Türk amebainisha kuwa timu ya ofisi hiyo nchini Sudan imegundua kuwa kati ya mwezi Januari na Aprili mwaka huu mashambulizi ya droni yamesababisha vifo vya raia wasiopungua 880 ikiwa ni zaidi ya asilimia 80 ya vifo vyote vya raia vinavyohusiana na mzozo huo.
“Ndege zisizo na rubani sasa zimekuwa sababu kuu ya vifo vya raia kwa kiasi kikubwa,” amesema Türk akiongeza kuwa, “kuongezeka kwa matumizi ya ndege hizi zisizo na rubani kunafanya vita hivi kuendelea kwa kasi hasa katika msimu wa mvua unaokuja, wakati ambao huko nyuma mapigano ya ardhini yalikuwa yanatulia. Mapigano haya yakiongezeka katika wiki zijazo huku kila upande ukijaribu kupata au kulinda maeneo unayotawala, kuna hatari kubwa ya vita kusambaa hadi majimbo ya kati na mashariki mwa nchi, jambo ambalo litaleta maafa makubwa ya vifo kwa raia katika maeneo mengi zaidi.”
Amesema, “hili halipaswi kuruhusiwa kutokea. Jumuiya ya kimataifa iko macho, isipokuwa hatua zichukuliwe bila kuchelewa, mzozo huu uko kwenye ukingo wa kuingia katika awamu nyingine mpya, yenye hatari zaidi.”
Mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu
Mkuu huyo wa Haki za Binadamu, amebainisha miongoni mwa mifano ya hivi karibuni ya mashambulizi, ni yale yaliyotokea tarehe 8 Mei huko Al Quz jimboni Kordofan Kusini, na karibu na El Obeid jimboni Kordofan Kaskazini, ambako raia 26 waliripotiwa kuuawa. Türk ametoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua madhubuti kuzuia uhamishaji wa silaha, zikiwemo droni za kisasa, kwenda kwa pande zinazopigana.
“Mashambulizi ya ndege hizi dhidi ya raia na mali zao yatazidi kuwa mabaya kama hakuna hatua zozote za kisheria zitakazochukuliwa, kwani kwa sasa pande zote mbili zimeanza kuzoea kutumia ukatili huu kama njia ya kawaida ya kupigana,” amesema Türk.
Pande hizo mbili, ambazo ni Jeshi la serikali ya Sudan (SAF) na upande wa upinzani Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), zimetumia droni kushambulia masoko kwa takribani mara 28 na vituo vya afya mara 12 katika kipindi cha miezi minne, jambo ambalo limesababisha baadhi ya vituo kufungwa na kuwalazimu raia kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu.
Aidha, mashambulizi hayo sasa yanasambaa nje ya Kordofan na Darfur, yakigusa maeneo ya Blue Nile, White Nile, na Khartoum, ambapo shambulio la tarehe 4 Mei kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum lilisababisha kusitishwa kwa safari zote za ndege.
Hofu ya njaa na usalama wa raia
Kamishna Mkuu ameonya kuwa kuongezeka kwa ukatili huo pia kutavuruga usambazaji wa misaada muhimu ya kibinadamu nchini humo. “Sehemu kubwa ya nchi, ikiwa ni pamoja na Kordofan, sasa inakabiliwa na ongezeko la hatari ya njaa na ukosefu mkubwa wa uhakika wa chakula, hali inayochochewa na ucheleweshaji unaotarajiwa au uhaba wa mbolea kutokana na mzozo wa Ghuba,” amesema Türk.
“Natoa wito kwa mara nyingine tena kwa pande zote kuhakikisha ulinzi wa raia, ikiwa ni pamoja na harakati salama katika maeneo yenye uhasama,” amesema Kamishna Mkuu. Ameongeza kuwa pande zinazopingana lazima ziwezeshe harakati salama za raia na kuwalinda dhidi ya vitendo vya kulipiza kisasi, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kiholela, ukatili wa kijinsia, ukamataji wa kiholela, na utekaji nyara.