Dar es Salaam. Baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam bado wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama huku wakilazimika kuvuna maji ya mvua kwa matumizi.

Hata hivyo, tangazo lilitolewa Mei 9, 2026, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) la ukosefu wa huduma ya maji kwa wastani wa saa 10, kuanzia Mei 10, 2026, lililalamikiwa na wananchi wakidai upungufu wa maji upo kwa muda mrefu huku wengine wakisema zaidi ya mwezi mmoja hawajaona maji ya bomba.

Mamlaka hiyo ilisema matengenezo yatakayofanyika yatawaathiri wananchi wanaohudumiwa kupitia mitambo ya Ruvu Chini Wilaya ya Bagamoyo na Ruvu Juu Wilayani Kibaha.

Hatua hiyo ililenga kuruhusu matengenezo ya miundombinu ya umeme katika kituo cha kupooza umeme cha Mlandizi ili kusaidia kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa muda mrefu.

Katika mitaa ya Sinza, Tabata, Kinondoni, Gongo la Mboto, Magomeni na Kariakoo, wananchi wanasema wamekuwa wakitegemea maji ya kununua kutoka kwa wauzaji binafsi au kuhifadhi maji ya mvua kwa matumizi ya nyumbani.

Mkazi wa Sinza Bamaga, Issa Abbas amesema mara nyingi hulazimika kutumia fedha nyingi kila wiki kununua maji kwa sababu maji kwake yanatoka mara moja au mbili kwa mwezi.
“Hata mvua zinaponyesha, hatuna vyombo na mifumo ya kuhifadhia maji ambayo yanaweza kutusaidia kupunguza kero hii kwa muda mrefu,”amesema Abbas.

Mkazi wa Tabata Shiba, Rehema Kondo amesema maji ya bomba hutoka kwa nadra na kwa kipindi hiki wanategemea zaidi kuvuna maji ya mvua.

“Nakaa hadi mwezi sijaona maji ya bomba lakini utasikia watu wa bondeni maji kwao yametoka jambo linalotupa wakati mgumu kuendelea kununua maji ya chumvi pamoja na kuhifadhi ya mvua,” amesema Rehema.

Mkazi wa Gongo la Mboto, Salehe Mshindo amesema wameamua kuagiza maji ya magari ambayo wanachanga kwenye nyumba moja na kulipia Sh20,000 kwa boza.

“Siku maji yakitoka ni usiku tunajikuta tunakesha na familia zetu kufuatilia maji ili kujaza kwenye vyombo tulivyonavyo na kipindi hiki cha mvua kidogo imetusaidia,”amesema.

Mkazi wa Magomeni Mikumi Kuluthum Ally amesema amejikuta akipokea malalamiko kutoka kwa wapangaji wake kuhusu upatikanaji wa maji.

“Nina wapangaji maeneo mawili Magomeni Mikumi na Mapipa, Mtaa wa Uweje maji hakuna wapangaji wanalalamika mpaka najisikia vibaya wananipa ushauri nichimbe kisima ili kuwaondolea shida hii,” amesema Kuluthum.

Akizungumza jana na Mwananchi, daktari bingwa kutoka Idara ya Mafunzo na utafiti wa magonjwa ya ndani Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya, Ernest Winchislaus amesema matumizi ya maji ya mvua bila kuyatibu yanaweza kusababisha magonjwa mbalimbali hatari kwa binadamu.

Amesema ili maji ya mvua yawe salama kwa matumizi ya binadamu, ni muhimu kuhakikisha paa na mabomba ya kupitisha maji yanasafishwa mara kwa mara ili kuondoa vumbi, majani, kinyesi cha ndege pamoja na uchafu mwingine unaoweza kuchafua maji hayo.

Dk Winchislaus amesema watumiaji wanatakiwa kuyaacha maji ya mwanzo ya mvua yapotee kabla ya kuanza kuyakusanya, kwa kuwa maji hayo mara nyingi hubeba uchafu uliokusanyika kwenye mabati na mifereji wakati wa ukame.

“Maji ya mvua yanaweza kuwa salama endapo yatakusanywa na kuhifadhiwa vizuri. Tatizo kubwa ni watu kuyatumia moja kwa moja bila kuyatibu,” amesema Dk Winchislaus.

Amesema matumizi ya maji yasiyotibiwa yanaweza kusababisha madhara mbalimbali kiafya ikiwamo kuhara, kipindupindu, homa ya matumbo, maambukizi ya tumbo pamoja na magonjwa ya ngozi.

“Wananchi wanapaswa kuwa makini kwa sababu maji yanaweza kuonekana safi kwa macho lakini yakawa na vijidudu hatari visivyoonekana,” amesema.

Pia, ameonya matumizi ya mabati ya zamani yenye kutu au yale yenye kemikali hatari katika uvunaji wa maji ya mvua, akieleza kuwa hali hiyo inaweza kusababisha kuingia kwa metali hatari ndani ya maji na kuathiri afya za watumiaji.

Hivi karibuni, akizungumza na Mwananchi Ofisa Mtendaji Mkuu Dawasa, Mkama Bwire alisema changamoto hiyo kwa kiasi kikubwa imetokana na udhaifu wa miundombinu.
Alisema upatikanaji wa maji si suala la chanzo pekee, bali ni mnyororo wa hatua nyingi kuanzia uzalishaji hadi usambazaji.

“Watu wengi wanaweza kuona maji yapo, lakini kuyafikisha kwa mteja ni mchakato wenye hatua nyingi. Kuna uzalishaji, kuna usafirishaji kupitia mabomba na kuna miundombinu ambayo wakati mwingine imechoka,” alisema.

Alisema uzalishaji wa maji kwa sasa unategemea uwezo wa mitambo pamoja na rasilimali zilizopo, hali inayosababisha baadhi ya maeneo kupata huduma kwa kiwango tofauti na mengine.

Katika maeneo kama Magomeni, Bwire alitaja kuwa baadhi ya mabomba ni ya muda mrefu na mengine yameziba kabisa, jambo linalosababisha maji kushindwa kuwafikia wananchi licha ya kuwepo kwa huduma hiyo.

“Unaweza kukuta eneo lina huduma ya maji, lakini hayafiki kwa sababu ya bomba lililoziba au miundombinu ya zamani. Sio kwamba huduma haipo, bali kuna hitilafu katika njia ya kuyafikisha na tumekuwa tukisafisha baadhi ya maeneo kuondoa tope na maji yameendelea kupita vizuri,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, amewasihi wananchi kushirikiana kwa karibu na mamlaka hiyo kwa kutoa taarifa za changamoto wanazokutana nazo ili ziweze kushughulikiwa kwa wakati.

Alisema si rahisi kwa Dawasa kufika kila eneo bila kupata taarifa kutoka kwa wananchi, hivyo mawasiliano ni muhimu katika kubaini na kutatua matatizo.

“Tunawahimiza wananchi wanapotambua changamoto kwenye maeneo yao watupatie taarifa mapema.Timu zetu zitafika kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki,” alisema.

Aidha, alisema mamlaka hiyo imeweka utaratibu rasmi wa kupokea malalamiko kupitia namba maalumu ya huduma kwa wateja ya 181, mwananchi anapaswa kupiga simu ili kupata namba ya kumbukumbu ya malalamiko yake.

Alisema mfumo huo unasaidia kufuatilia kwa urahisi tatizo lililoripotiwa na kuepusha upotoshaji unaoweza kujitokeza pale mtu anapodai kuwasiliana na Dawasa bila ushahidi wa kumbukumbu.

“Ni muhimu mwananchi akapiga namba ya huduma na kupata namba ya malalamiko. Hii inatusaidia sisi kujua tatizo liko wapi na nani ameliripoti ili hatua zichukuliwe kwa haraka.”

Changamoto hii pia ilibainishwa kupitia ripoti mpya ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), inayoonesha kati ya malalamiko 463,740 yaliyowasilishwa, asilimia 58.6 yanatokana na mivujo na presha hafifu ya maji.

Malalamiko hayo yapo kwenye Ripoti ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa mwaka wa fedha 2024/25 iliyozinduliwa Machi 19, 2026 mkoani Morogoro na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere juzi alipokuwa akiwasilisha ripoti yake ya ukaguzi kwa Rais Samia Suluhu Hassan ya mwaka 2024/25, alisema upotevu wa maji umeendelea kuisababishia Serikali hasara.

Alisema kwa mwaka 2024/25 upotevu wa maji umeongezeka kufikia asilimia 35 kutoka asilimia 32.

Kiwango hicho kipo juu ya lengo la kitaifa la kutozidi asilimia 20 hali iliyosababisha hasara ya Sh248.78 bilioni huku baadhi ya mamlaka zikiwa na kiwango kikubwa cha upotevu wa maji.

“Same-Mwanga anazalisha asilimia 100 ya maji asilimia 70 yanapotea, Dar es Salaam asilimia 53 ya maji yanayozalisha yanapotea, Morogoro asilimia 50 yanapotea kwa maana hiyo asilimia kubwa hayafikii wananchi au yanayowafikia hayatozwi,” alisema CAG Kichere.

Alisema chanzo kikubwa cha tatizo ni miundombinu chakavu na wizi wa maji, hali inayoathiri uendelevu wa mapato mamlaka za maji na kupunguza upatikanaji wa huduma na kutegemea ruzuku serikalini.

“Napendekeza Serikali iimarishe uwekezaji katika ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya maji, mifumo ya upotevu wa maji na kuchukua hatua ya miunganisho haramu, kupunguza hasara na kuongeza ufanisi wa sekta,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *