
Wafanyakazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Dunia tayari wako hapa kuipokea meli ya kitalii ya MV Hondius ambayo baadhi ya abiria wake waligundulika kuathiriwa na ugonjwa wa Virusi vya Hanta au Hantavirus, wengine wakapoteza Maisha, wengine wakalazimika kupewa matibabu ya haraka na waliosalia wakakwama ndani ya meli baharini karibu na nchi ya Cape Verde na sasa meli imesogea Hispania ili abiria waliokwamia ndani kwa siku kadhaa wafanyiwe uchunguzi zaidi na watakaonekana hawana maambukizi waruhusiwe kuondoka.
Dkt. Boris Pavlin kutoka WHO ambaye ni Mtaalamu wa Epidemiolojia ya Tiba yaani uchunguzi wa magonjwa anasema,
“Tumekuwa tukiwasiliana na wataalamu wa epidemiolojia walioko ndani ya meli hiyo ambao wamekuwa wakiwachunguza abiria na wafanyakazi ili kuhakikisha kuwa hakuna mwenye dalili zozote, na pia kujaribu kuelewa kiwango cha hatari na ukaribu wa watu hao kwa wale waliokuwa wagonjwa.”
Mwingine aliyeko hapa kutoka WHO ni Dkt. Ana Paula Coutinho Rehse, Afisa wa Kuzuia na Kudhibiti Maambukizi anasema:
“Jukumu langu kimsingi ni kuhakikisha pia kwamba taarifa tunazopata kutoka kwa wataalamu wa epidemiolojia zinawekwa katika muktadha wa namna tunavyoweza kutumia hatua za kinga na udhibiti, ili watu waweze kushuka kutoka melini, kupanda ndege, na tunatumaini hivi karibuni warejee katika maisha yao ya kawaida.”
Picha zilizopigwa kwa droni zinaonesha baadhi ya abiria wakitoka katika meli na kupanda katika boti ndogo ya wazi na mmoja wa wanaoshuhudia ni Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus aliyesafiri hadi huko Hispania kuhakikisha tukio hili linafanikiwa.