Songwe. Ubadhirifu wa Sh510,000 unatishia kuweka rehani kibarua cha Kaimu Mtendaji wa Kata ya Idiwili iliyopo Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Nerbati Nzowa.

Nzowa amesimamishwa kazi na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabir Makame, baada ya ubadhirifu huo. Pia, amekabidhiwa kwa Taasisi ya Kuzuia, Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Tuhuma za Nzowa zinatokana na kulalamikiwa na mmoja wa wananchi, wakati wa mkutano wa hadhara wa mkuu huyo wa mkoa kijijini Idiwili.

Kwa mujibu wa mwananchi huyo, Mkondwa Mnkondwa, fedha hizo zilitengwa kwa ajili ya maendeleo, lakini kaimu mtendaji huyo akazibadili na kudai hazikuwa za kijiji.

Makame ametoa uamuzi huo leo, Jumanne Mei 12, 2026 wakati wa mkutano wake wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika Kijiji cha Idiwili.

Katika maelezo yake mbele ya Makame, Mkondya amesema fedha hizo Sh510,000 zilitolewa na mwekezaji kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya kijiji, lakini zilibadilishwa matumizi.

Ameeleza mwekezaji huyo wa ujenzi wa kituo cha mafuta alitoa fedha hiyo ikiwa ni utekelezaji wa utaratibu wa kawaida wa kijiji kumtaka kila mwekezaji kuchangia maendeleo.

Malalamiko mengine yalitolewa na mwanakijiji mwingine, Siliasi Mwalyemo, aliyesema mtendaji huyo alichangisha Sh4.5 milioni kwa ajili ya ujenzi wa Sekondari ya Ilomba lakini zilizotumika ni Sh500,000 pekee.

Amesema fedha alizikusanya kwa wananchi usiku na ulipofika wakati wa kuhoji matumizi yake hakuwahi kuwa na majibu ya kueleweka.

Alichojibu mtuhumiwa

Alipopewa nafasi ya kujibu tuhuma hizo, Nzowa amesema hajawahi kupokea fedha kutoka kwa mwekezaji kwa ajili ya maendeleo, bali alifanya naye kazi kama dalali wa viwanja.

“Nilikuwa nafanya biashara ya udalali na mwekezaji na aliniambia nikimtafutia kiwanja atanipatia Sh500,000 na alitimiza ahadi yake kama alivyoniahidi,” amesema.

Kauli ya RC

Baada ya kusikiliza pande zote, Makame amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbozi, Abdallah Nandonde, kumsimamisha kazi mtendaji huyo kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.

“Kutokana na tuhuma zilizotolewa dhidi ya mtendaji huyo, niagize Takukuru kuanza mara moja uchunguzi wa tuhuma hizo. Viongozi wa wilaya na vyombo vya dola mfuatilie kwa karibu suala hilo ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Makame amewataka viongozi wa halmashauri na watendaji wa Serikali mkoani Songwe kusimamia kwa karibu nidhamu ya watumishi na kuhakikisha wananchi wanapata haki na huduma bora bila manyanyaso wala ukiukwaji wa sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *