Arusha. Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imetupilia mbali ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) la kutaifisha mali zinazodaiwa kumilikiwa na Samwel Emmanuel, aliyehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya.

DPP aliiomba Mahakama kutaifisha vipande kadhaa vya ardhi vinavyodaiwa kumilikiwa na Samwel ikiwemo eneo ambalo anadaiwa kununua kwa Sh200,000 katika Kijiji cha Shungubweni, Mkuranga mkoani Pwani.

Nyingine ni eneo ambalo halijapimwa analodaiwa kununua Sh400,000 lenye ukubwa wa mita za mraba 89, pamoja na lingine lenye thamani ya Sh437,000 na ukubwa wa mita za mraba 339.

DPP pia alitaka kutaifishwa kipande kingine kilichonunuliwa kwa Sh400,000 chenye ukubwa wa mita za mraba 310, sambamba na vipande vingine viwili vilivyonunuliwa kwa Sh300,000 kila kimoja.

Aidha aliiomba mahakama kutoa amri nyingine yoyote ambayo inaona inafaa, ambapo kupitia hati ya kiapo ya maombi hayo ilidaiwa mali zote hizo zilinunuliwa kwa fedha zinazotokana na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Uamuzi huo umetolewa jana Mei 11, 2026 na Jaji Sedekia Kisanya, aliyekuwa akisikiliza maombi hayo ya uhujumu uchumi namba 26918/2025 yaliyokuwa yamewasilishwa na DPP dhidi ya Samwel, na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.

Jaji Kisanya amesema pamoja na kuwepo kwa sheria kali zinazolenga kupambana na mapato ya uhalifu nchini, bado mahakama haiwezi kutoa amri ya kutaifisha mali bila ushahidi wa kuaminika na usio na mashaka makubwa ya kisheria.

Katika maombi hayo, Serikali kupitia DPP iliwasilisha maombi hayo chini ya Sheria ya Mapato yatokanayo na Uhalifu (Poca), ikidai kuwa mali kadhaa za ardhi zilizopo katika Kijiji cha Shungubweni, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, zilinunuliwa kwa fedha zilizotokana na biashara ya dawa za kulevya.

Katika maombi hayo, Serikali ilitaka vipande hivyo vya ardhi visivyopimwa pamoja na mali nyingine zinazodaiwa kumilikiwa na Samwel vitaifishwe na kuwa mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa Samwel alipatikana na hatia katika kesi ya uhujumu uchumi namba 24327/2024 na kuhukumiwa adhabu hiyo Desemba 13, 2024.

Kufuatia hukumu hiyo, DPP aliwasilisha ombi la kutaifisha mali hizo Novemba 10, 2025 akidai kuwa zilikuwa zimepatikana kwa mapato ya uhalifu.

Katika hoja zake, Serikali ilisema uchunguzi uliofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ulibaini kuwa Samwel alikuwa akifanya kazi kwa karibu na mfanyabiashara anayedaiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, Salehe Baselman.

Ulidai kuwa Samwel hakuwa na chanzo halali au biashara yenye uwezo wa kuzalisha fedha za kutosha kupata mali hizo zisizohamishika.

Kupitia hati ya kiapo upande wa mashtaka ulidai kuwa Samwel alikiri katika maelezo yake kuwa alikuwa akipokea dawa za kulevya kutoka kwa Basleman kwa ajili ya kuzihifadhi, kuzisambaza na kuziuza.

Aidha, Serikali ilitegemea kifungu cha 53(4) cha Sheria ya DCEA, ambacho kinaweka dhana kwamba mali yoyote iliyopatikana ndani ya miaka kumi kabla ya mtu kukamatwa kwa kosa la biashara ya dawa za kulevya inaweza kudhaniwa kuwa ni mali iliyochafuliwa isipokuwa ithibitishwe vinginevyo.

Hata hivyo, upande wa mjibu maombi hayo, ulipinga vikali madai hayo na kueleza kuwa mali hizo zilinunuliwa kwa fedha halali zilizotokana na shughuli mbalimbali za kibiashara na ufugaji.

Walidai kuwa Samwel alikuwa akijihusisha na shughuli za ufugaji wa ng’ombe huko Bukoba pamoja na kazi za usimamizi wa shughuli za kilimo na mifugo ambazo zilimpatia kipato halali.

Pia ilielezwa kuwa baadhi ya mali hizo zilinunuliwa kwa ushirikiano na mke wake ambaye ni mfanyabiashara na mwenye uwezo wa kifedha wa kusaidia ununuzi wa ardhi hizo.

Wakili wake alihoji pia uhalali wa ushahidi uliowasilishwa na Serikali akisema baadhi ya madai yaliyomo kwenye hati ya kiapo ya mpelelezi hayakuungwa mkono na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani.

Uamuzi wa Mahakama

Katika uamuzi wake, Jaji amesema suala kuu ni iwapo mwombaji ametimiza wajibu unaohitajika wa kuthibitisha uwiano na uwezekano wa kwamba maeneo hayo wanayotaka yataifishwe ni mali iliyochafuliwa kwa mujibu wa sheria.

Jaji huyo amesema sheria inatambua kuwa mali iliyochafuliwa ni pamoja na mapato yoyote yanayotokana moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja na uhalifu mkubwa kama biashara ya dawa za kulevya.

Hata hivyo, amesema ili mahakama iamuru mali itaifishwe lazima kuwepo ushahidi wa kuaminika unaoonyesha uhusiano wa moja kwa moja kati ya mali husika na mapato ya uhalifu.

Mahakama ilieleza kuwa baada ya kuchambua taarifa za onyo zilizowasilishwa kama vielelezo, ilibaini kuwa hazikuwa na maelezo yanayofanana na madai yaliyotolewa kwenye hati ya kiapo ya mpelelezi.

Kwa mujibu wa Jaji Kisanya, katika moja ya aya za hati ya kiapo, mpelelezi alidai kuwa Samwel alikiri kupokea heroini kutoka kwa Salehe Basleman kwa ajili ya kuhifadhi na kuuza.

Lakini baada ya mahakama kupitia maelezo ya onyo yaliyowasilishwa kama kielelezo, ilibaini kuwa Samwel hakukiri jambo hilo bali alieleza kuwa uhusiano wake na Basleman ulihusu kusaidia kupata viwanja na kusimamia ujenzi wa nyumba.

Mahakama pia ilibaini kuwa katika maelezo mengine, Samwel amesema wazi kuwa hakuwa akijua kama Salehe Basleman alikuwa anajihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Kutokana na tofauti hiyo, Jaji Kisanya amesema hati ya kiapo ya Serikali ilikuwa imejaa taarifa zisizoendana na ushahidi wa msingi uliowasilishwa mahakamani.

Akirejea maamuzi mbalimbali ya Mahakama ya Rufani kuhusu matumizi ya hati za kiapo zenye taarifa za uongo au upotoshaji, Jaji Kisanya amesema mahakama haiwezi kutegemea ushahidi wa namna hiyo katika kutoa maamuzi muhimu kama ya kutaifisha mali za mtu.

Mahakama ilisema kuwa kiapo kilichojaa taarifa zisizo sahihi hupoteza uaminifu wake na hakiwezi kuwa msingi salama wa kuamua haki za watu.

Kwa msingi huo, mahakama iliona kuwa hata dhana ya kisheria inayoruhusu mali kudhaniwa kuwa imepatikana kwa mapato ya dawa za kulevya ndani ya miaka 10 kabla ya kukamatwa kwa mtuhumiwa haiwezi kutumika bila uwepo wa ushahidi wa kuaminika.

Kutokana na sababu hizo, Jaji Kisanya alitupilia mbali maombi yote ya Serikali ya kutaka mali hizo zitaifishwe.

Aidha, katika uamuzi wake, Mahakama ilisisitiza kuwa pamoja na sheria za Tanzania kutoa mamlaka kwa Serikali kutaifisha mali zinazotokana na uhalifu, bado hatua hiyo haiwezi kufanyika kwa maelezo ya jumla au tuhuma zisizo na uthibitisho wa kutosha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *