Nyota wa Singida Black Stars, Mossi Nduwumwe ambaye ni raia wa Burundi, ameendelea kuwa moto wa kuotea mbali baada ya kupachika bao katika mchezo wa tatu mfululizo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo kwenye Uwanja wa Airtel, Singida, huku TRA ikiendelea kuzigomea timu za Dar.

Bao hilo ambalo alifunga katika dakika ya 68 kufuatia asisti ya Cirille Ande limeifanya Singida BS kupata ushindi wa bao 1-0 na kufikisha pointi 38 ikiwa nafasi ya nne, imeachwa na Azam ambayo ipo nafasi ya tatu kwa pointi tano na mchezo mmoja mkononi.

Nduwumwe ambaye ni kiungo mshambuliaji, alifunga mabao mawili Mei 5 wakati Singida BS ikiibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Pamba Jiji, akacheka tena na nyavu mara mbili wakati walima alizeti hao wakiishindilia Mtibwa Sugar mabao 4-0 kabla ya mechi ya jana kufunga bao moja.

Hivyo Mrundi huyo amepachika mabao matano katika mechi hizo ambazo zote Singida BS imecheza nyumbani, kiujumla msimu huu wa Ligi Kuu Bara, nyota huyo amefunga jumla ya mabao manane na ndiye kinara wa mabao wa timu hiyo.

Mrundi huyo kwa sasa ameingia anga za Clatous Chama wa Simba ambaye naye amefanya makubwa katika mechi tatu mfululizo.

Chama alifunga bao moja wakati Simba ikitoa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Yanga, akafunga bao moja ambalo liliifanya timu hiyo kuvuna pointi tatu muhimu dhidi ya maafande wa JKT Tanzania huku akifunga na kutoa asisti katika mchezo wa mwisho dhidi ya Tanzania Prisons ambapo waliwanyuka mvua ya mabao 4-0.

Nyota wa Yanga,Allan Okello leo naye atakuwa katika nafasi ya kutesa kama ilivyokuwa kwa Chama na Nduwumwe kama atatupia dhidi ya Dodoma Jiji kufuatia kufunga katika mechi mbili zilizopita.

Mechi nyingine ambayo ilichezwa jana, Jumanne ilishuhudiwa TRA United ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya JKT Tanzania.

Hii ina maana kuwa sasa hakuna timu yoyote kutoka Dar es Salaam ambayo imefanikiwa kuibuka na pointi tatu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha ilipokwenda kuvaana na TRA na hakuna timu iliyomaliza kwenye nne bora msimu uliopita iliyopata pointi tatu kwenye uwanja huo.

Simba na Yanga zilitoka sare huku Azam na Singida BS zikiambulia vichapo kwenye uwanja huo.

TRA ndiyo ilikuwa ya kwanza kujipatia bao kupita kwa Joseph Akandwanaho katika dakika 20, huku JKT ikisawazisha kupitia kwa Salum Hamis dakika ya 30 ya mchezo.

 Matokeo hayo yamewafanya wakusanya TRAkufikisha pointi 34 wakiwa nafasi ya sita pointi mbili nyuma ya JKT.

Mshambuliaji wa  TRA Ramadhani Chobwedo aliendelea kuonyesha makali yake kwenye mechi hii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *