Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakitoa mitazamo tofauti kuhusu mustakabali wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kufuatia kusitishwa kwa shughuli zake za kisiasa kutokana na zuio la mahakama, hali imeonekana kubadilika baada ya chama hicho kurejea rasmi katika majukwaa ya kisiasa nchini wiki iliyopita.

Licha ya viongozi wake kukaa kizuizini kwa muda mrefu, mikutano ya kisiasa iliyofanyika Arusha, Bunda na Mbeya, kila mmoja ukidumu kwa wastani wa saa 12, imeonyesha kurejea kwa nguvu ya chama hicho na kuibua mjadala mpya kuhusu ushawishi wake ndani na nje ya wafuasi wake.

Mbali na wanachama na wafuasi wa Chadema, baadhi ya wanasiasa na makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wametoa kauli hadharani zinazoashiria kupongeza kurejea kwa shughuli za chama hicho, wakikieleza kuwa ni sehemu muhimu ya ushindani wa kisiasa na demokrasia nchini.

Aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo, baada ya mkutano mkubwa uliofanyika jijini Arusha Mei 10, 2026, aliandika katika ukurasa wake wa Instagram kuwa yaliyoshuhudiwa katika mkutano huo yalionyesha kurejea kwa demokrasia nchini.

“Leo nimefurahi kuona ukurasa wa demokrasia umefunguliwa tena Arusha,” aliandika.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chiponda maarufu Baba Levo, akizungumza katika kipindi cha Medani Kuu kinachoendeshwa na Chief Odema kupitia Star TV, alisema Chadema bado ni chama kikubwa cha upinzani nchini.

“Mimi nakiheshimu sana chama cha Chadema, kimeleta upinzani nchini kwa muda mrefu. Napenda kukosolewa na nilijisikia vibaya walivyofungiwa kushiriki uchaguzi,” alisema.

Wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mei 8, 2026 kwenye eneo la Soko la Kuu jijini Arusha. Picha na Filbert Rweyemamu

Chanzo cha migawanyiko na hofu ya kuporomoka

Katika kipindi cha kusitishwa kwa shughuli zake, siasa za upinzani zilionekana kupoteza ushindani uliokuwa umezoeleka miaka ya nyuma. Baadhi ya viongozi wa Chadema walihama na kujiunga na vyama vingine, huku wengine wakihusika katika juhudi za kukijenga upya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), hali iliyozidisha tafsiri kuwa upinzani ulikuwa ukigawanyika zaidi.

Wakati huo huo, misukosuko ya kisiasa iliyomkumba Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu aliyekamatwa na kuendelea kushikiliwa gerezani kutokana na shauri linaloendelea mahakamani, ilizua mjadala kuhusu uwezo wa chama hicho kuendelea kuwa nguvu ya kitaifa.

Kwa baadhi ya wananchi, mazingira hayo yalionekana kuwa mwanzo wa kudhoofika kwa chama hicho, hasa kutokana na kupungua kwa shughuli zake za hadhara.

Pia, kulikuwa na mjadala mkubwa kuhusu iwapo kizazi kipya cha vijana kingeendelea kuwa karibu na chama hicho au kingeelekea katika vyama vingine vya siasa.

Wengine walihofia kuwa ukosefu wa mikutano ya hadhara ungewafanya wananchi kukisahau chama hicho taratibu.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema taifa, John Heche akiangalia ramani ya ofisi ya chama hicho wilayani Bunda kabla ya kuanza kwa harambee kwaajili ya kufanikisha ujenzi huo. Picha na Beldina Nyakeke

Mikutano ilivyorejesha hamasa

Hata hivyo, taswira inayoonekana sasa katika mikutano ya Chadema inaonyesha hali tofauti na matarajio ya baadhi ya waliokuwa na mtazamo huo.

Tangu kurejea kwake, chama hicho kimeonekana kuingia tena katika ulingo wa siasa kwa kasi iliyowahi kukifanya kuwa miongoni mwa vyama vyenye ushawishi mkubwa nchini.

Mikutano mikubwa iliyofanyika jijini Mbeya, Arusha na Bunda mkoani Mara, imevuta maelfu ya wananchi waliojitokeza kuwasikiliza viongozi wa chama hicho na kushiriki shughuli hizo za kisiasa.

Baadhi walitembea umbali mrefu kwa miguu, huku wengine wakisubiri pembezoni mwa barabara kuu kupokea misafara ya viongozi wa chama hicho, jambo lililozua mjadala mpana mitandaoni na katika duru za kisiasa.

Wachambuzi wa siasa na wadau wa demokrasia wameeleza kuwa Chadema bado inaonekana kubeba matumaini ya sehemu ya wananchi wanaounga mkono siasa zake za mageuzi nchini.

Kwa sasa, chama hicho kimeanza kutangaza kile kinachoitwa Operesheni Katiba Mpya, kampeni ya mikutano ya hadhara inayotarajiwa kuendelea katika maeneo ya Kahama, Mwanza na Serengeti.

Ajenda hiyo inaonekana kupewa uzito mkubwa na viongozi wa chama hicho, ambao wanaendelea kusisitiza umuhimu wa mabadiliko ya mfumo wa kisiasa nchini.

Kwa baadhi ya wachambuzi wa siasa, kinachoonekana sasa si tu kurejea kwa mikutano ya kisiasa, bali pia kurejea kwa ushindani wa kisiasa ambao kwa muda mrefu ulionekana kupungua nchini.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob akihutumia wakazi wa Arusha  kwenye mkutano uliofanyika Mei 8, 2026 eneo la Soko Kuu. Picha na Filbert Rweyemamu

Chadema haijawahi kufa

Mchambuzi wa siasa na mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Dk Salim Ahmed Salim, Denis Konga amesema Chadema hakijawahi kupoteza ushawishi wake licha ya changamoto mbalimbali ilizopitia katika miaka ya hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Konga, msingi wa chama hicho umejengwa kwa muda mrefu kama chama mbadala chenye uwezo wa kutoa ushindani wa kisiasa nchini.

Anasema hata hayati Mwalimu, Julius Nyerere aliwahi kuonyesha kuwa Chadema ilikuwa na nafasi ya kuwa nguvu kubwa katika siasa za Tanzania.

“Chadema haijawahi kufa. Msingi wake umejengwa kama chama mbadala kwa muda mrefu. Kiliwekeza kwa vijana wasomi vyuoni, jambo lilichokipa mtaji wa kisiasa, ushawishi na uwezo wa kuzungumzia matatizo ya wananchi kwa ufasaha,” anasema Konga.

Anasema operesheni zilizofanywa na chama hicho kati ya mwaka 2010 na 2015 za kuhamasisha na kusajili vijana wa vyuo kuingia katika siasa za mageuzi zilijenga msingi muhimu wa kisiasa ambao unaendelea kuonekana hadi sasa.

Kwa mtazamo wake, ujio wa Tundu Lissu katika uongozi wa juu wa chama hicho uliongeza hamasa mpya kwa wananchi wanaotamani mabadiliko ya kisiasa nchini.

Anasema mwitikio mkubwa unaoonekana sasa katika mikutano ya Chadema ni ishara ya ushawishi unaoendelea kujengwa katika ushindani wake dhidi ya CCM.

“Kuingia kwa Tundu Lissu katika uongozi pia kuliongeza chachu kwa chama hicho na matumaini kwa wananchi wanaotamani mageuzi,” anasema.

Anaongeza kuwa wananchi wengi wanahitaji kuona viongozi wenye uthubutu wa kusema ukweli na kutetea maslahi ya taifa bila kuonekana kuwa na mashaka.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ akizungumza wakati wa mkutano wake na wananchi ulipfanyika Uyole jijini Mbeya

Changamoto ya fedha na vyombo vya habari

Hata hivyo, Konga anasema changamoto kubwa inayokikabili Chadema kwa sasa ni uwezo wa kifedha pamoja na uwekezaji katika vyombo vya habari ili kufikisha ujumbe wake kwa wananchi wengi zaidi.

“Mbinu ya mikutano wanayoifanya itawasaidia sana, lakini ninahofu kuhusu uwezo wao wa kifedha katika kuendesha shughuli za kisiasa kwa ufanisi. Siasa za kisasa zinahitaji uwekezaji mkubwa katika mawasiliano na ushawishi wa umma kupitia vyombo vya habari,” anasema.

Anaongeza kuwa nguvu kubwa ya Chadema imeendelea kuwa ni uwezo wake wa kuzungumzia hoja zinazogusa maisha ya wananchi.

“Kinachowabeba ni uwezo wao wa kuzungumzia hoja zinazowagusa wananchi, ndiyo maana mikutano yao inaendelea kuvuta watu wengi,” anasema.

Pamoja na hayo, Konga anatahadharisha kuwa bado ni mapema kutoa hitimisho kuhusu nguvu ya sasa ya Chadema kwa kuangalia mikutano michache pekee.

Bado hakuna uwanja sawa wa kisiasa

Kwa upande wake, mwanahabari mkongwe na mchambuzi wa siasa, Ezekiel Kamwaga anasema Tanzania bado haijafikia mwafaka wa kisiasa unaoweza kuweka mazingira sawa ya ushindani wa kisiasa.

Kwa mtazamo wake, hali hiyo inafanya iwe vigumu kwa vyama vya upinzani, kikiwamo Chadema, kujijenga katika ushindani wa kweli dhidi ya chama tawala.

“Kwa sasa bado hatujafikia mwafaka wa kisiasa kama taifa, na hiyo ndiyo changamoto kubwa. Chadema inaendelea kufanya siasa katika mazingira yale yale ambayo imekuwa ikiyalalamikia kwa muda mrefu,” anasema Kamwaga.

Anasema madai ya Katiba Mpya na mwafaka wa kitaifa bado hayajapatiwa ufumbuzi, jambo linalofanya mazingira ya ushindani wa kisiasa kuendelea kuwa na changamoto.

“Madai ya Katiba Mpya na mwafaka wa kitaifa bado hayajafanyiwa kazi. Hivyo ni vigumu kusema kuna mazingira tulivu kwa vyama kujijenga kiushindani,” anasema.

Kwa mujibu wake, mazingira ya sasa bado hayatoi nafasi ya kupima kwa usahihi uwezo wa vyama vya siasa kujijenga upya na kushindana kwa haki. “Mimi nashauri kwanza kufanyike mwafaka wa kitaifa. Hapo ndipo tutapata mazingira ambayo yatawezesha kupima namna vyama vinavyojijenga kisiasa,” anasema.

Wananchi bado wana matumaini

Naye mdau wa demokrasia na haki za binadamu, Dk Ananilea Nkya anasema nguvu inayoonekana sasa kwa Chadema ni ishara kuwa wananchi bado wanakiona chama hicho kama mbadala wenye uwezo wa kuwasemea.

Anasema mikutano mikubwa inayofanyika katika maeneo mbalimbali nchini inaonyesha wazi kuwa wananchi hawajakichoka chama hicho na bado kina nafasi ya kujijenga kama tishio kwa vyama vingine katika ushindani wa kisiasa nchini.

“Chadema imerejea na inaonekana kuwa na nguvu yake ileile. Hii inaonyesha wananchi bado wanahitaji chama kinachowasemea,” anasema Dk Nkya.

Kwa mujibu wake, kusitishwa kwa shughuli za Chadema hakukuondoa hisia za wananchi kwa chama hicho, bali kulipunguza ushindani wa kisiasa kwa muda.

“Kufungiwa kwa shughuli zao hakukuwaondolea wananchi imani kwa chama hicho, bali kulitoa upinzani katika ushindani wa kisiasa kwa kipindi fulani,” anasema.

Ushindani ni msingi wa maendeleo

Dk Nkya anasisitiza kuwa ushindani wa kweli wa kisiasa ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa, sawa na ilivyo katika sekta nyingine za maisha.

“Hata kwenye michezo, ushindani mkubwa kati ya Simba na Yanga unachochea maendeleo ya soka,” anasema.

Anaongeza kuwa viongozi bora hawawezi kupatikana bila kuwapo kwa ushindani wa kisiasa na uhuru wa mawazo ndani ya jamii.

“Huwezi kupata maendeleo bila ushindani. Maadui wa maendeleo ni wale wanaozuia ushindani wa mawazo,” anasema.

Mjadala unaozidi kushika kasi

Kwa mtazamo wa jumla, wadau mbalimbali wanaona kurejea kwa Chadema kumefungua tena mjadala mpana kuhusu mustakabali wa siasa za ushindani nchini Tanzania.

Wakati wafuasi wa chama hicho wakitafsiri mikutano hiyo kama ishara ya matumaini mapya ya kisiasa, baadhi ya wachambuzi wanaamini bado kuna safari ndefu kabla ya kupima kama nguvu hiyo inaweza kugeuka kuwa ushindani mkubwa wa uchaguzi, kutokana na mazingira ya sasa ya kisiasa nchini.

Hata hivyo, pamoja na tafsiri hizo tofauti, jambo moja linaonekana wazi: Chadema imerejea tena katikati ya mjadala wa kisiasa nchini, na kadri mikutano yake inavyoendelea kuvuta maelfu ya wananchi katika maeneo mbalimbali, ndivyo mjadala kuhusu demokrasia, Katiba Mpya na mustakabali wa upinzani unavyoendelea kushika kasi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *