
Katika mahojiano yetu Farina Gorma amenieleza kwamba wanawake wengi wakimbizi wanaowasili katika mipaka ya Ulaya ambao wengi ni kutoka Afrika tayari wanakuwa wamepitia kiwewe kutokana na safari ndefu na ngumu, lakini wanachokutana nacho ni kama msumari wa moto juu ya kidonda, matatizo lukuki pale wanapojaribu kuelezea yaliyowafika kwa mamlaka za uhamiaji.
“Kwanza kabisa wanafika katika mipaka ya Ulaya wakati ambapo sera za mipaka zimekuwa kali zaidi, hawajui lugha wala mifumo ya Ulaya na wanatafuta msaada. Wengi wao ni manusura wa FGM lakini hata hawajui kuwa hilo linaweza kuwa sababu ya wao kuruhusiwa kubaki hivy wanakuja mpakani hata hivyo wanahitaji kuthibitisha kwa nini wako hapo.”
Kisha akasema mchakato wa kuelezea mara kwa mara simulizi zao za maumivu kwa maafisa wa uhamiaji, wakalimani na madaktari unaweza kuwaongezea maumivu ya kiwewe, hasa katika jamii ambako masuala hayo bado ni mwiko akisistiza kuwa
“Tunahitaji mifumo inayozingatia hali ya kiwewe katika sera, huduma za afya na hata katika namna mamlaka zinavyowashughulikia ili wanawake wasilazimike kuelezea simulizi zao tena na tena. Tunahitaji pia kuziwezesha jamii za diaspora na jamii mbalimbali za Waafrika ili ziwe tayari kusaidia watu wao wenyewe.”
Gorma anasema AfroKids International inafanya kazi kubwa na kwa karibu na hospitali, washauri wa kisheria, wataalamu wa afya ya akili na viongozi wa jamii ili kujenga imani na kuwaunganisha wanawake hao na msaada wanaouhitaji. Ameongeza kuwa uwezeshaji wa jamii ni muhimu katika kuwasaidia manusura kurejesha hali ya kujiamini na kujenga upya maisha yao baada ya kuonja shubiri na ndio maana wanakimbilia shirika hilo
“Kwanza kabisa watu wanakuja kwetu kwa sababu kama Waafrika wanawaamini Waafrika na hapo wanaweza kuzungumza kwa uhuru na sisi tunaelewa. Hivyo wanahisi kuwa salama na kisha tunashirikiana kuwasaidia kupata huduma sahihi. Tunajaribu kuwawezesha wanawake ili waweze kuwa na sauti yao wenyewe.”
Kwa Farina Gorma AfroKids International shirika linalofanyakazi katika nchi 41duniani ni daraja kwa wanawake na wasichana wakimbizi kusahau yaliyopita na kuanza kuganga yajayo.