Dar es Salaam. Wataalamu wa afya ya macho wameeleza kuwa kuimarishwa kwa programu za mwongozo wa kitaaluma kwa madaktari wanaosomea udaktari bingwa wa macho ni moja ya suluhisho muhimu la kupunguza ongezeko la wagonjwa wa mtoto wa jicho na tatizo la upofu nchini.
Hayo yameelezwa katika mafunzo maalumu ya mwongozo wa kitaaluma kwa madaktari wanaosomea udaktari bingwa wa macho yaliyoratibiwa na taasisi ya Eye Corps (IOP), yakihusisha wataalamu wa ndani na nje ya Tanzania kwa lengo la kuongeza ujuzi wa vitendo kwa madaktari hao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Eye Corps, Dk Susan Macdonald ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa macho, amesema Tanzania imeonyesha hatua kubwa kwa kuongeza idadi ya wanafunzi wa udaktari bingwa wa macho, lakini changamoto iliyopo sasa ni uhaba wa wakufunzi wa kuwapa mafunzo ya vitendo kwa kiwango kinachohitajika.
Amesema zamani nchi ilikuwa na wanafunzi sita pekee wa udaktari bingwa wa macho kwa mwaka, lakini sasa wameongezeka hadi kufikia wanafunzi 20 kwa mwaka katika programu za miaka mitatu hadi minne.
“Serikali imefanya uamuzi mzuri wa kuongeza idadi ya madaktari wa macho wanaosomea utaalamu wa kibingwa, lakini swali ni nani atawafundisha? Hatuna wakufunzi wa kutosha,” amesema Dk Macdonald.
Mkurugenzi Mtendaji wa Eye Corps, Dk Susan Macdonald ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa macho akitoa maelekezo kwa baadhi ya madaktari wanaosomea ubingwa na ubobezi wa macho (hawapo pichani).
Amesema kupitia ushirikiano kati ya Eye Corps na Wizara ya Afya, wamekuwa wakifanya kambi za matibabu katika maeneo yasiyo na madaktari bingwa wa macho huku wakitumia nafasi hiyo kuwafundisha madaktari wanaosomea utaalamu huo.
“Kwenye huduma mkoba zetu tunaenda na timu kubwa yenye wataalamu wabobezi pamoja na wanafunzi. Tunataka wagonjwa wapate huduma bora lakini pia tunataka wanafunzi wapate nafasi ya kujifunza kwa vitendo,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Macdonald, moja ya makosa yanayoweza kutokea ni madaktari wanaohitimu kutopata mafunzo ya kutosha ya upasuaji na baadaye kushindwa kufanya upasuaji katika maisha yao yote ya kazi.
“Lengo letu siyo tu kufanya operesheni nyingi kwenye kambi za matibabu, bali kuhakikisha kuna ufundishaji na mafunzo ya kutosha kwa madaktari hawa,” amesema.
Mkurugenzi wa Mafunzo wa Eye Corps, Dk Roger Furlon amesema taasisi hiyo inalenga kuendelea kushirikiana na Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na vyuo vya mafunzo ya udaktari ili kujenga mfumo endelevu wa kuwazalisha madaktari bingwa wazawa wenye uwezo wa kutoa huduma kote nchini.
Amesema changamoto kubwa ni kwamba baadhi ya madaktari wanaohitimu hupelekwa katika mikoa mbalimbali wakiwa peke yao bila kupata msaada wa kitaalamu wa karibu.
Mkufunzi na daktari bingwa wa Retina kutoka Hospitali ya CCBRT, Mustafa Yusufali amesema mwongozo wa kitaaluma ni muhimu kwa Tanzania kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi kulinganisha na uwezo wa vyuo kutoa mafunzo ya vitendo.
“Shule ni chache na wanafunzi ni wengi, hivyo wengi hawapati nafasi ya kutosha ya kufanya kwa njia ya vitendo. Mwongozo wa kitaaluma unawasaidia kuongeza ujuzi kwa kufanya mazoezi zaidi,” amesema.
Baadhi ya wanafunzi wa udaktari bingwa wakiwa katika mafunzo hayo.
Amesema teknolojia mpya inayotumiwa katika mafunzo hayo imekuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi kwa kuwa inawawezesha kuona kile anachokiona mwalimu wakati wa upasuaji.
“Kuna vitu mwalimu anaona lakini mwanafunzi hawezi kuona vizuri. Kupitia kamera na vifaa vya kisasa anaweza kuona hatua zote za upasuaji na kuelewa haraka zaidi,” amesema.
Dk Yusufali amesema tatizo kubwa la macho nchini kwa sasa ni mtoto wa jicho, huku akieleza kuwa tofauti na zamani ambapo ugonjwa huo ulikuwa ukiwaathiri zaidi wazee, sasa unaanza kuonekana hata kwa watu wenye umri wa miaka 40.
“Lishe na matumizi makubwa ya teknolojia vinaweza kuwa sehemu ya sababu zinazochangia wagonjwa kupata mtoto wa jicho mapema,” amesema.
Aidha amewahamasisha wananchi kwenda kupima macho mapema badala ya kusubiri hali kuwa mbaya.
“Watu wengi wanapuuzia tatizo la macho hadi linakuwa kubwa. Ukiona dalili nenda hospitali mapema,” amesema.
Kwa upande wake, daktari bingwa wa retina kutoka KCMC, Dk Maria Kissanga amesema mwongozo wa kitaaluma umekuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi wa udaktari bingwa kwani huwapa nafasi ya kuona magonjwa mbalimbali na kushiriki upasuaji kwa vitendo.
Amesema hivi karibuni walifanya kambi ya wiki mbili mkoani Mbeya ambapo waliwahudumia na kuwafanyia upasuaji wagonjwa karibu 170 huku wanafunzi sita wa udaktari bingwa wakipata nafasi ya kujifunza kwa karibu.
Dk Kissanga amesema wanafunzi hao hupimwa uwezo wao kwa mfumo maalumu unaoitwa Oscar unaotathmini hatua kwa hatua maendeleo ya mwanafunzi hadi kufikia uwezo kamili wa kufanya upasuaji kwa usahihi.
“Baadaye hawa wanafunzi nao watakuwa wakufunzi wa kizazi kijacho cha madaktari,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa Mafunzo wa Eye Corps Tanzania, Dk Dennis Nachipyangu amesema tangu mwaka 2018 taasisi hiyo imekuwa ikifanya kazi katika kanda mbalimbali nchini ikiwamo Kilimanjaro na Lindi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya.
“Tunataka daktari aliyeko kijijini aweze kutoa huduma kwa kiwango cha kimataifa kama daktari aliyepo mjini,” amesema.