Dodoma. Serikali imetangaza kuwa katika mwaka wa fedha 2026/27, Shirika la Reli Tanzania (TRC) halitatengewa ruzuku kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali kwa ajili ya mishahara wala matumizi mengine ya uendeshaji, kutokana na uwekezaji uliofanyika tangu mwaka 2017 uliliwezesha shirika hilo kujijenga kifedha.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Jumatano, Mei 13, 2026 na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Uchukuzi yenye thamani ya Sh2.9 trilioni, ambayo imebeba vipaumbele nane vya maendeleo ya sekta hiyo.

Waziri Mbarawa amesema TRC sasa imefikia hatua ya kuanza kujiendesha bila kutegemea ruzuku ya Serikali, na kwamba tangu Januari 2026 shirika hilo limekuwa likigharamia mishahara na matumizi mengine ya uendeshaji (OC) kwa kutumia mapato yake yenyewe.

 “Kwa kipindi cha takriban miaka 10, kiasi cha Sh12.92 bilioni  kila mwaka kilikuwa kinatolewa na Serikali kwa TRC kwa ajili ya mishahara, hivyo uwezo wa kujitegemea upo na inawezekana kwani tangu Januari mwaka huu tumeona hali hiyo,” amesema Profesa Mbarawa.

Kauli ya hiyo inaondoa malalamiko ya muda mrefu kwamba Shirika hilo lilikuwa linaitia hasara Serikali lakini hata zilipoanzishwa safari za treni ya mwendo kasi, kulikuwa na tetesi kwamba inajiendesha kwa hasara kutokana na kubeba viongozi na wajumbe wa chama kimojawapo.

Ni kutokana na hilo, Waziri amesema Serikali imeamua kuwekeza zaidi katika ujenzi wa reli katika vipande viwili vilivyobakia ikiwemo Tabora – Isaka (km 165) na Serikali imepata mkopo wenye masharti nafuu wa thamani ya Dola 1.3 bilioni za Marekani ambazo ni sawa na takriban Sh3.3 trilioni.

Amesema TRC itaanza kujiendesha bila ruzuku kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali na kwamba tangu Januari, 2026 wameanza kujitegemea kwa upande wa mishahara na matumizi mengineyo (OC) bila uwezeshaji kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali.

Waziri Mbarawa ametaja eneo lingine alilosema wamefanikiwa ni kwenye uwekezaji mkubwa wa Bandari ya Dar es Salaam ambao umevuka zaidi ya nusu ya malengo ya uwekezaji yaliyokuwa dola 250 milioni sawa na Sh650 bilioni ndani ya kipindi cha miaka mitano ambayo ni mafanikio makubwa ndani ya kipindi cha miaka miwili ya kwanza ya uwekezaji.

Amesema katika mwaka wa fedha 2026/27, maboresho yataendelea kupitia upanuzi wa miundombinu, uboreshaji wa mifumo ya utendaji, na kuimarisha uwezo wa kuhudumia mizigo kwa viwango vya kisasa.

Miongoni mwa mipango hiyo ni ununuzi wa mitambo ya kisasa ya upakuaji na upakiaji (cranes), ujenzi wa mageti mawili yanayounganisha bandari na Barabara ya Nelson Mandela, pamoja na uwekezaji katika mitambo ya kushughulikia shehena.

“Uwekezaji huo utaongeza uwezo wa kushughulikia shehena kwa asilimia 65 hadi kufikia tani 5.5 milioni huku huduma za mizigo mchanganyiko zikitarajia kuongezeka kwa asilimia 25 kwani mageuzi hayo yataongeza ushindani wa bandari za Tanzania na kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa lango kuu la biashara,” amesema Profesa Mbarawa.

Amevitaja vipaumbele vitakavyotekelezwa katika bajeti ijayo ikiwamo uendeshaji wa Reli ya Kisasa ya (SGR) na ukarabati na uboreshaji wa Reli ya zamani (MGR), uboreshaji wa miundombinu na huduma katika bandari, kuboresha usafiri wa anga, ujenzi na ukarabati wa meli na kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa.

Maeneo mengine yaliyoangaziwa ni kuboresha udhibiti, ubora na usalama wa huduma za uchukuzi na kuendelea na uboreshaji wa vyuo vya mafunzo vya kisekta ambapo kiasi cha Sh2.7 trilioni zitatumika kwa shughuli za maendeleo.

“Mheshimiwa Spika, miradi itakayotekelezwa katika eneo hili ni pamoja na uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam (DMGP), ambao utatekelezwa kupitia mapato ya ndani ya TPA ikiwamo uboreshaji wa bandari za mwambao wa Bahari ya Hindi, Bandari ya Bagamoyo, Mtwara (Kisiwa Mbao) na bandari za 28 Maziwa Makuu,” amesema Profesa Mbarawa.

Utekelezaji mwingine utakuwa katika Bandari za Mwanza North, Mbamba Bay, na uboreshaji wa Bandari ya Kigoma huku Bandari ya Dar es Salaam kupitia sekta binafsi, DP World inaendelea na mpango wa uwekezaji katika vifaa vya kisasa vya kuhudumia mizigo ili kuongeza ufanisi, kasi na ushindani wa huduma.

“Kwa mwaka wa fedha 2026/27, maboresho yataendelea kupitia upanuzi wa miundombinu, uboreshaji wa mifumo ya utendaji na kuimarisha uwezo wa kuhudumia mizigo kwa viwango vya kisasa na miongoni mwa mipango hiyo ni ununuzi wa mitambo ya kisasa ya upakuaji na upakiaji (cranes), ujenzi wa mageti mawili yanayounganisha bandari na Barabara ya Nelson Mandela,” amesema Profesa Mbarawa.

Amesema kwa upande wa sekta ya usafirishaji wa magari (PCC na PCTC), yenyewe inatarajiwa kukua kwa asilimia 30 kutokana na maboresho ya sera na miundombinu ambapo ifikapo mwaka 2028, sekta ya bandari inatarajiwa kuwa imepiga hatua kubwa ya mageuzi.

Usafiri wa anga

Kwa upande wa usafiri wa anga, bajeti inaelekeza ununuzi wa Ndege na Uimarishaji wa Kampuni ya ATCL, ujenzi wa Chuo cha Usafiri wa Anga, ujenzi, ukarabati na uboreshaji wa viwanja vya ndege vya Mwanza, Arusha, Mtwara, Serengeti, Kagera, Kilimanjaro (KIA) na Julius Nyerere (JNIA).

Nyingine ni Viwanja vya ndege vya mikoa ambapo imeguswa Moshi, Lindi, Njombe, Musoma na Singida huku akitaja Miradi ya Uboreshaji wa Vyuo vya Mafunzo ya Kisekta itakayotekelezwa ambayo ni ununuzi wa vifaa vya Kufundishia katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Maoni ya Kamati

Akisoma maoni ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Moshi Kakoso ameitaka Serikali ihakikishe inatoa fedha za maendeleo kama zilivyoidhinishwa na Bunge na kusimamia kikamilifu miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Wizara hii ili kuleta tija iliyokusudiwa.

“Kamati inashauri kuwa, Serikali ianze kutekeleza matumizi ya ada mpya kwa watumiaji wa Bandari nchini kuanzia Julai Mosi, 2026 ili kuhakikisha TPA inapata fedha za kuendeleza miundombinu ya Bandari nchini,” amesema Kakoso.

Akichangia kwenye bajeti hiyo, Mbunge wa Geita Vijijini Joseph Musukuma ameitaka Serikali kuwasimamia Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (Latra) kwa kuwa, wamegeuka kitega uchumi kwa Serikali na siyo msaada kwa wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *