LIGI Kuu Tanzania Bara inaendelea leo kwa michezo minne kupigwa, huku vita ya pointi tatu ikitarajiwa kusakwa kibabe kuanzia saa nane mchana. Katika vita hiyo, kuna shoo ya Clatous Chama na Seleman Mwalimu watakapoongoza mashambulizi ya Simba mbele ya Mashujaa.
Mapema saa 8:00 mchana, kutakuwa na michezo miwili ambapo Mtibwa Sugar itaikaribisha KMC, huku Tanzania Prisons nayo ikiwa mwenyeji wa Fountain Gate. Baada ya michezo hiyo, Simba itakuwa mgeni wa Mashujaa, kisha Azam itahitimisha siku kwa kuikaribisha Pamba Jiji.
Macho na masikio ya wengi yataelekezwa Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma kuanzia Saa 10:15 jioni ambapo Mashujaa itaikaribisha Simba kwenye mchezo unaosubiriwa kwa shauku kutokana na ubora wa timu hizo mbili kwenye ligi.
Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa kwenye ubora mkubwa wa matokeo ambapo mechi tano zilizopita imeshinda nne na kutoka sare moja dhidi ya Yanga. Katika michezo hiyo, Wekundu hao wamefunga mabao 13 na kuruhusu matatu pekee huku wakiendelea kuifukuzia Yanga iliyo kileleni mwa msimamo.
Wekundu hao watamtegemea mshambuliaji wao kinara Seleman Mwalimu ambaye ndiye anaongoza kwa mabao ndani ya kikosi hicho akiwa nayo saba, lakini pia kiungo fundi Clatous Chama ambaye amerejea kwenye kiwango bora baada ya kufunga mabao matatu katika mechi tatu zilizopita, naye atatazamwa.
Simba pia itashuka uwanjani ikiwa na rekodi nzuri mbele ya Mashujaa kwani katika michezo mitano ya ligi iliyowakutanisha, imeshinda yote ikifunga mabao manane na kuruhusu moja.
Hata hivyo, Mashujaa inayonolewa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, ina rekodi ya kutopoteza nyumbani msimu huu ikishinda nne na sare saba.
Akizungumzia mchezo huo, kocha wa Simba, Steve Barker, alisema anaamini utakuwa mgumu kutokana na ubora wa Mashujaa nyumbani, lakini ana imani wachezaji wake watatekeleza vizuri mpango waliouweka.
“Nilikuwa naangalia mechi ya mwisho tulipocheza nao, ilikuwa ngumu, naamini pia haitakuwa rahisi safari hii kwani ni timu inayoonyesha upinzani mkubwa ikiwa nyumbani, lakini tunataka kuendelea kushinda, naamini wachezaji wangu watatekeleza vizuri mpango wa mechi hii,†alisema Barker.
Kwa upande wa Mashujaa, moja ya silaha kubwa msimu huu imekuwa ugumu wa kufungwa nyumbani, jambo ambalo Simba italazimika kulitafutia majibu leo mbele ya kikosi hicho kinachofundishwa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.
Katika mechi tano zilizopita, Mashujaa haijapoteza, imetoa sare nne na kushinda moja dhidi ya TRA United kwa bao 1-0.
Tangu Julio aichukue timu hiyo kutoka kwa Salum Mayanga, hajapoteza mchezo wowote huku kikosi chake kikifunga mabao mawili katika michezo mitano ya mwisho. Mashujaa ipo nafasi ya tisa ikiwa na pointi 26 baada ya kufunga mabao 11 na kuruhusu 19, takwimu hizi ni kabla ya mechi za jana.
Simba pia italazimika kuwa makini na washambuliaji wa Mashujaa, Jafary Kibaya aliyefunga mabao mawili pamoja na Ismail Mgunda mwenye moja alilofunga dhidi ya TRA United kwani wakiwaachia nafasi, watalizwa.
Kocha Julio alisema licha ya kuheshimu ubora wa Simba, lakini kikosi chake hakitakuwa na hofu mbele ya Wekundu hao.
“Tunaiheshimu Simba lakini kama ambavyo siku zote nimekuwa nikisema, sidhani kama tuna sababu ya kucheza kwa hofu dhidi yao, nimewaambia wachezaji hizi ndio mechi ambazo zitawatambulisha juu ya ubora wao, tutakwenda kuwapa shida kucheza kwa utulivu wao,” alisema Julio.
HAWA WANALIAMSHA MAPEMA TU
Katika michezo ya mapema kuanzia saa 8:00 mchana, Mtibwa Sugar itaikaribisha KMC kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Mtibwa inarejea kucheza nyumbani kwenye Uwanja wa Jamhuri baada ya kifungo cha muda mrefu huku ikisaka pointi muhimu za kujiimarisha kwenye msimamo.
Katika mechi tano zilizopita, Mtibwa haijashinda mchezo wowote ikipoteza minne na kutoa sare moja. Mara ya mwisho kushinda ilikuwa Februari 2, 2026 ilipoifunga Prisons mabao 2-1. Walima miwa hao wanahitaji ushindi ili kupanda kutoka nafasi ya 12 hadi ya 10 kwenye msimamo.
Hali hiyo haipo tofauti kwa KMC ambayo nayo ipo kwenye hatari ya kushuka daraja. Mara ya mwisho kushinda ilikuwa Februari 3, 2026 ilipoifunga Mashujaa bao 1-0.
Iwapo KMC itapoteza mchezo wa leo, itaendelea kubaki karibu zaidi na eneo la kushuka daraja ikiwa nafasi ya 16 na pointi tisa.
MSAKO WA NSAJIGWA KWA MINZIRO
Mchezo mwingine wa saa nane mchana utakuwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ambapo Tanzania Prisons itakuwa mwenyeji wa Fountain Gate.
Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Shadrack Nsajigwa katika kuelezea maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Fountain Gate, alisema watashambulia mwanzo mwisho.
Nsajigwa ambaye ameiongoza timu hiyo kwa michezo tisa bila ushindi, presha imeonekana kuwa kubwa nje na ndani ya uwanja katika hesabu za kukwepa kushuka daraja.
Prisons haijawa na matokeo mazuri ikiwa nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikikusanya pointi 14, ambapo leo Nsajigwa atakuwa akisaka ushindi wa kwanza kwake tangu aungane na Wajelajela hao dhidi ya Fountain Gate ambayo imeonekana kuimarika chini ya Kocha Fred Felix ‘Minziro’.
Katika michezo 22 iliyocheza timu hiyo ya jijini Mbeya, imekusanya pointi 14 na kuwa nafasi ya 15 ambapo inahitaji ushindi mechi zilizobaki kujihakikishia kubaki salama Ligi Kuu Bara.
Akizungumza na Mwanaspoti, Nsajigwa alisema baada ya kusota kwa muda mrefu bila kupata pointi tatu, kesho huenda ikawa safari ya matumaini mapya watakapoilaza Fountain Gate na kuianza upya Ligi Kuu, huku akitoa angalizo kwa nyota wa kikosi chake.
Alisema baada ya kufanikisha kutengeneza muunganiko na unyumbulifu kwa timu katika kutengeneza nafasi bila kuzitumia vyema, amewaandaa vizuri wachezaji kuhakikisha kesho wanafanya kweli.
“Tumeshafungwa sana, ila sisi hatujashinda, kesho ni kushambulia tu kusaka mabao na kulinda pointi tatu, vijana nimewaandaa kiakili, kimbinu na kiufundi ili tuianze upya safari ya matumaini.
“Tunajua rekodi na historia yetu nyuma kwamba kila msimu huwa tuna mechi zinazotubeba hadi kubaki, hivyo hatujakata tamaa na tunaweza kubaki salama, ila lazima tushinde michezo hiyo,” alisema kocha huyo.
Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Fred Felix ‘Minziro’ amesema wanafahamu mchezo huo ugumu wake kutokana na wapinzani walivyo akisisitiza kuwa timu hiyo pia haijawa salama, hivyo lazima kupambania walichonacho kwa sasa.
Alisema ushindi na matokeo waliyopata katika mechi zilizopita hadi kuwa nafasi ya 10 kwa pointi 25, haiwafanyi kubweteka bali kulinda mwendelezo huo ili kukwepa kushuka daraja.
“Wachezaji wako tayari kwa mchezo na sisi hatuko salama sana, tunaenda kwa nidhamu, heshima na tahadhari katika mchezo huo kwa kuwa Prisons ni timu nzuri, ukifanya makosa wanakuadhibu,” alisema kocha huyo.
AZAM KUJIULIZA
Baada ya kutoka kuchapwa mabao 4-1 na TRA United, Azam leo itakuwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuikaribisha Pamba Jiji, mechi itakayoanza saa 12:30 jioni.
Kipigo ilichopokea kutoka kwa TRA United, kilikuwa cha kwanza kwa Azam kwenye ligi msimu huu, hivyo itaingia kwa hasira kulinda rekodi ya kutopoteza nyumbani kwani imeshinda sita na sare nne.
Azam imesisitiza kuwa inataka kurejea kwenye njia ya ushindi huku ikikumbuka kwamba mchezo wa kwanza dhidi ya Pamba Jiji uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 ulikuwa mgumu kwao.
Kwa Pamba Jiji, haina rekodi nzuri ikiwa ugenini kwani imeshinda mechi mbili pekee, huku ikipoteza tano na sare nne. Mechi nane zilizopita, Pamba Jiji imeshinda moja pekee, sare zikiwa nne na vichapo vitatu.