
Mwanza. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza imezuia hasara ya zaidi ya Sh27.5 milioni katika mradi wa maji wa Mahaha, Wilaya ya Magu baada ya kubaini matumizi ya nyaya (cable) zisizo na ubora ambazo zingeweza kusababisha kuharibika kwa mfumo wa sola unaosukuma maji kwenye pampu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Mei 14, 2026 Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Abnery Mganga amesema hitilafu hiyo ilibainika katika ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo uliofanyika kati ya Januari hadi Machi 2026.
Amesema uchunguzi ulibaini nyaya zilizotumika kuunganisha umeme kutoka kwenye sola paneli kwenda kwenye pampu hazikuwa za kiwango kilichoainishwa kwenye orodha ya makadirio ya mradi (BOQ).
Amesema badala ya kutumia waya uliokusudiwa aina ya ‘armoured cable’ ulitumika wa kawaida usio na ubora, hali ambayo ingeweza kusababisha mfumo wa sola kushindwa kufanya kazi na hivyo kuharibu pampu na vifaa vyote vya mradi vyenye thamani ya Sh27.5 milioni.
“Waya huo duni usiokuwa na kiwango kilichokusudiwa uliotumika kwenye kufunga pampu pamoja na sola paneli ambao kazi yake ni kutoa umeme kwenye sola paneli kwenda kwenye pampu ili kusambaza maji…
Haukuwa na uwezo wa kufanya kazi hiyo hali ambayo bila ya ufuatiliaji wa Takukuru ingesababisha pampu na solka paneli kufa na kusababisha hasara ya mradi mzima wa Sh400 milioni,”amesema Mganga.
Katika hatua nyingine, Takukuru imefanikiwa kurejesha ardhi ya kijiji yenye ukubwa wa ekari 26 na thamani ya Sh36 milioni katika kijiji cha Shigangama, Wilaya ya Kwimba, iliyokuwa imeuzwa kwa Sh13 milioni kinyume cha taratibu.
Mganga amesema katika tukio hilo, mnunuzi alilipa awali Sh9 milioni ambazo hazikuingizwa kwenye mapato ya kijiji, jambo lililokiuka taratibu za kifedha za Serikali za mitaa.
Baada ya uchunguzi, ardhi hiyo imerejeshwa kwa wana kijiji huku, wahusika ambao ni baadhi ya viongozi wa kijiji hicho kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria.
“Ardhi imerejeshwa na fedha zile Sh9 milioni zimerudishwa kwa mnunuzi ambaye hakuwa na hatia,”amesema.
Ameeleza katika kipindi hicho, Takukuru imepokea taarifa 79, ambapo 46 zinahusu rushwa na 33 hazikuhusu rushwa.
Amesema uchunguzi umeanzishwa kwa taarifa za rushwa, huku zisizohusu rushwa zikitolewa ushauri au kupelekwa kwenye taasisi husika kwa hatua zaidi.
“Tumefanikiwa kushinda kesi 13 kati ya 14 zilizotolewa uamuzi mahakamani na kesi mpya 14 zimefunguliwa na nyingine tisa za zamani zinaendelea kusikilizwa,”amesema Mganga.