Uamuzi huo ulithibitishwa na Makamu wa Rais wa WBC, Houcine Houichi, ambaye alisema baraza hilo lilifanya jitihada mbalimbali kuwasiliana na menejimenti ya bondia huyo kabla ya kuchukua hatua hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Houichi ambaye pia ni Rais wa African Boxing Union (ABU), alisema WBC ilikuwa ikiwasiliana mara kwa mara na kambi ya Majiha kuhusu wajibu wa kutetea ubingwa wake, lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda.

Kwa mujibu wa Houichi, Majiha aliendelea kushiriki mapambano yasiyo ya ubingwa badala ya kupanga pambano rasmi la kutetea mkanda huo, jambo lililoifanya WBC kutokuwa na chaguo zaidi ya kumvua taji hilo.

“Tumefanya jitihada kadhaa kuwasiliana na timu ya usimamizi ya bondia huyo kuhusu utetezi wa ubingwa wake, lakini kwa bahati mbaya juhudi hizo hazikufanikiwa,” alisema Houichi.

“Aliendelea kupigana mapambano mbalimbali yasiyo ya ubingwa huku mkanda ukiendelea kutokuwa hai kwa muda mrefu. Kwa mujibu wa kanuni za WBC, hatukuwa na chaguo jingine zaidi ya kufanya uamuzi huu.”

Houichi alisema Tanzania ina mabondia wengi wenye vipaji na uwezo wa kushindana kimataifa, lakini changamoto kubwa ipo kwenye mifumo dhaifu ya usimamizi wa mabondia hao.

“Nafahamu Tanzania ina mabondia wengi wenye vipaji na nguvu, lakini wanakosa usimamizi wa kitaalamu,” alisema. “Bondia anaweza kupambana kwa juhudi kubwa kupata pambano la ubingwa na kuwa bingwa, lakini pia anaweza kupoteza ubingwa huo kwa urahisi kutokana na kukosekana kwa usimamizi mzuri na kushindwa kupanga mapambano ya utetezi kwa wakati.”

Hatua hiyo ni pigo kubwa kwa Majiha ambaye alikuwa ameijengea Tanzania heshima kubwa kwenye ndondi za kulipwa baada ya kutwaa ubingwa wa WBC mwaka 2023. Mafanikio yake yaliwapa matumaini mashabiki wa ndondi nchini kwamba angekuwa mmoja wa mabondia wakubwa wa Tanzania kwenye medani ya kimataifa.

Hata hivyo, uamuzi huo sasa unamwacha bondia huyo bila mkanda huo wenye hadhi kubwa na kuzua maswali kuhusu mustakabali wa maisha yake ya ndondi za kulipwa.

Wadau wa ndondi nchini wamekuwa wakieleza mara kwa mara wasiwasi wao kuhusu ukosefu wa usimamizi na mipango bora kwa mabondia wa kulipwa, wakisema wengi wao hushindwa kuendeleza mafanikio baada ya kufanya vizuri kimataifa.

Kupoteza ubingwa huo kunatarajiwa kuwa funzo kwa mameneja na mapromota wa ndondi nchini kuhusu umuhimu wa kufuata kanuni za kimataifa za ndondi na kuhakikisha mabingwa wanatimiza masharti ya kutetea mataji yao ndani ya muda uliopangwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *