
Watu milioni 19.5 nchini Sudan wanakabiliwa na viwango vya juu vya kutokuwa na uhakika wa kupata chakula na hali hiyo itaendelea hadi mwishoni mwa mwezi huu wa Mei, idadi ambayo ni sawa na asilimia 41 ya wananchi wote nchini humo.
Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya uainishaji wa viwango vya upatikanaji wa chakula, IPC iliyochapishwa leo ikisema kiwango hicho ni cha tatu au IPC 3 kikitambuliwa kuwa ni janga kati ya vipimo vitano, ambapo kipimo cha tano ni cha juu ambacho ni baa la njaa.
Je ikiwa IPC 5 ina maana gani?
Kwa ainisho hilo, kwenye taifa hilo ambalo mgogoro wake wa kibinadamu ni mkubwa zaidi duniani, watu wengine 135, wako katika kipimo cha tano au IPC inayotambuliwa kuwa ni baa la njaa kwani wana upungufu mkubwa wa chakula, njaa kali, viwango vya juu sana vya utapiamlo, na vifo vinavyotokana na magonjwa au utapiamlo mkali.
Ripoti hiyo inasema watu wengine zaidi ya watu milioni 5 wamewekwa katika kipimo cha 4 au (IPC) ambacho ni dharura, ambapo hali inatarajiwa kuzorota zaidi katika msimu wa mwambo unaoanza mwezi Juni hadi Septemba mwaka huu.
Hatari ya maeneo kutumbukia kwenye baa la njaa
Ingawa hadi sasa hakuna eneo lililo katika hali ya baa la njaa, maeneo 14 jimboni Darfur Kaskazini, Darfur Kusini, na Kordofan Kusini yako katika hatari ya kukumbwa na baa la njaa ikiwa mapigano yataongezeka zaidi, upatikanaji wa chakula kuzorota, huduma za afya pamoja na hali za maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi kudhoofika, au watu zaidi kuhama makazi yao.
Utapiamlo mkali wa watoto umeenea sana, huku ikikadiriwa kuwa watoto 825,000 wataathirika vibaya mwaka 2026 kutokana na kupungua kwa upatikanaji wa matibabu.
Migogoro inaendelea kuwa na madhara makubwa kwa hali ya upatikanaji wa chakula na lishe ya watu wa Sudan.
Zaidi ya watu milioni 8.9 wamekimbia makazi yao ndani ya nchi, na inakadiriwa kuwa asilimia 40 ya vituo vya afya havifanyi kazi.
IPC huandaliwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na wadau mbali mbali zikiwemo serikali.
Athari mbayá za mgogoro Mashariki ya Kati
Mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati unaongeza changamoto nyingine katika hali ya Sudan, kwa kuchangia kupanda kwa bei za mafuta, chakula, na mbolea.
Upatikanaji wa misaada ya kibinadamu bado umewekewa vikwazo vikubwa, hali inayopunguza utoaji wa msaada pamoja na upatikanaji wa taarifa katika baadhi ya maeneo yaliyoathirika zaidi.
Hatua za kuchukua
Ripoti inataja hatua za haraka za kuchukua kuwa ni pamoja na kusitishwa kwa mapigano, kuboreshwa kwa upatikanaji wa misaada, na kuongeza kiwango cha msaada.
Hatua hizo, kwa mujibu wa ripoti hiyo ni muhimu ili kuzuia hali isiendelee kuzorota zaidi. “Vinginevyo, uwezekano wa kuwa na maboresho ya maana katika hali ya upatikanaji wa chakula na lishe nchini Sudan mwaka 2026 ni mdogo sana,” imesema ripoti.
Kuhusu IPC
IPC huandaliwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na wadau mbali mbali zikiwemo serikali.