“Na kutokana na dhamira iliyo wazi ya mageuzi na mafanikio yaliyopatikana hadi sasa, leo tunafurahi tena pamoja na Msimamizi wa sera Lewin, Mratibu Mkuu wa Misaada Fletcher, kutangaza ongezeko la ufadhili wa ziada wa dola bilioni 1.8 kwa misaada ya kibinadamu. Fedha hizi zitaokoa maisha zaidi duniani kote, lakini pia zitasukuma mbele mageuzi tuliyoyaweka kwa ajili ya ufanisi, uwajibikaji na athari endelevu.”

Tangazo hilo limetolewa na Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Mike Waltz kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa New York Marekani katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na maafisa wa Umoja wa Mataifa Mkuu wa Misaada ya Kibinadamu Tom Fletcher na Jeremy P. Lewin Naibu Msimamizi wa Sera na Programu na Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).

Balozi Waltz ameongeza kuwa Marekani bado ndiyo mchangiaji mkubwa zaidi wa misaada ya kibinadamu duniani lakini inataka kuhakikisha kila dola inayotoa inawafikia watu wenye uhitaji wa haraka kwa ufanisi zaidi.

“Mageuzi si hiari. Ni ya lazima ili kuhakikisha kila dola inawafikia watu walio katika hali ya dharura,” amesema Waltz, akisisitiza kuwa misaada lazima itafsiriwe kuwa matokeo halisi kwa walioko hatarini.

Mpango wa chakula wa dola bilioni 2 kuongoza mageuzi ya misaada

Waltz ametaja makubaliano ya maelewano ya mwezi Desemba yanayotoa dola bilioni 2 kwa msaada wa chakula, ikiwa sehemu ya kile alichokiita “mabadiliko ya misaada ya kibinadamu” unaoongozwa na Tom Fletcher. Mpango huo unalenga kupunguza urudufu wa kazi, kuboresha uratibu na kuongeza kasi ya utoaji wa misaada katika majanga kama njaa, vita na majanga ya asili.

Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, mageuzi haya yanalenga kupunguza urasimu unaochelewesha hatua za dharura na kuhakikisha misaada inafika kwa haraka zaidi kwa walioko hatarini.

UN yazipokea dola bilioni 1.8 kwa mikono miwili

Na mara baada ya tangazo hilo Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Msemaji wa Katibu Mkuu wa wa Umoja wa Mataifa amesema “Umoja wa Mataifa unapokea kwa mikono miwili mchango huo”, akibainisha athari zake za haraka kwa operesheni za kimataifa za misaada.

 “Mchango huu utawawezesha wahudumu wa misaada ya  kibinadamu kuwafikia mamilioni ya watu katika migogoro mikubwa zaidi kwa msaada wa kuokoa maisha,” amesema Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu Farhan Haq, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu katika taarifa hiyo.

Fletcher: Ni mchango muhimu kwa mfumo wa misaada uliotaabani

Kwa upande wake Mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa amekaribisha ahadi hiyo ya ziada ya Marekani ya dola bilioni 1.8 kwa juhudi za misaada duniani, akisema inakuja wakati muhimu ambapo mahitaji yanaongezeka huku ufadhili ukipungua. Katika taarifa rasmi, Tom Fletcher amesema msaada huo mpya utawezesha kuokoa maisha ya mamilioni ya watu waliokumbwa na migogoro mbalimbali duniani.

“Ninaungana na Katibu Mkuu kuishukuru Marekani kwa ahadi yake ya ziada ya dola bilioni 1.8 kwa jamii ya misaada ya kibinadamu,” amesema Fletcher alisema. “Katika wakati ambapo mahitaji yanaongezeka na ufadhili unapungua, msaada huu utasaidia kuokoa maisha ya mamilioni ya watu.”

Mageuzi ya kibinadamu yapata kasi kwa msaada

Fletcher amesema ufadhili huo unaongeza nguvu kwenye mpango wa awali wa Marekani wa dola bilioni 2 uliotangazwa Desembam waka jana, ambao ulisaidia kuimarisha shughuli za misaada zilizokuwa katika hatari ya kusimama katika majanga mbalimbali. Alisema mpango huo uliimarisha mageuzi yanayojulikana kama “Humanitarian Reset,” yanayolenga kuongeza kasi ya utoaji misaada, uwajibikaji na kipaumbele kwa walio hatarini zaidi.

“Tulichukua hatua haraka,” amesema Fletcher. “Dola bilioni 1.68 ziligawiwa kwa misaada ya kibinadamu yenye misingi ya haki, usawa na mahitaji halisi katika migogoro 18, na kufikia zaidi ya watu milioni 22 kwa msaada wa kuokoa maisha. Zaidi ya asilimia 90 ya msaada huo umeelekezwa kwa walio katika hali mbaya zaidi.”

Ameongeza kuwa muda wa ugawaji wa fedha umepunguzwa kwa nusu ili kuhakikisha misaada inawafikia watu haraka zaidi, huku akisisitiza kuwa mgawanyo wa fedha zote unaweza kufuatiliwa mtandaoni ili kuongeza uwazi na uaminifu. “Tuko katika wakati mgumu sana,” alionya, “tumezidiwa, tuna rasilimali chache, na pia tunashambuliwa zaidi hata hivyo tumeonesha kwamba tunaweza kutoa huduma hata katika mazingira magumu zaidi.”

Mageuzi ya UN yapanuka zaidi ya misaada ya dharura

Waltz pia amehusisha mabadiliko hayo ya kibinadamu na mageuzi mapana ya Umoja wa Mataifa, yakiwemo kupunguzwa kwa bajeti ya kawaida ya Umoja wa Mataifa, kupunguza gharama za uendeshaji, na mapitio ya baadhi ya operesheni za kulinda amani ambazo Marekani inaona hazifanyi kazi ipasavyo. Amesema lengo ni kuirejesha Umoja wa Mataifa kwenye majukumu yake ya msingi kama uokoaji wa maisha na ufanisi wa operesheni za amani.

“Umoja wa Mataifa lazima ubadilike. Uwe mwepesi, wenye uwajibikaji zaidi na ulio karibu na watu unaowahudumia,” amesema Waltz, akisisitiza kuwa mageuzi hayo yanaendana na vipaumbele vya Marekani chini ya Rais Dolnad J. Trump.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *