
Tathmini ya siri iliyofanywa na shirika la kijasusi la Marekani, CIA, imebaini kuwa washirika wa Marekani katika eneo la Ghuba ya Uajemi wamegawanyika kuhusu iwapo waunge mkono vita vipya dhidi ya Iran.
Kwa mujibu wa vyanzo vinavyoifahamu tathmini hiyo, jarida la Capital & Empire limeripoti kwamba baadhi ya nchi za pwani ya Ghuba ya Uajemi zinataka vita, huku nyingine zikiona diplomasia kuwa njia bora na zinasita kutoa uungwaji mkono wa kisiasa ambao Marekani na Israel zinauhitaji ili kuanzisha mashambulizi mapya ya kijeshi dhidi ya Iran.
Tathmini hiyo imebainisha kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain zingependelea kuendelea kwa mashambulizi dhidi ya Iran, licha ya kuwa tayari zilikumbwa na mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka Iran wakati wa vita vya siku 40 vilivyotokea hivi karibuni.
Matokeo ya jumuiya ya ujasusi wa Marekani yanaendana pia na tathmini ya Trita Parsi, mtaalamu wa uhusiano kati ya Marekani na Iran.
Amesema kuwa UAE na Bahrain zina hofu kwamba ikiwa Marekani itafikia makubaliano na Iran, zitaachwa zikikabiliana na Iran iliyo na nguvu zaidi bila kuwa na uungwaji mkono madhubuti wa Marekani.
Kwa mujibu wa tathmini ya CIA, Saudi Arabia, Qatar na Kuwait kwa upande mwingine sasa zinaunga mkono mazungumzo kati ya Marekani na Iran.
Parsi amesema: “Saudi ilishajiisha sana vita hivi dhidi ya Iran, lakini sasa imeanza kujuta.”
Aidha, tathmini hiyo imegundua kuwa Oman, ambayo ina uhusiano wa kirafiki na Iran, inapinga hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya Iran pamoja na “kizuizi cha kijeshi cha majini” cha Marekani dhidi ya nchi hiyo.
Uchokozi haramu wa Marekani na Israel dhidi ya Iran ulianza tarehe 28 Februari kwa mashambulizi ya anga yaliyosababisha kuuawa kwa maafisa wakuu na makamanda wa Iran.
Nchi za pwani ya Ghuba ya Uajemi zilitoa ruhusa kwa tawala hizo mbili vamizi kutumia ardhi na anga yao kuanzisha mashambulizi dhidi ya Iran.
Jeshi la Iran lilijibu kwa kutekeleza mawimbi 100 ya mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyolenga maeneo nyeti na ya kimkakati ya Marekani na Israel kote katika eneo hilo.
Tarehe 8 Aprili, baada ya siku arobaini za vita, usitishaji wa mapigano wa muda uliosimamiwa na Islamabad ulianza kutekelezwa. Hata hivyo, duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya Tehran na Washington ilishindwa kufikia makubaliano kutokana na madai makubwa yaliyowasilishwa na Marekani.